Virusi vya corona: Idadi ya walioambukizwa Kenya sasa yafikia 535

Mutahi Kagwe

Chanzo cha picha, Ministry of Health Kenya/Twitter

Maelezo ya picha,

Waziri wa Afya wa Kenya Mutahi Kagwe

Kenya imerekodi viwango vya juu vya maambukizi ya virusi vya corona kwa siku baada ya wagonjwa wapya 45 kuthibitishwa leo na kufikisha 535 jumla ya watu waliopatikana na ugonjwa wa Covid -19.

Bw. Kagwe amesema wagonjwa hao wamepatikana baada ya sampuli 1,077 kufanyiwa uchunguzi katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Wagonjwa 29 wote walithibitishwa kuwa wa Nairobi,wanatokea mtaa wa Eastleigh, huku wengine 11 wakiwa ni wa Mombasa na wangine watano wakitokea Wajiri kaskazini mwa Kenya.

Wizara ya Afya pia imetangaza kuwa wagonjwa tisa ambao walikuwa wameambikizwa wamepona na kufukisha 182 watu waliopona kutokana na maradhi hayo.

Katika juhudi za kudhibiti maambukizi Kenya bado inaendeleza marufuku ya watu kutotoka nje kuanzia saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri.

Marufuku ya usafiri kuingia na kutoka mji kuu wa Nairobi na miji mingine kama vile Madera ,Mombasa, Kilifi na Kwale pwani ya Kenya pia iliwekwa kukabiliana na maambukizi.

Maelezo ya picha,

Katika juhudi za kudhibiti maambukizi Kenya bado inaendeleza marufuku ya watu kutotoka nje kuanzia saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri.

Hivi karibuni hata hivyo Wizara ya Afya iliweka masharti mapya ya uendeshaji migahawa Kenya.

Wizara hiyo ilisema kuwa itaruhusu migahawa kuanza kufunguliwa kuanzia saa 11 asubuhi na 10 jioni.

Watakaoingia kuhudumiwa watahitajika kufuata utaratibu uliopo wa kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono na kuvaa barakoa kama kawaida. Hatua ya kutokaribiana itaendelea kutekelezwa umbali wa mita 1 baina ya mtu mmoja hadi mwengine.

Lakini watakaoruhusiwa kutoa huduma ni wale watakaokuwa wamepimwa pekee.

Pia kulingana na wizara ya afya, katika migahawa hiyo, huduma ya kujiwekea chakula bado imesitishwa.

Wizara hiyo imetoa agizo la watu wote wanaoingia migahawani kupimwa kiwango cha joto na kuruhusiwa tu kuingia ikiwa litakuwa chini ya nyuzi 37.5 na mgahawa husika kuarifu wizara mara moja kuhusu mtu atakayepatikana akiwa na kiwango ha juu zaidi ya hicho, kwa kupiga simu kupitia nambari 719 ili kupata mwongozo zaidi.

Bwana Kagwe aliwataka raia wote wa Kenya kuendeleza nidhamu na kuchukua jukumu wao wenyewe binafsi katika juhudi za kubabiliana na janga hili.

"Hali ya Kenya itabadilika kwasababu yako wewe. Ikiwa tutajuchukua jukumu kama watu binafsi, bila shaka tutakabiliana na virusi hivi," Kagwe amesema.

Waziri pia amegusia kwamba sasa Wakenya wameanza kutekeleza sheria na kanuni zilizowekwa na serikali upande wa usafi.

"Visa vya matatizo ya tumbo vimepungua tena pakubwa, visa vya kuharisha vimepunga," waziri kagwe amesema.

Katika kukabiliana na ugonjwa wa covid-19, serikali imeunda kamati 5 za kimkakati kutoa mwongozi wa njia zitakazofanikisha kenya kushinda vita hii.