Virusi vya Corona: Rais wa Sierra Leone kujitenga baada ya mlinzi kuambukizwa virusi

Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio

Mlinzi wa Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio ameambukizwa virusi vya corona.

Rais wa nchi hiyo alitangaza siku ya Jumatatu usiku kuwa ana afya njema ingawa mfanya kazi wake ana maambukizi.

Amesema pia familia yake yote iko salama na hakuna aliyeonesha dalili za kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Rais Bio atakaa karantini kwa siku 14 kwasababu alikuwa karibu na mlinzi wake, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Umaru Fofana.

Sierra Leone mpaka sasa ina wagonjwa 43 wa virusi vya corona.

Botswana

Mwanzoni mwa mwezi Aprili Botswana ilisema kuwa inamuweka karantini Rais wa nchi hiyo pia wabunge, baada ya muuguzi ambaye alikuwa kwenye kikao maalumu cha bunge kukutwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi

Kikao hicho maalum kiliitishwa na Rais Mokgweetsi Masisi kutaka idhini ya kutangazwa hali ya hatari kwa miezi sita kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.

Lakini wabunge walishtushwa baada ya kugundua kuwa mhudumu wa afya aliyekuwa akiwapima virusi vya Covid-19 siku moja kabla alikutwa na maambukizi.

Rais Masisi alijitenga kwa siku 14 mwezi uliopita baada ya kusafiri kwenda nchi jirani ya Namibia.

Nigeria

Msaidizi mkuu wa Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari alikutwa na virusi vya corona.

Abba Kyari, akiwa na umri wa miaka ya 70 alikuwa mtu muhimu kwa Rais Buhari na serikali yake kwa ujumla.

Siku ya Jumamosi ofisi ya Rais Buhari Ilitangaza kifo cha Abba Kyari

Kyari alikuwa na historia ya maradhi mengine kama kisukari.