Virusi vya corona: Imamu na Askofu Tanzania waeleza kwanini wameamua kufunga nyumba za ibada

  • Ambia Hirsi
  • BBC News Swahili
Mikono imeshikilia msalaba

Chanzo cha picha, Getty Images

Nyumba za ibada nchini Tanzania zingali wazi tofauti na maeneo mengi ulimwenguni wakati huu wa janga la virusi vya corona.

Rais wa nchi hiyo John Pombe Magufuli ameruhusu makanisa na misikiti kusalia wazi ili watu waombe kwa imani zao dhidi ya virusi hivyo hatari.

Lakini, baada ya kasi ya maambukizi kuongezeka Imamu mmoja na Askofu mmoja nchini humo wamechukua hatua zao binafsi za kufunga nyuma za ibada.

Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo la Rulenge-Ngara amesitisha ibada zote za jumuiya katika jimbo lake huku Imamu Said Haroun kutoka mkoa wa Arusha pia amefunga msikiti anaoungoza.

Kufahamu kwa nini wamechukua hatua hiyo BBC imezungumza nao wote wawili.

Askofu anasema alichukua uamuzi huo ili kuwalinda waumini.

"Baada ya kujifunza kutoka kwa nchi jirani na nchi za Ulaya na Marekani tukiona jinsi virusi vinavyoteketea watu wengi sana na kwa muda mfupi.

Na maambukizi ya mgonjwa wa kwanza virusi vya corona, mkoani Kagera aliyekuwa anatokea Burundi alivyobainika katika eneo letu, tukaona ni busara kufunga makanisa.

Kwa sababu maambukizi mengi yanapitia katika mkusanyiko na watu na Afrika bado tuna imani sana, hivyo wanakuja sana kanisani hivyo tukaona kuwa ni bora kusitisha misa kwa muda.

''Si kwamba hatuna imani, au hatumpendi Mungu au hatumuamini hapana, ni kutokana na hatari iliyopo mbele yetu."

Chanzo cha picha, Getty Images

Naye Imamu Said Haroun wa mkoani Arusha anasema, alifikia uamuzi wa kufunga msikiti ili kuzuia maambukizi ya Corona.

"Hapa Arusha tuliamua kufikia hatua ya kufunga msikiti baada kuwepo kwa tetesi kuwa kuna wengi hawajapata vipimo na hivyo si rahisi kujua nani anaumwa.''

Na baada ya kuona mgonjwa wa kwanza ametokea mkoani kwetu na bado waumini hawafuati au hawazingatii maelekezo ya yaliyotolewa, tukaona ni vyema kufunga ili kuepusha madhara zaidi.

Tahadhari na njia ya kujikinga na ugonjwa huu bado haufuati, maisha ya waumini wetu ni muhimu zaidi ndio maana tumeamua kuchukua tahadhari mapema hata kama serikali haijatoa maelekezo.

Lakini Tanzania kumekuwa na siku tatu za kusali kwa muda wa siku tatu.

Askofu anasema anafurahi kuwa serikali yake inampenda Mungu na anashukuru kwa hilo lakini ni vyema kwa watu kusali nyumbani ili kujikinga na maambukizi.

''Kuna wakati kanisa lilipata shida na watu wakasali kwenye mahandaki lakini sasa mahandaki yetu yako kwenye nyumba zao, sehemu ya kukomunika ndio watakosa lakini neno la Mungu wanaweza kusali wakiwa nyumbani.'' alisema

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa waumini wa dini ya Kislamu siku ya Alhamisi ni siku muhimu sana katika kalenda ya kidini.

Alhamisi wiki hii inaashiria mwanzo wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, wakati ambao waumini wanatakiwa kufunga kula na kunywa kuanzia machwo hadi jioni jua linapotua.

Lakini mwaka huu kutokana na janga la Covid-19 lililokumba dunia nzima na kusababisha kufungwa kwa maeneo ya ibada ikiwa ni pamoja na kuzuru miji mitukufu ya - Mecca, Medina pamoja naeneo mengine duniani.

Nchini Tanzania Imam Said Haroun kutoka msikiti wa Msasani mjini Arusha ameamua kufunga msikiti wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

''Tunahofia janga la corona litawaathiri waumini wetu na njia pekee ya kukomesha maambukizi ni kufunga msikiti'' alisema Sheikh Harun

Huenda watu wengi wakapongeza hatua yake lakini swali ni je kwanini serikali ya Tanzania haijatoa amri kufungwa kwa sio tu misikiti lakini pia na maeneo mengi ya kuabudu?

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Waumini Wa Kiislamu wakiwa kwenye ibada

Akijibu swali la BBC Sheikh Harun alisema hatua yake imezingatia mafundisho ya dini ya kiislamu kwa sababu ni dini inayojali maslahi ya binadamu.

Hatua hiyo hata hiyo imepokelewa kwa hisia mseto. Anasema kuna wale ambao wanaunga mkono na wale wanaopinga lakini wametuoa mafunzo kwa umma na baadhi yapo wameelewa.

Sheikh Harun anasema Msikiti pia uliwahi kupata changamoto, na waislamu wakatakiwa kusali nyumbani hivyo si jambo geni kwa waislamu kusitisha kusali msikitini kwa ajili ya janga.

''Janga lishawahi kutokea hata wakati wa uhai wa Mtume Mohammad...na wakati huo Mtume aliwaambia maswahaba wake ikiwa mtu ameambukizwa ajitenge iliasiwaambukize watu wengine''

Aliongeza kuwa huenda serikali inasubiri kuona mikakati iliyoweka kama itafanya kazi lakini wao kama viongozi wa kidini waliafikiana kuchukua hatua kwa kuzingatia mafundisho ya Quran.

Aidha viongozi wote wawili wamesisitiza kuwa hawajakurupuka kuchukua maamuzi haya, hawaoni kuwa maamuzi yao hayakuwa sahihi.

Wanasema wataendelea kutoa maelekezo kwa waumini na uzuri mitandao inasaidia.

Bora waumini wajiombee wao wenyewe wakiwa nyumbani na waliombee taifa waikiwa nyumbani kwa wakati huu wa dharura.

Hatuazilizochukuliwa kudhibiti maambukizi ni zipi?

  • Shule zote na vyuo vya elimu vimefungwa mpaka itakapotangazwa ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya corona nchini humo.
  • Pamoja na kuzuia mikusanyiko yote ya watu wengi yakiwemo matamasha ya muziki, mikutano ya hadhara mbalimbali ikiwemo ya kisiasa.
  • Magari ya usafiri wa umma hatayakiwi kujaza abiria, na wote lazima wawe wameketi vitini.
  • Ndege za abiria zimezuiwa kutua nchini humo.
  • Kuanzia Jumatatu ya Aprili 20 ni lazima kwa wakaazi wote wa Dar es Salaam kuvaa barakoa wanapokuwa maeneo ya umma.
  • Biashara zote za chakula jijini Dar es Salaam zinatakiwa kufunga bidhaa zao na kutoruhusu watu kula kwenye migahawa.