Wasichana Pakistan: Mwanaume akamatwa kwa kuua binamu zake juu ya video tatanishi'

Muhammad Aslam in police custody, 20 May, 2020

Chanzo cha picha, North Wazirastan police

Maelezo ya picha,

Polisi walikua wakimtafuta Muhammad Aslam kwa siku kadhaa

Polisi wamemkata mwanaume anayeshukiwa kutekeleza mauaji ya wanawake wawili vijana nchini Pakistan baada ya video kusambaa mitandaoni inayomuonesha mwanaume mmoja akiwabusu.

Muhammad Aslam anashukiwa kutekeleza mauaji ya binamu zake wenye umri wa miaka 18 na 16.

Mwanaume kwenye video hiyo, mmiliki wa simu iliyochukua video hiyo pamoja na jamaa wa wanawake hao wote wamekamatwa.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema ghasia dhidi ya wanawake bado ni tatizo kubwa nchini Pakistan.

Wasichana hao waliuawa wiki iliyopita katika Kijiji cha Shamplan, eneo la Garyom mpaka wa Kaskazini na Kusini mwa Waziristan jimbo la Khyber Pakhtunkhwa.

Eneo hilo ni la kijijini ambapo wenyeji wanaendeleza misimamo mikali na mara nyingi sheria za jamii hutekelezwa na kuzingatiwa zaidi kuliko zile za taifa.

Wanaharakati wanasema karibia wanawake 1,000 huuawa kila mwaka kote nchini humo katika kile kinachofahamika kama "mauaji ya heshima" - kwa kuvuka mipaka kulingana na matendo yao kwenye mitandao ya kijamii.

Safari ndefu ya kuhakikisha haki inapatikana

Sheria za eneo la Waziristan zina maanisha kwamba suala la mambo ya ngono au tabia za namna hiyo ni jambo lisilokubalika kabisa. Hivyo basi video hiyo iliyosambaa mitandaoni ilipokelewa kwa mshtuko mkubwa.

Maafisa wa polisi wapya waliletwa eneo hilo miaka miwili iliyopita kuhakikisha kwamba sheria ya serikali inafuatwa na wao ndio walioamua kuchukua hatua.

Kwasababu "mauaji ya heshima" yanachukuliwa kama suala la kifamilia na hakuna malalamiko yoyote yanayowasilishwa, maafisa wa kaskazini mwa Waziristan walichukua hatua wenyewe madai ya mauaji hayo yalipoibuka.

Awali, maafisa walikuwa wameandikisha shitaka linalomuhusisha mshukiwa na mauaji, lakini kwasasa wameongeza kipengele chenye kuhusisha nia ya kusababisha madhara, kuficha ushahidi na uhalifu wa njia ya kielektroniki.

Kifungu cha kusababisha madhara kinazuia wanafamilia wa aliyeuawa kumuondolea anayedaiwa kutekeleza mauaji mashitaka, hatua ambayo inaruhusiwa chini ya sheria za Kiislamu za Pakistan za miaka ya 1980.

Lakini bado kuna njia ya kufanya kesi hiyo kuwa thabiti kabisa dhidi ya mshukiwa. Changamoto iliyopo kwa sasa ni kupata miili ya waliouawa na kuifanyia uchunguzi.

Wachunguzi wanaamini kwamba miili hiyo ilichukuliwa na familia na kupelekwa eneo jirani la Kusini mwa Waziristan kuzikwa. Wanasema wanashirikiana na maafisa wa Kusini mwa Wazirstan kubaini makaburi ya waathiriwa.

Aidha maafisa wa polisi watahitaji kibali kutoka kwa hakimu wa mahakama kufukua miili ya wasichana hao.