Virusi vya corona: Kenya yathibitisha wagonjwa 23 wapya

Maeneo ya umma yanyunyiziwa dawa Kenya

Chanzo cha picha, AFP

Idadi ya wagonjwa wa virusi vya corona nchini Kenya imeongezeka hadi 672 baada ya wagonjwa wapya 23 kukutwa na virusi hivyo katika kipindi cha saa 24.

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumapili katibu msimamizi wa maswala ya Afya nchini Kenya Rashid Aman amesema kuwa idadi ya waliopona virusi yafika 239 baada ya wagonjwa wengine 32 kupona virusi hivyo.

Kati ya idadi hiyo wagonjwa 12 wameripotiwa kutoka Mombasa , sita kutoka Mandera wanne kutoka Nairobi na mmoja kutoka Kajiado.

Dkt Aman amesema kwamba wagonjwa watatu wa;likuwa wakitoka katika vifaa vya karantini.

Amsema kwamba sampuli 32,097 zilifanyiwa vipimo nchini kufikia sasa.

Ili kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo , serikali imewaagiza madereva wote wa malori ya masafa marefu kufanyiwa vipimo vya lazima saa 48 kabla ya kuanza safari zao.

Waziri Utalii Najib Balala amewashukuru wafanyakazi wote wa Afya kwa kuwa mstari mbele katika vita dhidi ya ugonjwa wa corona.

Amesema kwamba sekta ya ulatii imeathiriwa sana na virusi vya corona.

''Tunataka kuifungua sekta ya Utalii polepole kwasababu ndio ilioathirika vibaya na corona'', alisema bwana Balala.

Amewaomba Waislamu kuheshimu mikakati ya kukabiliana na corona ili kuzuia maambukizi.

''Wakati unapofungua baada ya kufunga mchana kutwa , usikaribiane na watu , kula pamoja kwa makundi ni sharti kusitishwe'', alisema.

Hatua zilizochukuliwa na Kenya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona:

1.Wizara ya Afya na huduma za umma imeanzisha hazina ya kuwasaidia wafanyakazi wa Afya wanaokabiliana na mlipuko wa virusi vya corona

2. Wizara ya elimu itachukua hatua kuwalinda wanafunzi kutokana na athari mbaya za hatua zilizochukuliwa kukabiliana na Covid-19

3. Mamlaka ya usambazaji wa tiba nchini Kenya imeondoa masharti ya ununuzi wa vifaa vya kujilinda dhidi ya Covid-19 kwa takriban miezi mitatu ili kurahisishia kaunti kununua vifaa hivyo.

4. Nyumba za watu wasiojiweza jijini Nairobi zitafaidi kutokana na fedha zilizotengwa na serikali kusaidia familia zisizojiweza

5.Bunge litapitisha tena mapendekezo na miswada kuhusu vichocheo vya uchumi.

6. Ili kuhakikisha msaada unagawanywa kwa njia salama, mfuko wa hali ya dharura wa kukabiliana na Covid-19, Kenya na mashirika mengine ya usalama yatashirikiana kuratibu miradi kama ule wa Adopt a Needy Family, ambapo raia wa Kenya wanasaidiana kipindi hiki cha janga kuhakikisha hatua zinachukuliwa bila kufuata urasimu

Maelezo ya picha,

Jinsi chanjo ya corona itakavyofanya kazi