Virusi vya corona: Vipimo vinavyotumika kupima corona Tanzania havina hitilafu

Institut Pasteur laboratory workers perform PCR (Polymerase Chain Reaction) tests to determine whether patients are positive for the new COVID-19 coronavirus, in Antananarivo, April 23, 2020

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Hadi chanjo itakapopatikana, WHOinasema kupima na kutafuta walioambukizwa ndio njia salma ya kudhibiti virusi

Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (CDC) kimesema kwamba vifaa vya kupimia virusi vya corona nchini Tanzania havina shida yeyote. Leo Alhamisi, Mkuu wa Afrika CDC amewaambia waandishi wa habari kuwa ofisi yake inavijua vilivyo vipimo hivyo.

"Vipimo ambavyo Tanzania inatumia tunajua kwamba vinafanyakazi vizuri," Dkt. John Nkengasong amesema hivyo katika mkutano na wanahabari wa njia ya mtandao.

Kauli hiyo ya Mkuu wa Africa CDC, inapingana na kauli ya rais wa Tanzania ambaye alisema huenda vipimo hivyo vikawa na matatizo.

Kituo hicho cha Africa CDC pamoja na wakfu wa Jack Ma, Shirika la msaada la bilionea wa China, lilisambaza vifaa hivyo, Nkengasong amesema na kuongeza kwamba vilidhinishwa na wanachojua ni kwamba vinafanya vizuri.

Kituo hicho kiko chini ya Umoja wa Afrika kina majukumu ya kuratibu mapambano dhidi ya mlipuko wa mangonjwa barani Afrika.

WHO inasema nini?

Kwa upande wake Shirika la Afya Duniani kupitia Mkuu wake wa bara la Afrika Dkt Matshidiso Moeti limesema halikubaliani na kauli ya Rais Magufuli kuwa vifaa vya kufanyia vipimo vya corona vina maambukizi ya virusi.

''Tunaamini kwamba vifaa vya kufanyia vipimo vilivyotolewa vinazingatia ubora wa kimataifa na zimenunuliwa kupitia WHO na zile zilizotolewa kama msaada na WHO Jack Ma hazijaingiwa na virusi'' alisema Dkt. Moeti

Aliongeza kusema, '' Samahani sikubaliani na kauli ya [Rais wa Tanzania] kwamba vifaa vya kufanyia vipimo vilivyopo vina maambukizi ya virusi. Kwa kweli hatukubaliani na kauli hiyo.Rais Magufuli atilia mashaka ufanisi wa maabara, uchunguzi kufanyika.

Siku ya Jumapili, rais Magufuli alikihutubia taifa alitilia mashaka ufanisi wa vifaa vya kupima corona katika maabara kuu ya nchi hiyo.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Rais Magufuli amekemea tabia ya watu kufanya mzaha na kutisha wengine kupitia mitandao ya kijamii

Magufuli alieleza kuwa aliagiza sampuli za Wanyama na matunda kupewa majina ya binadamu na umri kisha kupelekwa ili zipimwe bila wataalamu wa maabara hiyo kujua na matokeo yakarudi kuwa baadhi ya sampuli hizo zimekutwa na maambukizi ya corona.

"…Lazima ugundue kuna mambo ya ajabu yanafanyika nchi hii. Ama wahusika wa maabara wamenunuliwa na mabeberu, ama hawana utaalamu jambo ambalo si kweli kwa kuwa maabara hii imetumika sana katika magonjwa mengine. Ama zile sampuli zinazoletwa maana vifaa vyote vinatoka nje, hivyo lazima kuna kitu fulani kinafanywa," alisema Magufuli.

Magufuli amesema kutokana na taarifa hizo anaamini kuna watu ambao walipewa majibu yasiyo sahihi.

"Lazima kuna watu wameambiwa positive lakini si wagonjwa wa corona, na inawezekana wengine wakafa kwa hofu."

Jambo hili linaweza kuwa ni moja ya sababu kuu ya kutotolewa kwa takwimu mpya kufikia sasa.