Virusi vya Corona: Simulizi ya muuguzi ambaye hushuhudia saa za mwisho za wagonjwa wa corona

Nurse by a bed in a ICU

Chanzo cha picha, INA FASSBENDER / AFP

Kupata huduma ya mashine ya kusaidia upumuaji (Ventileta) inaweza kumaanisha tofauti kati ya maisha na kifo kwa wagonjwa walio mahututi kutokana navirusi vya corona. Lakini wakati mwingine hata mashine hizi za kupumua haziwezi kuokoa maisha ya mtu.

Kuzima mashine hizi ni sehemu ya majukumu ya Juanita Nittla.

Yeye ni Muuguzi mkuu kwenye kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ya Royal Free jijini London, na amekuwa akifanya kazi katika hospitali ya taifa kama mtaalamu wa huduma kwa wagonjwa mahututi kwa kipindi cha miaka 16 iliyopita.

Kazi hii inatesa mno kisaikolojia inaumiza mno, anasema mhudumu huyu mwenye miaka 42. ''Wakati mwingine ninahisi kama nahusika na kifo cha mtu.''

Mashine za upumuaji huchukua nafasi ya mfumo mzima wa upumuaji wa mwanadamu iwapo virusi vya corona vitasababisha mapafu kushindwa kufanya kazi. Mashine hii humpa mgonjwa nafasi ya kupambana na maambukizi, lakini wakati mwingine mashine hii haitoshi.

Jopo la matabibu hukabiliana na uamuzi mgumu kuhusu muda wa kusitisha kazi ya mashine hiyo kwa wagonjwa ambao hawapati nafuu. Uamuzi hufikiwa baada ya kufanya uchunguzi wa kujiridhisha, kutathimini sababu mbalimbali kama vile umri wa mgonjwa, maradhi mengine ya muda mrefu waliyonayo jinsi wanavyopambana na virusi na uwezekano wao wa kupona.

Chanzo cha picha, Juanita Nittla

Maelezo ya picha,

Kuzima mashine ya ventileta ni sehemu ya majukumu ya Juanita Nittla.

Mwanzo wa zamu ya alfajiri katika wiki ya pili ya mwezi Aprili, Bi Nittla aliambiwa na msimamizi wa ICU kuwa kazi yake ya kwanza itakuwa kusitisha tiba kwa muuguzi mwenye miaka 50 aliyeathirika na virusi vya corona

Vikwazo vilivyokuwepo wakati huo ilimaanisha kuwa alipaswa kuzungumza na binti wa mgonjwa huyo kwa njia ya simu kumueleza kitakachotokea (kwa kuwaWaziri wa Afya nchini humo, Matt Hancock alisema kuwa ndugu wa karibu na familia watakuwa na nafasi ya kushuhudia na kumuaga ndugu yao kabla ya kuaga dunia, maelekezo mapya kuhusu wagonjwa wa corona walio katika hali mbaya)

''Nilimhakikishia tena kuwa mama yake hakuwa katika maumivu na alionekana kuwa sawa,'' Bi Nittla alisema. ''pia nilimuuliza kuhusu matakwa ya mama yake na hitaji la imani yake ya dini.''

Mgonjwa wa Bi Nittla alikuwa katika eneo la vyumba vinane, alizungukwa na watu ambao pia walikuwa hawajitambui.

"Nilifunga mapazia na kuzima kengele zote."

Timu ya matabibu ilisimama kwa muda na wakaacha kuongea, na Bi Nittla akaweka simu karibu na sikio la mgonjwa, na akamuomba binti yake azungumze.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Ventileta - mashine iliyopo kushoto mwa picha - husaidia wagonjwa mahututi kupumua

Bi Nittla alipiga muziki ambao familia iliomba. Kisha akazima mashine.

''Nilikaa pembeni yake, nikiwa pembeni yake nimeshika mikono yake mpaka alipofariki,'' alisema.

Mgonjwa alifariki katika kipindi si chini ya dakika tano baada ya Bi Nittla kuzima mashine ya kumsaidia kupumua.

''Nilitazama taa za mashine zikiwaka na mapigo ya moyo yakionekana kwenye mashine yakigonga alama sifuri kwenye skrini,'' alisema. Bi Nittla aliondoa mipira iliyokuwa ikimpatia dawa mgonjwa.

Binti wa mgonjwa bado alikuwa akizungumza na mama yake akisali kwenye simu. Bi Nittla alinyanyua simu kumwambia kuwa sasa basi imekwisha.

''Kwa msaada wa mfanyakazi mwenzangu, nilimsafisha na kumfunga kisha kumuhifadhi kwenye mfuko maalum wa kuhifadhia miili. Niliweka ishara ya msalaba kwenye paji lake la uso kabla ya kuufunga mfuko,'' alisema.

Kuweweseka

Bi Nittla anasema kuwa kuweza kushughulika na watu walio katika hali ya kufa kumemsaidia sana kuweza kuendelea kulichukulia kawaida janga hili.

Kutokana na idadi kubwa ya watu wanaofika kulazwa, kitengo cha wagonjwa mahututi kimepanuliwa kutoka vitanda 34 mpaka vitanda 60.

'' Kwa kawaida katika kitengo hiki huwa kuna utaratibu wa muuguzi mmoja kushughulika na mgonjwa mmoja. Sasa imekuwa muuguzi mmoja kwa kila wagonjwa watatu,'' anasema Bi Nittla.

''Ikiwa hali itaendelea kuwa mbaya, itakuwa muuguzi mmoja kwa kila wagonjwa sita.''

Baadhi ya wauguzi katika jopo lake wameonesha dalili ya kuwa na maambukizi na sasa wamejitenga.

Hospitali inawafunza wauguzi wengine ili waweze kufanya kazi katika kitengo cha wagonjwa mahututi.

''Kabla ya kuanza zamu huwa tunashikana mikono na kusema'baki salama'. Huwa tunalindana wenyewe kwa wenyewe. Tunahakikisha kila mmoja wetu anavaa glovu, barakoa na vifaa vya kujikinga vyema,'' anasema Nittla.

Chanzo cha picha, Juanita Nittla

Maelezo ya picha,

Bi Nittla anasema wauguzi wa ICU hujumuika pamoja na kutakiana kheri kabla ya kuanza kwa zamu

ICU hurekodi kifo kimoja kila siku, juu ya wastani waliokuwa wakirekodi kabla ya janga la corona.

''Inatisha ,'' anasema Bi Nittla.Kama muuguzi mkuu, wakati mwingine analazimika kuondoa hofu aliyonayo.

''Ninapata ndoto .Ninashindwa kulala.Nina hofu kuwa nitapata maambukizi.Kila mmoja ana hofu.''

Mwaka jana hakuwa kazini kwa miezi kadhaa baada ya kupata kifua kikuu. Anafahamu kuwa uwezo wake wa mapafu umedhoofu.

''Watu huniambia sitakiwi kufanya kazi lakini hili ni janga.Ninaacha kila kitu kando na kufanya kazi yangu,'' anasema.

''Mwishoni mwa zamu yangu ya siku huwa ninawaza wagonjwa waliofariki wakiwa chini ya uangalizi wangu, lakini huwa nafuta mawazo hayo ninapotoka nje ya jingo la hospitali.''

Tangu alipozungumza na BBC, Bi Nittla ametakiwa na mwajiri wake kubaki nyumbani, kutokana na hali yake ya kiafya. Amepanga kuendelea kutoa msaada kwa kufanya kazi za kuongoza,akifanya kazi akiwa nyumbani.