Virusi vya corona: Utafiti wa kubaini iwapo mbwa anaweza kugundua virusi hivyo umeanzishwa

Mbwa wa kunusa ugonjwa

Chanzo cha picha, DHSC

Utafiti wa iwapo mbwa walio na utaalamu wa kimatibabu wanaweza kugundua virusi vya corona katika wanadamu unatarajiwa kuanza.

Mbwa hao tayari wamefunzwa jinsi ya kubaini harufu za saratani, malaria na ugonjwa wa parkinson na Shirika la Medical Detection Dogs.

Awamu ya kwanza ya majaribio hayo itaongozwa na taasisi ya usafi ya London na tiba za kitropiki, pamoja na chuo kikuu cha Charity na Durham.

Utafiti huo umepata ufadhili wa takriban £500,000 kutoka kwa serikali ya Uingereza.

Waziri wa uvumbuzi Lord Bathel amesema kwamba anatumai kwamba mbwa hao watatoa matokeo ya haraka ikiwa ni mikakati ya serikali kuongeza vipimo vyake kwa umma.

Utafiti huo utaangazia iwapo mbwa hao kwa Jina Covid Dogs - wanaoshirikisha Labradors na Cocker spaniels - wanaweza kugundua virusi hivyo miongoni mwa wanadamu kupitia harufu kabla ya dalili kujitokeza.

Utafiti huo utabaini iwapo mbwa hao ambao wana uwezo wa kuwachunguza hadi watu 250 kwa saa wanaweza kutumika kama njia ya mapema ya kugundua virusi vya corona miongoni mwa wanadamu.

Awamu ya kwanza itahusisha wafanyakazi wa idara ya Afya katika hospitali za London ambao watakusanya sampuli kutoka kwa wale walioambukizwa na wale ambao hawajaambukizwa.

Sampuli za harufu ya mwili zinaweza kutoka katika vyanzo kadhaa ikiwemo barakoa zilizotumika.

Mbwa sita - Norman, Digby, Storm, Star, Jasper na Asher - watafanyiwa mafunzo kugundua virusi hivyo kutoka kwa sampuli zitakazotolewa.

Shirika hilo la hisani limesema kwamba mafunzo hayo yanaweza kuchukua kati ya wiki sita hadi nane.

Chanzo cha picha, Medical Detection Dogs

Chanzo cha picha, DHSC

Baada ya majaribio ya miezi mitatu , serikali itaamua maeneo ambayo inadhani mbwa hao watakuwa muhimu.

Uwezekano mkubwa ni kwamba wanaweza kutumiwa katika milango ya kuingia nchini kama vile viwanja vya ndege ili kuwafichua wanaobeba virusi hivyo .

Mbwa hao pia wanaweza kutumika katika vituo vya kupima virusi hivyo kama njia nyengine za kuwapima watu.

Zaidi ya miaka 10 ya utafiti uliokusanywa kutoka katika mbwa hao wa tiba, umeonesha kwamba wanaweza kufunzwa kunusa harufu ya ugonjwa.

Claire Guest mwanzilishi wa shirika hilo la hisani na afisa mtendaji alisema kwamba ana uhakika mbwa wao wataweza kubaini harufu ya virusi vya corona.

''Iwapo hilo litabainika rasmi , mbwa hao basi watapelekwa katika awamu ya pili ya kuwapima moja kwa moja walioambukizwa na ambao hawajaambukizwa , ambapo baadaye tutashirikiana na mashirika mingine kuwafunza mbwa zaidi'' , alisema.

Mbwa wamefunzwa kugundua malaria kutokana na harufu mbaya ya sampuli ya nyayo.

Profesa James Logan , kutoka shule ya usafi mjini London na dawa za kitropiki alisema kwamba: Kazi yetu ya awali imeonesha kwamba malaria ina harufu mbaya na kupitia mbwa hao wa tiba tulifanikiwa kuwafunza mbwa kugundua ugonjwa huo.

Hii pamoja na utambuzi kwamba magonjwa ya mapafu yanaweza kubadili harufu ya mwili, inatufanya tuwe na matumaini kwamba mbwa pia wanaweza kugundua Covid-19.

Watafiti hao pia wamefanikiwa kuwafunza mbwa kugundua saratani na ugonjwa wa parkinson katika wanadamu.