Virusi vya corona: Serikali, sayansi na sintofahamu ya mapambano dhidi ya corona Tanzania

Maabara

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Hadi chanjo itakapopatikana, WHO inasema kupima na kutafuta walioambukizwa ndio njia salama ya kudhibiti virusi

Wakati serikali zote duniani zimeendelea kujifunza namna sahihi ya kupambana na ugonjwa huu, zipo zinazosifika na zile zinazokosolewa kwa namna zinavyopambana na Corona.

Afrika Mashariki, serikali kama zile za Rwanda na Uganda zimesifiwa juu ya sehemu ya mapambano yake; Rwanda, kwa mfano, namna inavyowasaidia wananchi wasiojiweza na Uganda kwa kuweka hatua kali za mapambano tangu mwanzo kabisa wa ugonjwa huo na kuendelea kutoa taarifa za kina juu ya mwenendo wa maambukizi, na kuzitoa mara kwa mara.

Tanzania kwa upande mwingine inakosolewa vikali kwa ujumla wa namna inavyopambana na gonjwa hili. Kuanzia hatua ilizozichukua hadi usiri uliogubika katika utoaji wa takwimu zinazohusu COVID-19

Ukosoaji kutoka ndani na nje

Mwanzoni mwa janga la corona, ukosoaji ulianza kuongozwa na viongozi wa siasa wa upinzani nchini pamoja na wafuasi wao. Lakini hivi sasa ukosoaji umevuka mipaka na kujumuisha mashirika makubwa ya kisayansi na ya kimataifa ya Africa Africa Centres for Disease Control and Prevention (CDC) na Shirika la Afya Duniani tawi la Afrika (WHO Afrika).

Ukosoaji kutoka kwa mashirika haya unatia uzito si tu kwasababu ni ya kitaalamu lakini pia ndio mashirika yaliyo mstari wa mbele katika kuongoza sera na mbinu za upambanaji dhidi ya ugonjwa wa corona ulimwenguni kote.

Tarehe 23 Aprili, kiongozi wa WHO Afrika aliikosoa serikali ya Tanzania kwa kusema kuchelewa kwa kuweka masharti makali ya kupunguza misongamano kulichangia ongezeko kubwa na la ghafla la wagonjwa wa corona nchini.

Tarehe 6 May, aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya na rafiki wa karibu wa Rais John Magufuli, Raila Odinga alikiambia kituo cha habari cha Afrika Kusini SABC News kwamba ana wasiwasi na namna serikali ya Tanzania inavyokabiliana na maambukizi nchini humo na kwamba anaamini Magufuli anashauriwa vibaya.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni aliifananisha jumuiya ya Afrika Mashariki kama nyumba kubwa yenye vyumba vingi na kusema nyakati zingine inawezekana ikawa kazi kuiweka nyumba hii katika hali nzuri kwasababu wakati 'vyumba' vingine vinaweza kuwa vimedhibitiwa vizuri, vingine vinakuwa havijadhibitiwa vizuri.

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA

Maelezo ya picha,

Rais wa Tanzania, Dokta John Magufuli

"Mungu ndiye aliyesema kwamba Afrika Mashariki ni moja. Chumbani ni Uganda, sebuleni ni Kenya, na sebule nyingine ni Tanzania….kwamfano sasa tumeiondoa corona kutoka hapa, kutoka chumbani (Uganda), lakini sebuleni huko….."alisema Museveni akimalizia kwa kikecho.

Kukosolewa huku kunakovuka mipaka kujumuisha mashirika ya kimataifa yenye wataalamu na uzoefu wa kupambana na majanga kama haya, ukosoaji kutoka kwa viongozi wa nchi na wengine hata marafiki wa karibu wa Tanzania na Magufuli mwenyewe kunatoa picha ya kutokuridhishwa kwa namna serikali inavyopambana na janga hili kunakotokea nchini kunavuka misingi ya chama au chuki binafsi dhidi ya serikali.

Nani hasa anayeongoza mapambano?

Mwanzoni kabisa mara tu baada ya kuthibitishwa kwa mgonjwa wa kwanza wa corona nchini, serikali iliunda kamati iliyojumuisha wizara na sekta mbali mbali kutoka serikalini.

Ikiongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, serikali ilisema kamati hii si tu ndio itaongoza uratibu wa mapambano dhidi ya corona nchini, lakini Waziri wa Afya, Waziri Mkuu na Rais mwenyewe, ilitangazwa, ndio watakuwa wasemaji wakuu wa mwenendo mzima wa mapambano nchini ikiwa ni kuanzia kutangazwa kwa idadi mpya ya wagonjwa nchini hadi usimamizi wa utoaji huduma kwa waliambukizwa na kufariki kutokana na corona.

Hata hivyo, ni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ambaye amekuwa akisifiwa na wengi na kuitwa 'shujaa' wa mapambano haya - mbali na wahudumu wa afya waliopo mstari wa mbele katika kutibu wagonjwa wa corona.

Kwa sehemu, sifa hizi anazomwagiwa Mwalimu hazitokani tu na wakati wa nyuma alipokuwa akionekana mara kwa mara akitoa taarifa za mwenendo wa maambukizi, lakini pia ni kutoka na taarifa na maelekezo kutoka wizara ya afya ambayo yamekuwa yakizingatia miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Marais wa Afrika mashariki Uhuru Kenyatta, paul kagame, Yoweri Museveni na John Pombe Magufuli

Baadhi ya taarifa hizi zimekuwa hata zikikinzana na ushauri ambao amekuwa akiutoa Magufuli. Kwa mfano, wakati Magufuli akihimiza watu kutumia njia za kujifukiza kama sehemu ya kinga na tiba dhidi ya corona, taarifa kutoka Wizara ya Afya zimekuwa zikisisitiza msimamo wa WHO kuwa corona haina dawa na kuwatahadharisha watu dhidi ya mbinu hiyo huku zikiwataka wataalamu kujitokeza na kutoa mwongozo kuhusu kujifukiza.

Mwanzoni kabisa Magufuli alimwagiwa sifa kwa kuongoza kwa mfano. Picha zake alizokuwa akisalimiana na kuagana na kugusana miguu pekee na viongozi mbali mbali wa upinzani waliomtembelea Ikulu ziligeuka gumzo duniani kote juu ya kiongozi wa nchi anayeongoza mapambano dhidi ya corona kwa mfano.

Rais kufanyia kazi Chato

Kadiri siku zilivyokwenda, Magufuli aliendelea kukosolewa kwa 'kukaa kiti cha nyuma' katika kuongoza mapambano haya. Wakosoaji wake kwa mfano wamemtaka arudi jijini Dar es Salaam au aende Dodoma na kutoka mjini kwao Chato ambapo amekuwepo kwa wiki kadhaa sasa.

Wengi wamekuwa wakitafsiri uwepo wake mjini Chato kama namna ya kujificha.

Hata hivyo, Magufuli mwenyewe ametetea uwepo wake huko Chato kwa kusema anaweza pia kuongoza mapambano dhidi ya corona hata kutokea huko alipo.

"Wengine wanasema nipo Chato. Kwani waliambiwa Chato huku sitakiwi kuwepo huku? Huku si ndiko nitazikwa? Nikienda Moshi kesho, nako watasema niko Moshi nimekimbia wapi? Makao makuu yapo Dodoma. Lakini hizi ni siasa, za kutumia kila kitu ni siasa. Hapa ndipo wakati watu tunatakiwa kusimama pamoja katika kupambana na hili," alisema Magufuli katika hafla ya kumuapisha waziri mpya wa Sheria na Katiba.

Lakini kama kiongozi mkuu wa nchi, ambaye kauli yake ni rahisi kugeuzwa kuwa sera na watendaji wake wa chini, Magufuli amekuwa akikosolewa kwa kutoa kauli zinazopingana na ushauri wa kitaalamu wa wataalamu wa magonjwa ya maambukizi kama corona lakini hata ushauri kutoka mashirika ya kimataifa ya kisayansi yanayoongoza mapambano haya kama WHO na CDC.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Nchi za kiafrika zinafanya jitihada mbalimbali kudhiti maambukizi ya Covid-19

Magufuli kwamfano amevitilia shaka vifaa vya kupimia corona nchini na wataalamu wanaofanya kazi katika maabara hiyo. Ameenda mbali zaidi na kudai kwamba inawezekana vifaa hivyo vimepandikizwa na 'mabeberu' na watumishi wa maabara wanatumiwa na 'mabeberu'

Shutuma hizi zimetupiliwa mbali na Africa CDC ambapo imesema vifaa vinavyotumika Tanzania vinafanana na vile vinavyotumika barani kote Afrika. Wameongeza pia kwamba wamekuwa wakishirikiana na nchi zote barani Afrika katika kuwafundisha watumishi wa maabara na kutatua changamoto zinazotokana na utumiaji wa vifaa hivyo na utaratibu wa upimaji wenyewe

Sera ya mapambano

Hadi hivi sasa, sera ya Tanzania katika kupambana dhidi ya corona haiko wazi. Inawezekana serikali ina mwongozo inaoutumia katika mapambano haya, lakini tofauti na nchi zingine barani Afrika na kwingineko, sera kamili inayoongoza serikali ya Tanzania katika mapambano haya haiko hadharani.

Nchi kama Sweden kwamfano, sera yao ni kuwalinda wazee na waliowadhaifu kiafya. Afrika ya Kusini kwa upande mwingine inafata sera ya kulinda jamii nzima, ikidhihirika katika nguvu kubwa iliyowekwa katika kupima Umma kwa maelfu, kuwatambua walioathirika na wale waliokutana nao na kuwatenga wasiambukize wengine walio salama.

Kwa Tanzania, wakati shule, vyuo na michezo vimezuiliwa kwa muda, makanisa, misikiti, masoko na vilabu vya pombe - ambavyo vyote vinakusanya watu wengi kwa wakati mmoja mahali pamoja - vyote vimeachwa viendelee.

Zoezi la upimaji pia limegubikwa na mkanganyiko. Vifaa na wataalamu wa upimaji wanatiliwa shaka, idadi ya waliopimwa haitolewi hadharani na utoaji wa taarifa za mwenendo wa maambukizi si wa mara kwa mara na hivyo kuuacha Umma gizani kuhusu picha kamili ya ukubwa wa janga la corona nchini.

Magufuli amekataa wazi hoja ya kutumia mbinu ya kuwakataza watu kutoka majumbani kwao ifahamikayo kwa lugha la kiingereza kama 'lockdown.'

"Hili tatizo litaondoka, na tuendelee kuchukua precautions (tahadhari) hizo hizo ambazo zinatakiwa kuchukuliwa. Tusilihusishe hili na uchumi wa nchi yetu. Bado tupo kwenye elementary stage (hatua za awali), tusipanic (tusitaharuki). Tuendelee kuchapa kazi, uzalishaji uendelee maradufu zaidi. Tusitishane. Na wanasiasa waache kutumia hili kama agenda, halitawasaidia. Mtu anazungumza kufunga Dar es Salaam, kufunga Tanga, sifungi, nilishasema. Lazima Watanzania tuendelee kuishi, tuchape kazi na kuchukua precaution," alisema Magufuli katika hafla ya kumuapisha waziri mpya wa sheria na katiba.

Kwa kauli kama hii, wachambuzi wanasema inawezekana sera ya Tanzania ikawa ni kulinda uchumi wa nchi na kipato cha Mtanzania mmoja mmoja huku nguvu zaidi ikielekezwa kwa wagonjwa wa Corona walio na dalili kubwa na wale ambao hali zao zimefikia mahututi

Wapo wanasayansi na wachumi wanaokubaliana na mtazamo wa Magufuli. Lakini wanaoukosoa wanauona ni kama kuutanguliza mbele uchumi badala ya watu, wananchi.

Ukandamizwaji wa Sauti Tofauti

Kama ambavyo serikali imekuwa hodari katika kuwaadhibu wakosoaji katika masuala ya kisiasa, katika janga hili la Corona pia hali imekuwa vivyo hivyo.

Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii Dkt Nyambura Moremi na Meneja wa Udhibiti wa Ubora wa maabara hiyo Jacob Lusekelo wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi baada ya shutuma kwamba inawezekana watumishi wa maabara hiyo wanatumiwa na 'mabeberu'.

Polisi jijini Arusha ilimkamata wakili maarufu Alberto Msando kwa madai ya kutoa kauli ya uchochezi. Msando alikamatwa baada ya kusambaa kwa video iliyomwonyesha akiwaambia waandishi wa habari kuwa hali ya Corona ni mbaya sana.

Mwanzoni mwa Aprili, makampuni ya runinga matatu ya Star Media Tanzania Limited, Multichoice Tanzania Limited and Azam yalipigwa faini ya Sh 5 milioni, takribani dola $2160 kwa kile mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) ilidai kuwa ni kurusha taarifa ya uongo na kupotosha.

Duniani kote, mamlaka zinaadhibu wasambaza taarifa za kupotosha kuhusu Corona. Lakini kinachokosolewa ni pale serikali inapoamua kuadhibu taarifa inayoonekana kuikosoa serikali na namna inavyopambana na Corona.

Hatua kama hii inawafanya wengi wahisi kwamba kuna kitu kisicho kizuri serikali inakificha na hivyo kuongeza wasiwasi kwamba inawezekana tatizo la maambukizi na idadi ya vifo nchini ni kubwa kupindukia.

Mtindo wa Uongozi wa Magufuli haujabadilika

Hata kwa serikali zinazosifika kuwa na uongozi mahiri na mfumo thabiti wa huduma za afya, janga hili bado limeziyumbisha. Idadi ya maambukizi na vifo imeendelea kupanda na kulemea serikali zenye uchumi mkubwa na uwezo thabiti wa kupambana na Corona.

Lakini utofauti ni kwamba viongozi wa serikali zinazosifika kuwa mahiri na kuonyesha weledi katika kupambana na janga hili ni wale wasiotupia lawama nchi zingine au kundi Fulani la watu nchini - badala yake wanatoa muongozo wa kupambana na ugonjwa, namna serikali zao zinavyosaidia biashara na uchumi nchini, wanawatia moyo wananchi wao.

Magufuli kwa upande mwingine amekuwa akikosolewa kwa kuendelea kuelekeza lawama kwa 'mabeberu' na wapinzani wa kisiasa na wafuasi wao nchini.

Kama jinsi alivyowashutumu 'mabeberu' katika kile anachokiita vita ya uchumi alipoanzisha mageuzi katika sekta ya madini, vivyo hivyo Magufuli ameendelea kuelekeza lawama zake kwa 'mabeberu' hata katika swala la ugonjwa wa Corona.

Katika hotuba yake ya May 3, Magufuli alidokeza kwamba inawezekana 'mabeberu' wameipatia Tanzania vifaa vibovu na kuendelea kuwatumia wataalamu wa maabara inayopima maambukizi kutoa takwimu zisizo sahihi ili kukuza tatizo la corona nchini tofauti na hali halisi iliyopo.

"Kuna mambo ya ajabu yanayofanywa katika nchi hii. Aidha wahusika wa laboratory (maabara) ile wamenunuliwa na mabeberu, aidha hawana utaalamu, which is not true (kitu ambacho si kweli) kwasababu maabara hii imetumika sana katika magonjwa mengine, aidha zile sampuli zinazoletwa, kwasababu mpaka reagent zinatoka nje, mpaka zile swaps, vi pamba vile vya kuwekwa kwenye ile nanilii, vinatoka nje. Kwa hiyo, lazima kuna kitu Fulani kinafanywa," alisema Magufuli.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Rais Magufuli amekemea tabia ya watu kufanya mzaha na kutisha wengine kupitia mitandao ya kijamii

Siku chache baadae, viongozi wa kikanda wa mashirika ya kimataifa yanayoongoza mapambano dhidi ya ugonjwa huu Africa CDC na Shirika la Afrya Ulimwenguni tawi la Afrika (WHO Africa) walijitokeza na kupinga vikali shutuma kwamba vifaa vya upimaji vinavyotumika na maabara ya Tanzania ni vibovu na kwamba wataalamu wake wanatumika na 'mabeberu'.

Aina hii ya uongozi wa Magufuli ya kutumia nguvu na muda mwingi katika kuelekeza lawama kwa wengine inamfanya aonekane kukataa uhalisia na ukweli juu ya madhara halisi ya corona na hivyo kushindwa kupambana na ugonjwa wenyewe kiufanisi.

Hata hivyo serikali imekuwa ikikanusha madai kwamba inatetereka katika kupambana na corona na kwamba mbinu inazotumia si thabiti.

Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje imetoa mifano kwamba tangu mwanzo serikali imekuwa ikiongoza si tu nchini, lakini hata kikanda, ikitoa mifano ya mikutano ya Mawaziri ya jumuiya, ile ya kiuchumi ya nchi zilizopo Kusini mwa Afrika (SADC) na ile ya Afrika Mashariki.

"Madai yanayotolewa kuwa Tanzania imelegalega ama kujitenga katika kupambana na ugonjwa wa COVID 19 si ya kweli kwa kuwa Tanzania imetoa uongozi madhubuti katika eneo iliyopewa dhamana ya uongozi ya Uenyekiti wa nchi SADC na imeifanya na inaendelea kuifanya kwa heshima na bidii zote," alisema Profesa Palamagamba Kabudi alipokuwa nchini Madagascar ambapo alikwenda kuchukua dawa ya mitishamba inayopigiwa chapuo kukinga na kuponya virusi vya corona.