Virusi vya Corona: Wagonjwa wapya 15 wathibitishwa Kenya

Dkt Mercy Mwangangi
Maelezo ya picha,

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Kenya Dkt Mercy Mwangangi ameonya juu ya virusi kuwagharimu zaidi vijana.

Wizara ya Afya nchini Kenya imetangaza ongezeko la wagonjwa 15 wapya waliothibitishwa kuwa na virusi vya corona na kufikisha 296 jumla ya watu wanaougua Covid-19 nchini humo.

Wagonjwa 11 ni raia wa Kenya na wanne ni raia wa kigeni ambao walikuwa miongoni mwa watu 545 waliofanyiwa vipimo vya kubaini ikiwa wana virusi vya ugonjwa huo katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Akizungumza na wanahabari Jumanne, Katibu mkuu wa wizara hiyo Dkt. Mercy Mwangangi amesema visa saba vya maambukizi vilirekodiwa Mombasa pwani ya Kenya, sita mjini Nairobi na viwili katika mji wa kaskazini mashariki wa Mandera.

''Hakuna hata mmoja kati yao aliyekuwa na amesafiri'' alisema na kuongeza kuwa watu sita kati yao walikuwa karantini na wengine tisa walipatikana kupitia mkakati wa serikali wa kuwatafuta watu wanaoshukiwa kuambukizwa baada ya kutangamana na watu waliathirika.

Dkt. Mwangangi apia alitangaza kuwa watu watano zaidi wametolewa hospitali baada ya kupona na kuongeza idadi ya watu waliopona kutokana na virusi vya corona kufikia 74.

Wizara ya Afya pia imezindua kampeini kwa jina 'Saa sita'.

Wakenya wameombwa kuungana kuwapa pongezi wahudumuwa afya kila siku ya Jumatano "saa sita''.