Virusi vya corona: Shirikisho la kandanda Tanzania lajiandaa kuendelea kwa ligi

Magufuli

Chanzo cha picha, IKULU

Shirikisho la mpira wa miguu nchini Tanzania TFF pamoja na bodi ya ligi hiyo TPLB zinajiandaa kuendelea na ligi ya mchezo huo nchini licha ya kuwepo kwa virusi vya corona.

Kulingana na taarifa liliotuma kwa vyombo vya habari na shirikisho hilo limeanza kujiandaa kwa mwechi za ligi hiyo kufuatia hatua ya rais wa taifa hilo John Pombe Magufuli kupendekeza kundelea kwa ligi hiyo.

Akizungumza katika hafla ya kumuapisha waziri mpya wa maswala ya katiba siku ya Jumapili Mwigulu Nchemba nyumbani kwake huko Chato, Magufuli alisema kwamba amewasilisha pendekezo hilo kwa washauri wake ambao wanakutana kujadiliana jinsi mashindano hayo yatakavyoanza.

Hatahivyo aliongezea kwamba mashabiki watalazimika kutazama mechi hizo katika runinga ili kuzuia uwezekano wa maambukizi ya virusi vya corona.

Chanzo cha picha, IKULU

Katika taarifa yao TFF na TPLB wamesema kwamba wanaendelea na mchakato wa ndani kuelekea kurejea kwa ligi.

Hatahivyo taarifa hiyo imeongezea kwamba kurejea kwa ligi hiyo hatahivyo kutetegemea uamuzi wa serikali ambayo itatangaza muda mwafaka wa kurudi kwa ligi hiyo.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kwamba kwa sasa mchakato huo ni wa ndani na kwamba wanachama wa shirikisho hilo wanapaswa kutekeleza agizo la awali la kuepuka mikusanyiko.

Wamesema kwamba watatoa muongozo mwengine baada ya kupata muongozo wa serikali.

Akizungumzia kuhusu kurejea kwa ligi hiyo rais Magufuli alisema: Napendekeza kwamba tuanzishe mechi za ligi yetu ya soka , lakini watu wataruhusiwa kutazama katika runinga. Nasubiri ushauri wa wataalam ili ligi iendelee'', alisema katika hotuba ilipeperushwa moja kwa moja kutoka nyumbani kwake Chato Geita.

Tanzania iliripoti kisa chake cha kwanza cha Covid-19 tarehe 16 mwezi Machi. Tangu wakati huo, idadi hiyo imeongezeka maradufu hadi 480.

Kati ya visa hivyo wagonjwa 167 wamepona na wameruhusiwa kujiunga na familia zao nyumbani huku watu 16 wakiripotiwa kufariki.

Tarehe 16 mwezi Machi, taifa hilo lilitangaza kufungwa kwa shule kuanzia zile za chekechea hadi fomu 6 kwa siku 30.

Akizungumzia kuhusu soka, rais Magufuli amesema kwamba hakuna ushahidi kwamba wale wanaofanya mazoezi wanaweza kuathiriwa na mlipuko wa Covid-19.

'Inawezekana kwamba tutaishi na Covid-19 kama vile ambavyo tumekuwa tukiishi na virusi vya ukimwi na magonjwa mengine'', alisema.