Virusi vya corona: ''Nilimzika binamu yangu kupitia Facebook Live'

  • By Mercy Juma
  • BBC News, Nairobi
Mourners at Chris' funeral in western Kenya

Chanzo cha picha, Mercy Juma

Kila mtu anafahamu marufuku ambayo serikali ya Kenya iliweka dhidi ya shughuli za mazishi katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya corona.

Watu 15 peke yake ndio walioruhusiwa kujumuika katika shughuli za mazishi ya binamu yangu, Chris, na kila kitu kilipaswa kufanyika kufikia saa tatu asubuhi, saa za Afrika mashariki.

Majira ya saa moja asubuhi, wote tulikuwa tunasubiri kwenye simu zetu na komputa, kuangalia mazishi hayo ambayo yalikuwa yanaruka mubashara katika kurasa ya Facebook.

Mimi ni miongoni mwa mamia ya watu walitoa heshima ya mwisho kwa Chris kupitia mtandao. Alikuwa mtu wa watu - na ilikuwa majonzi makubwa kwa familia kumpoteza.

Alikuwa mcheshi, alikuwa anaweza kukuchekesha hata kabla hajafika ndani ya nyumba - kwanza ulikuwa unaanza kumsikia kuanzia akiwa umbali wa mita 200 akiwa getini.

Chanzo cha picha, Courtesy of Mercy Juma

Maelezo ya picha,

Jamaa na rafiki wanasema Chris alihitaji kuzikwa kwa heshima

Na Chris alikuwa amezoea kujitoa kwa watu, alikuwa hakosi kwenye shughuli za misiba na harusi.

Alikuwa muhamasishaji mkubwa, alikuwa anawahimiza watu kushiriki kila matukio.

Hivyo kwa siku hii, tumejitoa kwake pia ingawa ni tofauti na ilivyozoeleka.

'Hatukuweza kucheza muziki alioupenda'

Chris alikuwa ni binamu yangu wa karibu lakini tulikuwa katika nyumba moja na alikuwa zaidi ya kaka kwangu.

Alifariki huko magharibi ya Kenya, mjini Kisumu siku ya Jumapili ya Pasaka, baada ya kuugua kwa wiki kadhaa kwa matatizo ya ini.

Serikali ilitoa utaratibu wa mazishi yake. Alipaswa kuzikwa ndani ya siku tatu.

Lakini ndugu wengi na rafiki zake walikuwa Nairobi ambako kulikuwa na marufuku ya kutoka nje au kutoka na kuingia katika mji huo hivyo si kila mtu aliweza kuhudhuria mazishi yake.

Ibada ya mazishi yake ilikuwa fupi. Hotuba hazikuruhusiwa na waliimba nyimbo kidogo sana.

Chris alipenda muziki - alikuwa anapiga vyombo vya muziki katika bendi ya kanisa la 'Salvation Army'. Ilikuwa ni huzuni kubwa hakuna mtu aliyeenda kupiga nyimbo aliyopenda.

Nilikuwa nasoma maoni ya marafiki zake ambao walisoma wote na wafanyakazi wenzake katika mtandao wa Facebook.

Katika msiba wa kidigitali, watu walituma salamu za rambirambi na kuzungumzia namna Chris alivyokuwa mtu mwema.

Na nilidhani labda nipige picha yale maoni na kuchapisha kama kitabu cha salamu za rambirambi.

Kila kitu kilikuwa tofauti, hatukuweza kukumbatiana, kushikana mikono au kufutana machozi.

Mercy Juma
BBC
The Facebook Live failed so I could not watch Chris’ final journey to the very end"
Mercy Juma
BBC reporter

Hatukuweza kutoa heshima za mwisho kwa kumuangalia mara ya mwisho katika jeneza lake.

Mpendwa wako anapofariki huwa tunataka kupata faraja na haikuepo na isingewezekana kwa sababu hatukuwa pamoja.

Nilisikitika sana na kukasirika. Sikuwahi kuvuta fikra kuwa ningeweza kumzika mpendwa wangu kwenye mtandao wa kijamii. Ilikuwa kama filamu ukiachilia tu kuwa nilikuwa miongoni mwa waigizaji.

Na mbaya zaidi Facebook Live ilikata hata kabla mazishi hayajamalizika, kulikuwa kuna matatizo ya mtandao.

Hivyo sikuweza kuangalia safari ya mwisho ya Chris mpaka mwisho. Sikuona jeneza likifunikwa.

Katika jamii nyingi za kiafrika, kifo na mazishi ni jambo ambalo linagusa jamii kwa ukaribu sna. Tamaduni nyingi wanaona kuwa ni njia ya kuelekea maisha mengine.

Kwa mababu zetu- kuna watu ambao walikufa lakini bado wanaishi katika jamii zetu.

Hii ina maanisha kuwa mtu anapokufa anapaswa kuagwa vizuri katika mazishi yake na ndio nmekuwa nikiona hivyo kizazi kwa kizazi.

Kwa jamii ya watu wa magharibi mwa Kenya eneo ambalo nimetokea kama mluo au mluhya, mtu akifa na mazishi yake yanakuwa tukio muhimu sana.

Mazishi yanakuwa kama sherehe 10 tofauti za mwisho

Mfu anapewa heshima kubwa na baada ya mazishi yake inafuata sherehe kubwa ya kumuaga.

Kwanza mazishi yote huwa hayaharakishwi, haswa pale wazee wanapofariki. Kifo kinatambuliwa kama sherehe, yaani majonzi na huzuni katika sherehe.

Coronavirus
Getty Images
Coronavirus: Key facts

  • Spreadswhen an infected person coughs droplets into the air

  • Virus-packed droplets can be breathed in

  • Dropletscan also land on a surface

  • Touching surface and then eyes, nose or mouth creates risk

  • Washing of hands is therefore recommended after touching surfaces

Source: BBC

Msiba wa mtu mzima huwa unachukua angalau wiki nzima .

Watu wanahuzunika kwa kelele na vilio kwa siku kadhaa.

Watu wanajumuika kwa pamoja na kuomboleza kumpoteza mpendwa wao.

Moto huwa unawashwa usiku ambapo watu wanalala nyumbani kwa mfiwa wakiwa wanafarjiana, wanalia na kumuombe mtu aliyetangulia.

Ngo'ombe na mbuzi huchinjwa ili chakula kingi na vinywaji kutolewa kwa ajili ya kuwafariji wafiwa. Vilevile huwa inaonyesha umoja wa majirani.

Maiti huwa inaletwa nyumbani siku moja au mbili kabla ya kuzikwa.

Chanzo cha picha, Courtesy of Mercy Juma

Maelezo ya picha,

Watu 10 pekee ndio walioruhusiwa kuhudhuria mazishi

Huwa wanailaza katika nyumba kuonyesha ishara kuwa walimpenda na wamekubali kifo chake.

Kwa kabila la waluo, kutoka magharibi ya Kenya, ni miongoni mwa watu wenye tamaduni ya aina yake ya kuzika kwa kifahari nchini Kenya.

Yaani huwa kuna kama sherehe 10ambazo huwa zinajumuisha matangazo ya kifo , kuna sherehe ya kuondoa kivuli cha roho ya marehemu nyumbani, kunyoa nywele kwa wafiwa, na mwisho sherehe za kumbukumbu ya marehemu.

Matukio yote hayo yanahitaji watu kujumuika kwa pamoja kwa wingi.

Lakini kwa wakati huu wa mlipuko wa corona, taratibu zote ambazo zilizoeleka zilikatazwa kufanyika katika mazishi yeyote yawe ya mtu aliyefariki kwa corona au sababu nyingine ya kifo.

'Niliomboleza mwenyewe'

Wakati wa siku mbili za kifo cha Chris na maziko yake' , watu walikatazwa kuimba kwa nguvu usiku kwa sababu wangeweza kuwafanya majirani wajongee katika msiba na kuomboleza na wafiwa.

Hakuna moto uliowashwa na watu kuuzunguka. Na wakati wa mazishi hakuna aliyekaribia jeneza, hakuna kukumbatiana, kushikana mikono, kugusana na kubusiana.

Wawakilishi wa serikaliwalikuwa hapo kuhakikisha sheria zote za kutokaribiana zifuatwa.

Chanzo cha picha, Courtesy of Mercy Juma

Maelezo ya picha,

Kawaida waombolezaji hurusha michanga kidogo ndani ya kaburi

Siku arobaini baada ya marehemu kuzikwa, huwa kuna ibada ya kumbukumbu na hiyo huwa inapaswa kuwa sherehe yake ya mwisho. Sisi tena hatutaweza kumuona tena Chris na hatutaweza kumuaga kama taratibu za tamaduni zetu zinavyotaka .

Ninahisi sijamaliza kuhuzunika kumpoteza Chris. Hakupaswa kuagwa namna hii na alihitaji kuzikwa vyema Zaidi.

Labda corona ikiisha na tukirudi katika maisha tuliozoea- tunaweza kukumbatiana, kulia pamoja na kuomboleza kifo chake kama ilivyopaswa.

Pia unaweza kutazama:

Maelezo ya video,

Wachezadensi wa Ghana wanaosindikiza wafu wanaovuma mtantaoni