Waridi wa BBC: Nilibakwa na wanaume watatu siku ya harusi yangu

  • Anne Ngugi
  • BBC News Swahili
Watu walikuwa wameanza kuzungumza vibaya kuhusu Terry kuwa amerogwa

Chanzo cha picha, Terry Gobanga

Maelezo ya picha,

Watu walikuwa wameanza kuzungumza vibaya kuhusu Terry kuwa amerogwa

Terry Gobanga ni Kasisi, Mke na mama wa watoto wawili aliyezaliwa mjini Nairobi nchini Kenya japo makao yake kwa sasa ni nchini Marekani katika jimbo la Texas.

Terry Gobanga - wakati huo akijulikana kama Terry Apudo - siku iliyoandaliwa kama ya harusi yake jamaa na marafiki walifika wakimsubiri bibi harusi ambaye ni Terry lakini hakuonekana wala hakuna aliyejua aliko.

Hakuna aliyedhani kuwa alikuwa ametekwa nyara, akabakwa na kisha kuachwa kama mzoga barabarani kilomita kadhaa kutoka nyumbani kwao.

Ni matukio ambayo yalibadilisha kabisa maisha ya Terry. Hivi leo anaishi na makovu yaliyopita ila yeye ni mshindi.

Chanzo cha picha, Terry Gobanga

Maelezo ya picha,

Terry na mumewe wa kwanza aliyefariki baada ya kufunga ndoa naye kwa siku 29 pekee

Tukio hili lilianzaje?

Terry anaelezea kuwa mpango wenyewe wa sherehe ya harusi yake ulikuwa makhsusi na ilikuwa iwe kubwa mno kama anavyokumbuka.

"Mimi kama Kasisi , nina wafuasi wa kanisa langu na hawakuwa wachache pia kulikuwa na marafiki, pamoja na watu wa jamii yangu na pia wa kutoka upande wa mume wangu, tulikuwa tufunge harusi katika kanisa kubwa la All Saints cathedral jijini Nairobi, Kenya, nilikuwa nimekodi nguo ya harusi iliyokuwa inapendeza ".

Kwa bahati mbaya usiku huo wa kabla ya harusi , Terry aligundua kuwa alikuwa na baadhi ya mavazi ya mchumba wake, kama tai na kadhalika na ilikuwa ni muhimu mavazi ya bwana harusi yaandamane , kwa hiyo rafiki aliyekuwa naye usiku huo alijitolea kuwasilisha mavazi hayo mapema asubuhi kabla ya sherehe ya harusi kuanza, kwa hiyo Terry na rafiki wake waliamka mapema, na ikawa kuwa Terry alikuwa anamsindikisha yule rafiki hadi kituo cha basi .

Chanzo cha picha, Terry Gobanga

Maelezo ya picha,

Ndoto ya harusi ya Terry ilizima kama mshumaa

Lakini alipokuwa njiani anarejea nyumbani ,alimpita mwanaume mmoja aliyekuwa ameketi katika sehemu ya mbele ya gari , mara ghafla akamnyanyua kwa nguvu kutoka upande wa nyuma na kumpachika katika sehemu ya nyuma ya gari hilo , tukio ambalo anasema lilifanyika kwa sekunde hivi.

Ndani ya gari hilo mlikuweko wanaume wengine wawili na ghafla gari likashika kasi.

Terry anakumbuka " Kipande cha nguo kilishindiliwa kwa nguvu ndani ya kinywa changu , huku nikipiga mayowe nikirusha miguu na mikono juu nikilia waniache huru ni siku ya harusi yangu , hapo ndipo nilipata ngumi ya kwanza , huku mmoja wa wananume hao akiniamrisha nishirikiane nao au nife."

Terry anakumbuka kuwa wanaume hao walikuwa wanambaka mmoja baada ya mwingine . Anasema alihisi kuwa angekufa , lakini alizidi kupambania maisha yake , anakumbuka kuwa mmoja wa wanaume hao ambaye alikuwa analiendesha gari hilo, alisimamisha kando, na ikawa ni nafasi yake kumbaka , alimtoa mdomoni kipande cha nguo kilichotumiwa kubana sauti yake, Terry alisema

"Nilijua kuwa maisha yangu yalikuwa yamekwisha niliamua kumwachia huyo mwanamume alama ya milele, hapo ndipo niliuuma uume wake kwa nguvu, huku alipiga kelele za ajabu "

Kilichofuatia ni Terry kudungwa kisu tumboni mwake na ghafla bin vuu akasukumwa nje ya gari ambalo lilikuwa linaendeshwa kwa kasi mno , hapo hapo alizimia, Terry anasema kuwa alielezwa kuwa damu zilikuwa zinamdondoka huku akiwa mtupu sehemu za chini za mwili wake .

Chanzo cha picha, Terry Gobanga

Maelezo ya picha,

Terry Gobanga

Aliepuka kifo kwa namna gani?

Saa sita zilipita tangu alipotekwa nyara , ni mtoto mmoja aliyeshuhudia akitupwa nje ya gari hilo, aliyepiga kelele na watu wakaja kumuokoa , yeye anasema kuwa alikuwa amezimia kama aliyefariki .Kwa hiyo afisa wa polisi walipowasili walijua kuwa amefariki na walimfunika kwa blanketi kama aliyefariki na safari ya kumpeleka chumba cha kuhifadhia maiti Ilianza .

" sikuwa nikipata hewa vizuri kwani nilifunikwa blanketi , nilikuwa hoi na hapo ndipo afisa wa polisi alisema kuwa yuko hai , na wakageuza gari hadi hospitalini nilipoanza kupata matibabu "Terry alisema.

Terry alifika hospitalini akiwa hajitambui, kwa hiyo alipoanza kupata ufahamu alikuwa tu analia na kutoa matamshi ya harusi na ndoa tu, anasema kuwa alikuwa amevimba mwili mzima , isitoshe alikuwa na kidonda kikubwa tumboni mwake kutokana na jeraha la kisu .

Juhudi za kutafuta jamaa wake zilianza , kanisani nako wasiwasi ulikuwa umeanza kwa kuwa bibi harusi alikuwa haonekani , na kwa hiyo watu walikuwa wameanza kumtafuta wasijue la kufanya .

Baadaye mchumba wake , jamaa wake walifahamishwa kilichomkuta Terry,na ilikuwa ni kwa mshtuko kwa wao wote.

" Nakumbuka aliponiona mchumba wangu alikuwa radhi kunihudumia ,hadi nipone ili tufunge harusi ,Mchumba wangu alikuwa ameibeba nguo yangu ya harusi ,na alikuwa anasema kuwa bado alikuwa anatamani kunioa licha ya yote yaliyonitokea "Terry alisema

Terry anasema kuwa akiwa hospitalini alipokea habari kuwa hataweza kushika mimba kutokana na majeraha ya kisu ambacho kilipasua hadi tumbo la uzazi , kando na hayo alipewa matibabu na dawa ya kuzuia kushika mimba na hata kuzuia kuambukizwa virusi vya HIV .

Chanzo cha picha, Terry Gobanga

Maelezo ya picha,

Huyu ni Kasisi Terry Gobanga

Je Terry alikuwa anaandamwa na bahati mbaya?

Terry anakumbuka kuwa alihisi kana kwamba ilikuwa ni makosa yake , na akiwa hospitalini alikuwa anamuomba msamaha mchumba wake ila mchumba wake alikuwa anampa moyo pamoja na watu wa jamii yake.

Mnamo Julai mwaka 2005, miezi saba baada ya kubakwa Terry alifunga ndoa , na kisha baadaye wakaenda fungate na mchumba wake .

Siku 29 baada ya ndoa yao , anakumbuka kuwa nyumba walioamua kuishi maisha kama Mume na mke ilikuwa na baridi mno ,na kwa hiyo mume wake aliwasha jiko la mkaa ili kujilinda dhidi ya baridi , Terry anasema mumewe wake aliliweka lile jiko kwenye chumba chao cha kulala , baada ya kula chakula cha usiku , Mume aliondoa lile jiko na kuliweka nje , wakati huo chumba chao kilikuwa na joto la kutosha .

Ila walipolala mumewe alianza kuwa na shida ya kupumua,vile vile Terry alianza kuwa na shida ya kupumua pia.

Na baada ya muda kidogo mume wake alishindwa kupumua kabisa , huku Terry akijikaza kuwaita majirani ili wawasaidie .

Majirani waliwasaidia kuwafikisha hospitalini, wote wakiwa katika hali mahututi.

"Mume wangu alifariki usiku huo sababu za kifo chake ni kuwa alikuwa amevuta hewa ya Carbon monoxide ambayo ni sumu , hii hewa ilitokana na jiko la mkaa lililokuwa chumbani mwetu , Daktari alisema kuwa nilikuwa na bahati sana kuishi kwa kuwa pia mimi nilikua nimevuta hewa hiyo yenye sumu " anakumbuka Terry

Kurudi tena kanisani kwa mazishi ya mumewe watu walikuwa walianza kuzungumza vibaya kuhusu Terry , wengine wakisema kuwa amerogwa , au yeye ndiye alikuwa na bahati mbaya katika maisha yake , wengine pia walikuwa na maoni kuwa kule kubakwa kwake kulikuwa chanzo cha matukio mabaya katika maisha yake.

Terry alianza kuamini mengi yaliyosemwa kwa kuwa hata yeye alikuwa anajiuliza maswali mengi sana , hususani kama Kasisi alishindwa kuelewa ni kwanini Mwenyezi Mungu alikuwa anakubali mateso na mahangaiko ya aina hiyo kumkuta?

Chanzo cha picha, Terry Gobanga

Maelezo ya picha,

Watu walikuwa wameanza kuzungumza vibaya kuhusu Terry kuwa amerogwa

Ndoa ya pili ya Terry

Terry alijiapiza hatoolewa tena maishani mwake , kwani kuhimili matukio kama hayo aliona kama mzigo na mlima mkubwa kuukwea , anasema kuwa matukio katika maisha yake hawezi kutamani yampate mtu yeyote kwani yana uchungu mwingi mno

"Uchungu wa matukio haya ulikuwa ni mwingi mno hadi kwenye kucha zangu" Terry Anasimulia alichokuwa anahisi wakati huo.

Wakati huo kuna mwanaume mmoja ambaye alikuwa anafuatilia mno kupona kwa hisia na pia maisha yake Terry, Huyu ni mwanaume kwa jina Tonny Gobanga , ambaye alikuwa anamhimiza katika maisha na mara kwa mara kumtembelea .

Muda sio muda Bwana Tonny alimweleza Terry kuwa alitamani kumuoa , Ila Terry hakuwa na jibu kwake alianza kwa kumweleza anunue jarida moja ambalo lilikuwa limeandikwa kuhusu maisha ya kubakwa kwake ,alisome kwanza kabla ya kutamani kumuoa .

Chanzo cha picha, Terry Gobanga

Maelezo ya picha,

Terry Gobanga na mumewe wa sasa Tonny Gobanga

Na kwa kweli Terry anasema kuwa Tonny alisoma kuhusu maisha yake na bado akamweleza kuwa alitamani amuoe , na je alipomweleza kuwa hana uwezo wa kujifungua mtoto , Tonny alimwambia kuwa watoto ni zawadi kutoka mbinguni , wajaaliwe watoto wasijaaliwe yeye anatamani tu Terry awe mke wake wa ndoa .

" Kwa hiyo nilisema ndio na kukubali Tonny anioe , ila Tonny alipowaeleza wazazi wake kuhusu azma hio , kwa kujua kilichonikuta walimkataza kunioa , licha ya hayo harusi ilifanywa japo baba mkwe hakufika katika harusi yetu , watu 800 walifika lakini naamini wengi walifika kushuhudia harusi yangu kutokana na matukio ya maisha yangu ya hapo nyuma "Terry anakumbuka

Ilikuwa miaka mitatu tangu harusi yake ya kwanza , na kwa hiyo Terry alikuwa na uoga pamoja na hofu kuu kuhusu ndoa nyingine , hususan kwa mume mwingine.

''Mwaka mmoja tangu ndoa , nlianza kuhisi vibaya , lakini nilipokwenda hospitalini Dakitari aliniambia kuwa nilikuwa na ujauzito , kwa kweli nilishtuka nisijue cha kufanya'' . Terry alisema

Na kwa kweli baada ya muda alijifungua mtoto wa kike na baada ya miaka mengine minne nilibarikiwa na mtoto wa pili .

Terry ameandika kitabu kuhusu maisha yake kwa jina Crawling out of the Dark kingine ni kuwa yeye na shemeji zake wote akiwemo Baba Mkwe ni marafiki mno. Uhusiano wao uko shwari na amekubalika katika jamii ya mume wake , ni miaka 12 tangu ndoa yake ya pili na anasema ana kila sahabu ya kutabasamu na kutoa shukrani kwake mwenyezi Mungu kwa umbali amemleta .

Terry anasema kuwa aliwasamehe waliombaka , japo hawakuwahi kamatwa na polisi anasema kuwa amepona kutokana na yaliyomkuta na ndiposa alifungua shirika lisilo la kiserikali kwa jina Kara Olmurani, kituo kinachofanya kazi sana na waathirika wa ubakaji .