Virusi vya Corona: Zanzibar yapokea mashine yenye uwezo wa kupima watu 288 kwa siku

Kipimo cha corona

Chanzo cha picha, Getty Images

Zanzibar imepokea mashine ya kupimia ugonjwa wa homa kali ya mapafu, Corona, kufuatia agizo la Rais Dk Ali Mohamed Shein kwa Wizara ya Afya kufanikisha upatikanaji wa mashine za kupimia ndani ya miezi mitatu.

Mashine zingine mbili zinatarajiwa kupokelea wakati wowote, na zitafungwa visiwani Unguja na Pemba, imesema taarifa kutoka Idara ya Habari Maelezo Zanzibar.

Mashine hii iliyopokelewa leo, inauwezo wa kutoa majibu ndani ya saa nane kwa vipimo vya watu 96.

"…hivyo kwa saa 24, ina uwezo wa kutoa majibu ya vipimo 288," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kupokewa kwa mashine hii kunakuja wakati ambapo vipimo vya COVID-19 vimesimama kutolewa Tanzania bara kupisha uchunguzi katika maabara ya taifa.

Uchunguzi huu ulikuja baada ya Rais John Magufuli kutilia shaka utendaji kazi wa vifaa na wataalamu wa maabara hiyo ambapo alidai pamekuwa na utoaji wa majibu 'positive' mengi kuliko kawaida katika maabara hiyo.

Zanzibar pia wamekuwa wakitumia maabara hiyo.

Shirika la afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika na kituo cha kupambana na kuzuia maradhi kilicho chini ya Umoja wa Afrika (Africa CDC) hata hivyo walitupilia mbali madai haya ya Magufuli.

Walisema vifaa pamoja na wataalamu walioko katika maabara ya Tanzania wana ufanisi kama ule ule walionao wataalamu na vifaa vinavyotumika kote barani Afrika.

Jana Alhamisi, Africa CDC iliitaka Tanzania kutoa takwimu mpya za mwenendo wa ugonjwa wa corona nchini humo.

Mkurugenzi wa Africa CDC, Dkt John Nkengasong amesema kuwa kituo chake kwa kutumia takwimu hizo kipo tayari kushirikiana na Tanzania kwa kuipatia msaada wa kitaalamu na kiufundi unaohitajika.

Mkurugenzi Africa CDC

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mkurugenzi wa Africa CDC Dkt John Nkengasong amesema kituo chake kipo tayari kushirikiana na Tanzania.

"Hili ni janga kubwa kwa bara (Afrika) lote na dunia kwa ujumla… hivyo ni kwa faida ya Tanzania kutoa takwimu kwa wakati ili tufahamu mapungufu yapo wapi na tuwasiadie kadri itakavyohitajika," alisema Dkt Nkengasong katika mkutano na wanahabari kwa njia ya mtandao.

Mara ya mwisho kwa Zanzibar kutangaza takwimu mpya ilikuwa ni Jumatano ya wiki ilopita Mei 7. Huku Tanzania Bara ikitoa takwimu za mwisho Aprili 29.

Mpaka sasa taarifa rasmi zinaonesha kuwa kwa ujumla wake Tanzania kuna wagonjwa wa Corona 509, waliopona 183 na waliofariki kutokana na maradhi hayo ni 21.

Coronavirus
Banner