Virusi vya Corona: Maswali yaibuka juu ya uwazi wa taarifa za corona Tanzania

Rais Magufuli

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Rais Magufuli amekemea tabia ya watu kufanya mzaha na kutisha wengine kupitia mitandao ya kijamii

Baada ya wiki moja ya ukimya, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa hii leo amethibitisha idadi ya wagonjwa wa corona nchini humo kufikia 480.

Kabla na hata baada ya Majaliwa kuzungumza hii leo, kumekuwa na mijadala mikubwa mitandaoni pamoja na wanasiasa wa upinzani ambao wamekuwa wakitilia shaka uwazi wa taarifa kutoka serikali ya nchi hiyo.

Tanzania ikiwa ni Muungano wa nchi mbili ina wizara mbili za Afya, moja ikishughulika na Zanzibar na nyengine ikishughulikia Tanzania Bara.

Mara ya mwisho kwa upande wa bara kutoa taarifa juu ya maambukizi mapya na vifo ilikuwa ni Jumatano ya wiki iliyopita (Aprili 22) na toka hapo ndiyo taarifa mpya imetoka hii leo.

Ijumaa ya Aprili 24 Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wa Tanzania bara alitangaza wagonjwa 37 kupona. Kufikia sasa idadi rasmi ya waliopona nchini humo ni 167.

Kwa upande wa pili wa Zanzibar umetangaza takwimu mpya za maambukizi mara mbili, Ijumaa ya wiki iliyopita wagonjwa 15 na Jumanne wiki hii wagonjwa saba.

Idadi rasmi ya vifo iliyotangazwa leo ni 16 huku Waziri Mkuu Majaliwa akisisitiza kuwa si wote wanaokufa ni kutokana na corona.

Hali hiyo imepokelewaje?

Hayo yanajiri huku katika siku za hivi karibuni watu pamoja na wanaharakati wakituma picha za video mitandaoni zikionesha wanaodaiwa kufariki kutokana na corona wakizikwa nchini humo, hali inayozua wasiwasi kwa baadhi ya watu kuwa kuna ongezeko la wagonjwa na vifo ambavyo havijaripotiwa rasmi.

Mwandishi wa habari na mwanaharakati nchini Tanzania Bi Maria Sarungi kupitia mtandao wake wa Twitter kabla ya Waziri Mkuu kutangaza takwimu mpya alisisitiza kuwa wananchi wanaweza kuhimili ukweli.

"Watanzania siyo watoto, na ni wazo potofu kudhani kuwa kuficha takwimu eti inasaidia kutotupa hofu! Kimya huzidisha hofu kwa sababu ni dhahiri ugonjwa wa #coronavirus unaleta athari zilizowazi katika jamii! Tuambiwe ukweli…" ameandika Bi Sarungi.

Baada ya Majaliwa kuzungumza akaandika: "Safi, ni vyema kuendelea kutoa takwimu - hili ni jambo muhimu sana! MSIACHE!..."

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini humo cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe ambaye amekuwa akilizungumzia janga la corona mara kwa mara ameiambia BBC kuwa uwazi wa takwimu ni jambo muhimu katika mapambano dhidi ya janga hilo.

"Ni haki ya kikatiba wananchi kupewa taarifa muda wote (Ibara ya 18 ya katiba). Serikali inawanyima Wananchi Taarifa muhimu kwa ajili ya kujikinga na maambukizi jambo ambalo ni kosa kubwa…"

Maelezo ya picha,

Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania Zitto Kabwe ameonya bila uwazi janga la Covid-19 litasalia kwa muda mrefu nchini humo.

Bwana Kabwe ameeleza kuwa kuna mapungufu; "Takwimu za Tanzania Bara kwanza zina mapungufu ya kutosema idadi ya watu waliofanyiwa vipimo. Pili hazisemi wagonjwa wapo maeneo gani ya miji. Tatu zinatolewa kwa kuchelewa…"

"Sitaki kuhisi kuna kitu kinafichwa. Nataka Serikali itimize wajibu wake... Hivi sasa tuna shuhudia misiba mingi, mazishi ya watu usiku usiku na hata miili ya watu mitaani. Bila kuwa wawazi wananchi watapata hofu kubwa na kusababisha maafa zaidi...Bila uwazi tutakuwa na Covid 19 kwa muda mrefu sana hapa Tanzania."

Kumekuwa na mfululizo wa vifo vya watu maarufu nchini Tanzania ijapokuwa sababu ya vifo vyao kutosemwa kuwa ni corona kumekuwa na mjadala wa hatua za tahadhari ambazo zimekuwa zikichukuliwa kwenye mazishi yao.

Mathalani, mazishi ya mbunge wa viti maalumu na Mchungaji Getrude Lwakatare pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evod Mmanda yalifanyika chini ya usimamizi wa serikali na tahadhari kubwa zilichukuliwa. Taarifa rasmi zilizotolewa ni kuwa viongozi wote hao waliumwa kwa kipindi kifupi.

Maelezo ya picha,

Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameonya juu ya upotoshaji wa takwimu mitandaoni

Pia kumekuwa na picha za video kadhaa mitandaoni zikionesha kuzikwa kwa watu kwa tahadhari kubwa usiku.

Hata hivyo Waziri Mkuu Majaliwa ameonya juu ya upotoshaji wa takwimu mitandaoni.

"…kwa sasa kumeibuka tabia ya watu kutoa takwimu ambazo sio sahihi ambazo zinasababisha mtafaruku ndani ya jamii usiokuwa wa lazima na mimi nataka nieleze pia kuwa uzushi wa vifo wa kwamba kila kifo ni cha corona sio sahihi sana tunasahau kwamba kuna magonjwa mengine yanayoua pia. Tunajua tuna magonjwa kama vile BP, malaria kisukari, ukimwi na magonjwa mengine pia ambayo yanaua."

"Idadi ya wanaokufa tuwaachie madaktari watuambie badala ya kila mmoja kusema anachokiona yeye. Tuache tabia ya kupotosha umma, tuwaache wataalamu wetu waendelee na kazi yao na watupe taarifa ili sisi tuwafikishie. Jukumu letu bado lipo palepale la kuhakikisha serikali inasimamia afya ya watanzania…"amesisitiza majaliwa.

Jumatano ya Aprili 22 rais John Pombe Magufuli pia alizungumza na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi hiyo na kugusia juu ya takwimu na vifo.

"…hizi takwimu za wagonjwa wanaopona nazo zitangazwe ili wananchi waondoe hofu ya kwamba ukipata ugonjwa huu lazima ufe…kwa taarifa nilizonazo mpaka sasa wamekufa watu 10, hivyo si kweli kuwa kila anayekufa ni corona."

Tanzania kukosolewa na WHO

Alhamisi ya wiki iliyopita, kiongozi mwandamizi wa Shirika la Afya Duniani- WHO aliikosoa Tanzania kwa kuchelewa kuchukua hatua za mapema kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo.

Tarehe 24 Aprili Mkuu wa WHO wa bara la Afrika Bi Matshidiso Moeti alisema kumekuwa na hofu juu ya kukua kwa kasi ya maambukizi katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

"Kwa hakika tumeona kuwa watu kuacha kutangamana, pamoja na kupiga marufuku kwa mikusanyiko ya watu wengi kumechukua muda mrefu kufanyika na tunaamini kuwa hayo yanaweza kuwa ni moja ya mambo yaliyosababisha ongezeko la kasi la wagonjwa wa corona," alisema Dkt Moeti katika mkutano na wanahabari.

Tanzania pia imekosolewa kwa msimamo wa rais Magufuli wa kuendelea kuruhusu nyumba za ibada kuwa wazi. Hata hivyo baadhi ya viongozi wa dini nchini humo wamechukua hatua binafsi za kufunga maeneo yao ya ibada kwa hofu ya kusambaza maambukizi ya corona.

Licha ya jiji la Dar es Salaam kuwa ni kitovu cha maambukizi nchini humo Rais Magufuli amepingana na rai za kulifunga jiji hilo.

"Wapo wengine wanatoa mawazo ya kuifunga Dar es Salaam, hili haliwezekani. Dar es salam ndio centre (sehemu) pekee ambapo collection (makusanyo) ya revenue (mapato) inapatikana kwa nchi yetu...Zaidi ya asilimia 80 ya mapato yanakusanywa Dar es Salaam," alisema Magufuli Jumatano Aprili 22.

Pia alisisitiza kuwa kutokana na wingi wa wakaazi wake, ilikuwa ni jambo la kutegemewa kitakwimu kwa jiji hilo kuwa na wagonjwa wengi zaidi.

Hatua zilizochukuliwa kudhibiti maambukizi ni zipi?

  • Shule zote na vyuo vya elimu vimefungwa mpaka itakapotangazwa ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya corona nchini humo.
  • Pamoja na kuzuia mikusanyiko yote ya watu wengi yakiwemo matamasha ya muziki, mikutano ya hadhara mbalimbali ikiwemo ya kisiasa.
  • Magari ya usafiri wa umma hatayakiwi kujaza abiria, na wote lazima wawe wameketi vitini.
  • Ndege za abiria zimezuiwa kutua nchini humo.
  • Kuanzia Jumatatu ya Aprili 20 ni lazima kwa wakaazi wote wa Dar es Salaam kuvaa barakoa wanapokuwa maeneo ya umma.
  • Biashara zote za chakula jijini Dar es Salaam zinatakiwa kufunga bidhaa zao na kutoruhusu watu kula kwenye migahawa.