Viusi vya corona: Runinga ya Citizen nchini Kenya yasikitika kumuita rais Magufuli 'mkaidi'

rais Magufuli
Maelezo ya picha,

rais Magufuli

Runinga yenye watazamaji wengi nchini Kenya imesema katika taarifa iliotangazwa katika chumba hicho cha habari kwamba inajuta kumuita rais Magufuli 'mkaidi' , katika ripoti yake iliozungumzia kuhusu sera zake katika kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona.

Tanzania haijaweka masharti makali kuhusu mikutano ya watu kama ilivyofanywa na mataifa mengine duniani.

Katika ripoti hiyo ya runinga ya Citizen iliopeperushwa hewani tarehe 22 mwezi Machi , bwana Magufuli alinukuliwa akisema kwamba mlipuko wa virusi vya Covid-19 haufai kutumiwa kama sababu ya kuathiri uchumi wa Tanzania.

Runinga hiyo inayopeperusha matangazo yake katika eneo la Afrika Mashariki , ilisema katika ripoti hiyo kwamba haikuwa na madhumuni ya kuwapotosha raia wa Tanzania.

Taarifa hiyo ilisema :

Tunanukuu: Tarehe 22 Machi , tuliripoti kuhusu mipango iliowekwa na serikali ya Tanzania kukabiliana na janga la virusi vya corona. Katika ripoti hiyo tulimuita rais Magufuli 'mkaidi'.

Tunanukuu ujumbe: Katika mahojiano na runinga ya Citizen , balozi wa Tanzania nchini Kenya alisema kwamba Magufuli anaunga mkono juhudi za kieneo na kimataifa kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona .

Tunanukuu ujumbe: Utumizi wa neno 'mkaidi' dhidi ya rais Magufuli hauna msingi .

Idadi ya wagonjwa Tanzania yafikia 88 baada ya wengine 29 kuthibitishwa

Serikali ya Tanzania ilithibitisha wagonjwa 29 wapya wa virusi vya corona siku ya Jumatano .

Kulingana na taarifa ya wizara ya Afya nchini humo wagonjwa 26 kati yao wapo katika mji wa Dar es Salaam huko wawili wakipatikana mjini Mwanza na mmoja akiwa katika eneo la Kilimanjaro.

Waziri wa Afya Ummi Mwalimu alisema kwamba ufuatilianaji wa watu waliokaribiana na wagonjwa hao unaendelea.

Hatahivyo waziri huyo alitangaza habari njema akisema kwamba hadi kufikia Jumatano takriban watu 11 wamepona virusi hivyo lakini akaongezea kwamba watu wanne walifariki.

Ongezeko hilo la wagonjwa linajumlisha wagonjwa wapya sita waliotangazwa na waziri wa Afya wa kisiwa cha Zanzibar.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Raia wa Tanzania wanaruhusiwa kukongamana katika maeneo ya kuabudu

Idadi ya wagonjwa wa Corona Zanzibar yaongezeka

Waziri wa Afya kisiwani Zanzibar Hamad Rashid Mohammed alitangaza kifo cha kwanza cha mgonjwa wa corona kisiwani humo.

Kulingaana na waziri huyo mwathiriwa ni mwanamume mwenye umri wa miaka 63 mwenyeji wa kijiji cha kijichi aliyefariki Jumamosi iliopita na kuzikwa saa chache baadaye.

Aidha pia alitangaza wagonjwa wengine sita wapya wakiwemo wanaume watano na mwanamke mmoja wote raia wa Zanzibar.

Wote wamethibitishwa kukosa historia ya kusafiri nje ya nchi.

Dar es Salaam yabuni vituo vya kukusanya sambuli za corona.

Wakati huohuo vita dhidi ya maambukizi ya corona vimeimarishwa baada ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kutangaza vituo vya Afya na hospitali ambapo wakaazi watepeleka sampuli zao za ili kupimwa virusi vya corona.

Mkuu huyo anasema kwamba lengo la vituo hiyo ni kuzuia maabukizi ya virusi hivyo hususan wakati huu ambapo kumekuwepo na ongezeko la wagonjwa.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Vipimo vya Umma kufanyika Tanzania

Makonda amesema kwamba hatua hiyo inajiri baada ya wakaazi walio na dalili za virusi kuingia katika vituo vya Afya na kujichanganya na wengine bila kujua.

Baadhi ya vituo vilivyochanguliwa katika wilaya ya Kinondoni ni Hospitali ya Mwananyamala, Kituo cha Afya cha Mgomeni, Kituo cha Afya cha Mikoroshoni, kliniki ya IST Masaki, Hospitali ya TMJ Mikocheni pamoja na Hospitali ya Rabininsia eneo la Wazo.

Katika Wilaya ya Ilala vituo hivyo ni Hospitali kuu ya Amana , Hospitali ya Mnazi mmoja, Hospitali ya Buguruni, Hospitali ya Regency, Hospitali kuu ya Muhimbili, Hospitali ya Aga Khan, na Hospitali ya Hindu Mandal.

Katika Wilaya ya Temeke, wakaazi watapeleka sampuli zao katika hospitali kuu ya Temeke.

Mbagala Hospitali ya Rangi Tatu. Kituo cha Afya cha Yombo, na Hospitali ya TOHS Chan'ombe.

Wilaya ya Ubungo wakaazi wametakiwa kwenda katika hospitali ya Sinza , Kituo cha afya cha Kimara, Hospitali ya Bochi na hospitali maalum ya Mloganzila.

Nao wakaazi wa Wilaya ya Kigamboni watapeleka sampuli zao katika kituo cha Afya cha Vijibweni, Hospitali ya Aga Khan na kituo cha Afya cha Kigamboni