Virusi vya corona: Mwananume anayezika watu waliokufa kwa corona India

Health workers in PPE suits and family members perform funeral prayers before the burial of a coronavirus disease in Delhi.

Chanzo cha picha, Hindustan Times

Maelezo ya picha,

Mara nyingi wahudumu wa afya huwa wanahudhuria mazishi hayo kama hatua ya kuzia maambukizi ya corona

Kwa miongo mitatu, Abdul Malabari amekuwa akihifadhi miili ya watu ambao jamaa zao hawajajitokeza. Lakini hakuwahi kufikiria kwamba ipo siku atazika wengine ambao familia zao wangelipenda sana kuaga miili hiyo lakini haiwezekani kwasababu ya ugonjwa wa Covid-19. Mwanahabari wa BBC Gujarati's Shaili Bhatt anaelezea.

"Kazi yangu haina muda maalum," anasema mwanaume huyo, 51. "Punde tu ninapopigiwa simu, moja kwa moja tunatoka na vifaa vyetu."

Kila wakati mtu anapokufa kwa virusi vya corona huko Surat - magharibi mwa mji wa Gujarat - maafisa humuitwa Bwana Malabari. Hadi kufikia sasa mji huo umerekodi vifo 19 na wengine 244 wakithibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.

Idadi ya Gujarat imefikia 3,548.

"Wakati wa kipingi kigumu kama hiki, Abdul bhai [kaka yake] amekuwa wa msaada mkubwa," anasema Ashish Naik, Naibu kamishna wa eneo la Surat.

Bwana Malabari anasema hii ni kazi yake kwa hiyo amekubali kuifanya licha ya hatari iliyopo. Kwasasa hivi timu yake inakula na kulala katika ofisi yake ya kutoa msaada, ili kulinda familia zao dhidi ya maambukizi.

Siyo mara ya kwanza Bwana Malabari kujitoa kutenda makuu hata kwa watu asio wafahamu. Ukarimu wake ulijitokeza miaka thelathini iliyopita - pale ambapo ugonjwa usiokuwa wa kawaida ulipokuwa umejitokeza na kupelekea kile anachofanya hii leo.

Chanzo cha picha, NARINDER NANU

Maelezo ya picha,

Makaburi kote nchini India hunyunyiziwa dawa baada ya waliokufa kwa Covid-19 kuzikwa

Mtu huyo asiyemfahamu ni Sakina ambaye alikuwa na ugonjwa wa Ukimwi. Mume wake na kijana wake walikuwa wamempeleka hospitali lakini baada ya kupokelewa wakatoroka. Juhudi za kuwatafuta baada ya jamaa yao kufa hazikufua dafu.

Na hivyo basi Sakina akawa yupo kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kwa mwezi mmoja. Maafisa wa eneo walikuwa hawajui la kufanya na kutoa wito kwa Muislamu anayeweza kujitolea kumzika.

Bwana Malabari, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 21 pekee, aliguswa na tangazo hilo na kuamua kutoa msaada wake.

Akawasiliana na shirika la pekee huko Surat ambalo lilikuwa linazika miili ya watu ambao haijachukuliwa na jamaa zao lakini wakamwambia kwamba mwanamume anayefanya kazi hiyo anasafiri kwahiyo itabidi wamsubiri hadi atakaporejea.

Pia unaweza kusoma:

"Nilihisi kwamba sio sawa," Bwana Malabari anasema. Kwahiyo akaenda hospitali na kuwaarifu maafisa kwamba yeye mwenyewe atachukua jukumu la kumzika mwanamke aliyetorokwa na jamaa zao aliyefahamika kama Sakina.

Mwili wake, anakumbuka, ulikuwa unanuka. Lakini hilo halikumzuilia kutekeleza alichokusudia, na akazungumza na wanawake wengine ili waweze kuuosha mwili ule kwa kuzingatia utamaduni wa Kiislamu. Lakini walikataa, anasema, kwasababu Sakina alikuwa na ugonjwa wa Ukimwi ambao ufahamu wake miaka ya 1990, ulikuwa mchache mno.

Kwahiyo Bwana Malabari akaamua kufanya kazi hiyo mwenyewe, akamiminia mwili huo ndoo kadhaa za maji kabla ya kwenda kumzika.

Anasema hapo ndipo alipobaini kuwa mji wa Surat hauwezi kutegemea mtu mmoja kwa kazi hiyo.

"Ilinichukua siku nzima, na pia nikabaini kwamba siwezi kufanya kazi hii peke yangu."

Kwahiyo akaanza shirika lake la kutoa msaada. Anasema awali, familia yake, ambayo inaendesha kiwanda cha nguo ilipinga wazo hilo.

"Nakumbuka nikiwaarifu kwamba Dini ya Kiislamu inasema hilo ni jukumu la kil mmoja kusaidia kuhakikisha mtu anafanyiwa mazishi inavyostahiki kabla ya kuzikwa kama ubinadamu na heshima. Nilikuwa ninafanya hivyo kama mwanadamu mwengine yeyote."

Chanzo cha picha, Hindustan Times

Maelezo ya picha,

Mara nyingi wahudumu wa afya huwa wanahudhuria mazishi hayo kama hatua ya kuzia maambukizi ya corona

Maelezo ya picha,

Bwana Malabari amekuwa akizikwa watu asiowajua kwa miaka 30

Leo hii, watu wameingiwa na hofu kuhifadhi miili ya watu waliokufa kwasababu ya Covid-19 ingawa ukiangalia sababu zingine kama vile wataalamu wa afya wanavyosema kwamba virusi hivyo haviwezi kusambaa baada ya mtu kufa, japo vinaweza kuwa hai kwenye nguo kwa saa kadhaa.

Kwahiyo mwili ukishafungwa kwenye mfuko, hakuna mwengine hata familia wanaweza kuuona tena mwili huo.

Bwana Malabari na timu yake wanachukua tahadhari yote - wanavaa barakoa, gulavu na nguo maalum. Pia wameoneshwa namna ya kutayarisha miili.

Kwanza, wananyunyizia mwili kemikali na kisha wanaufunga kwa karatasi ya plastiki ili wasiambukizwe, kabla ya kuusafirisha kwa kutumia moja ya magari mawili maalum kusafirisha waathirika wa Covid-19. Magari hayo yananyunyiziwa vieuzi kila baada ya kutoka kuzika mtu, na eneo la makaburi pia linanyunyiziwa dawa baada ya mazishi.

Ingawa hayo yote yanafanyika, hofu dhidi ya virusi hivyo imesababisha maandamano katika baadhi ya miji nchini India na watu wanaishi karibu na makaburi.

Bwana Malabari anasema pia amekumbana na matatizo mengine lakini kuna baadhi ya watu ambo amefanikiwa kuzungumza nao na kuelewana.

Kigumu zaidi, anasema, ni kukabiliana na familia ambazo haziwezi kumuaga mpendwa wao - na wengi wao pia wameweka kwenye karantini.

"Wanalia mno na kuzungumzia kumuona jamaa wao aliyekufa. Tunajaribu kuwaarifu kwamba hilo haliwezekani kwasababu ya usalama wao na kuwahakikishia kwamba tutafanya maandalizi kulingana na utamaduni wa dini zao."

Anasema wakati mwingine mwanafamilia ameruhusiwa kutazama mazishi kwa mbali: "Tunawachukua kwa gari tofauti na kuwata wasimame kwa mbali na kuomba sala zao.

Chanzo cha picha, Hindustan Times

Maelezo ya picha,

India imekuwa ikitekeleza kanuni ya kutotoka nje tangu Machi 25

Pia mambo yamebadilika sana katika mji wa Surat tangu alipomzika Sakina miaka hiyo yote iliyopita.

Kwasasa, anasema, watoto wake watatu - msichana na wavulana wake wawili wanamuonea fahari. Shirika lake limekua na kufikia kuwa na wanachama 35 pamoja na wafadhili 1,500 pamoja na usaidizi kutoka kwa maafisa.

Anachofurahi kabisa, anaongeza ni kwamba timu yake inajumuisha watu wa imani tofauti tofauti. "Tuna tu wa dini ya Wahindu waliojitolea kuzika miili ya Waislamu, na Waislamu waliojitolea wanaochoma miili ya Wahindu."

Mara nyingi, anasema, wanaishia kuwa na miili ya wasiokuwa na makazi au waliogongwa barabarani ambao hawajawahi kutambuliwa na jamaa zao.

"Huwa tunapata miili kwenye mito na mifereji au njia za treni. Na wakati mwengine tunazika miili iliyooza."

Anasema athari za kile wanachofanya ni vugumu kukielezea, kwa miaka mingi, hilo limekuwa likimpa matatizo ya kulala, kutokuwa na hamu ya kula na pia uwezo wake wa kuwa na muda wa kufurahi na familia.

Lakini hajawahi kufikiria kuacha kazi hiyo.

"Moyoni mwangu, napata hisia ya kufurahhia kile ninachofanya na hakuna kinachoweza kunifanya niachane nayo."