Virusi vya corona: Kwanini bado watu wanakusanyika kuabudu?

Waumini wakisali

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Waumini wakisali

Makundi ya kidini katika sehemu mbali mbali duniani yamekuwa yakikataa ushauri wa kisayansi wa kutotangamana kwa sababu ya hatari ya maambukizi ya virusi vya corona.

Sasa mshauri maalum ya Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa dini au imani, Dk Ahmed Shaheed, anahimiza serikali "kuzuia udhihirisho fulani wa imani ya kidini wakati unapokuwa tishio kwa afya ya Umma" - hatua ambayo anasema sheria za kimataifa zinaruhusu.

Akiongea na BBC, Ahmed Shaheed alisema anaamini viongozi wa dini pia wanahitaji kuchukua jukumu katika kuhamasisha watu kutotangamana.

Alisema "watendaji wa kiimani wana jukumu - ikiwa sio jukumu la kisheria - kuhakikisha kwamba pia wanakuza ustawi wa jamii."

Kufanya ibada ingawa kuna maambukizi ya Covid-19

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mwanamke akiwa anaimba huku amevalia Barakoa

Wakati Wakristo wengi hivi karibuni waliadhimisha Pasaka bila uwepo wa wengine, makanisa kadhaa huko Marekani walifanya ibada za kibinafsi.

Mchungaji wa Louisiana Tony Spell aliripotiwa akidai watu elfu moja walihudhuria ibada ya Jumapili ya Pasaka katika Kanisa lake la Life Tabernacle, licha ya Gavana kupiga marufuku mikusanyiko ya watu zaidi ya 50.

Huko Pakistan idadi ya viongozi wa dini ya Kiislam wanapuuza marufuku ya serikali kuhusu mkusanyiko wa watu watano na zaidi.

Nchi inaanza kupunguza baadhi ya vizuizi na kuna wito kutoka kwa viongozi wengine wa dini kwa watu kuruhusiwa kukusanyika ili kusali, haswa wakati wa Ramadhani.

Waziri Mkuu Imran Khan anasema atajadiliana na viongozi wa dini kujua ni hatua gani zinazopaswa kutumika wakati wa mwezi mtukufu.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Raia wa Pakistan wakifanya ibada

Baadhi ya watu walioambukizwa Covid-19 nchini Pakistan wamehusishwa na watu wanaorudi kutoka hija huko Mashariki ya Kati, na mikusanyiko ya kikundi cha wamishonari wa Kiisilamu Tablighi Jamaat.

Hafla za Tablighi Jamaat pia zimehusishwa na maambukizi nchini India, Indonesia, na Malaysia.

Huko Korea Kusini, maelfu ya watu wameambukizwa, ambao wengi wamehusishwa na Kanisa la Shincheonji.

Kikundi hicho katika wiki za hivi karibuni kimeomba msamaha kwa namna walivyowajibika katika kushughulikia janga hili, na kinasema kimekuwa kikishirikiana na serikali. Lakini maafisa wanasema baadhi ya wanachama wake bado wanakataa kupimwa.

Wanasayansi na wataalamu wa matibabu wameonya mara kwa mara kwamba mkutano katika vikundi unaweza kueneza ugonjwa zaidi, na inaweza kuhatarisha maisha ya watu.

Kwa hivyo ni nini kinachowachochea kukusanyika ili kuabudu licha ya maonyo?

Suala la kuamini

Bastiaan Rutjens ni mwanasaikolojia wa Uholanzi anayebobea katika mifumo ya dini na imani.

Anasema jinsi watu wanavyoona serikali inashawishi jinsi watu wanavyofuata ushauri rasmi, akisema kwamba huko Marekani "kuna hali ya kutoaminika kwenye jimbo''.

"Watu wengine wanapambana sana na kufuata ushauri wa Serikali - kwa sababu hawaamini Serikali yenyewe kwa kuanzia."

Rutjens anaamini hii inamaanisha kuwa watu hao basi wana uwezekano mdogo wa kuwaamini wataalam wanaohusishwa na serikali, kama wanasayansi na wataalamu wa matibabu.

Kumfuata kiongozi wako

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Wakati mwingine ni kichwa cha serikali kuhamasisha watu kukusanyika kwa ibada.

Rais wa Tanzania John Magufuli amewahimiza raia wake kuendelea kwenda makanisani na misikitini.

Ingawa nchi haijachukua hatua za kutotoka nje, shule zimefungwa na mikusanyiko mingine ya umma imepigwa marufuku.

Sheikh Hassan Said Chizenga ni msemaji wa Mufti wa Tanzania.

Anakubaliana na maoni ya Rais, akisema "sala unayoifanya msikitini ni bora mara 27 kuliko [ombi] unaloomba nyumbani kwako".

"Kwa hivyo, kutekeleza hilo ni muhimu kwa sababu tunaomba na tumwombe Mwenyezi Mungu atusaidie kuvishinda virusi."

Lakini amri ya kutochangamana ikitolewa, Sheikh Chizenga anasema shirika lake - Baraza la Kitaifa la Waislamu Tanzania - litaheshimu hilo.

Kwa sasa, Sheikh Chizenga anasema misikiti inatoa huduma fupi za ibada na imewataka watu waende na mikeka yao ya sala.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Makanisa yameendelea kuwa wazi

Uhuru wa dini

Kuweza kukusanyika kwa ibada pia kumezungumziwa kama suala la uhuru wa kidini.

Lakini Ahmed Shaheed wa UN anasema uhuru wa kidini una mipaka.

"Nadhani katika hatua hii ni ngumu sana kubadili [tabia] isipokuwa kwa kanuni kali." anasema.

"Jambo la muhimu zaidi ni kuhakikisha kuwa serikali ulimwenguni kote zinawasiliana waziwazi, kwa kushawishi na kwa mamlaka juu ya hali hii." anasema mwanasaikolojia wa Uholanzi.

"Watu wanahitaji kuhisi serikali inadhibiti, na watu wanahitaji kutegemea wataalam wanaofahamisha serikali."