Virusi vya corona: Mashine ya kupima corona 'yakutwa na hitilafu Tanzania'

@umwalimu

Chanzo cha picha, @umwalimu

Wizara ya afya nchini Tanzania imetangaza kwamba uchunguzi wa serikali uliokuwa ukifanywa katika maabara kuu ya nchi hiyo umebaini kuwa moja ya mashime ya kupima corona ilikuwa na hitilafu.

Waziri Ummy Mwalimu hii leo ametangaza matokeo ya uchunguzi aliyoagiza kufanyika baada ya Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kutilia shaka ufanisi wa maabara hiyo.

"Kamati imebaini kuwepo kwa mapungufu ya uendeshaji wa kitaaluma katika upimaji wa vipimo na uhakiki wa ubora wa majibu'' amesema Waziri Mwalimu.

Pia kumebainika kuwepo kwa udhaifu katika uhifadhi wa vipimo vya covid-19, aidha imebainika kuwepo kwa upungufu wa Wataalamu"- Waziri Afya Ummy mwalimu amesema.

Wizara ya afya nchini humo imeweka wazi kwamba sasa vipimo vitakuwa vinafanyika katika maabara iliyopo mabibo.

"Kuanzia sasa shughuli zote za upimaji wa maabara ya taifa zitafanyika katika maabara mpya ya mabibo yenye vifaa vya kisasa vyenye ubora na uwezo wa kupima sampuli 1,800 ndani ya saa 24"- amesema Ummy Mwalimu.

Kulingana na wizara hiyo, maabara iliyotumika awali na kukutwa na mapungufu ilikuwa na uwezo wa kupima sampuli 300 kwa saa 24 na ilianzishwa mwaka 1968 katika ofisi za NIMR, mtaa wa Obama DSM, na sasa imeamamrishwa kupima magonjwa mengine.

Vipimo vinavyotumika kupima corona Tanzania havina hitilafu (CDC)

Pamoja na majibu hayo ya uchunguzi wa kamati maalum, Mei 7 Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (CDC) kilisema kwamba vifaa vya kupimia virusi vya corona nchini Tanzania havina shida yeyote.

"Vipimo ambavyo Tanzania inatumia tunajua kwamba vinafanyakazi vizuri," Dkt. John Nkengasong alisema hivyo katika mkutano na wanahabari wa njia ya mtandao.

Kauli hiyo ya Mkuu wa Africa CDC, inapingana na kauli ya rais wa Tanzania ambaye alisema huenda vipimo hivyo vikawa na matatizo.

Kituo hicho cha Africa CDC pamoja na wakfu wa Jack Ma, Shirika la msaada la bilionea wa China, lilisambaza vifaa hivyo, Nkengasong alisema na kuongeza kwamba viliidhinishwa na wanachojua ni kwamba vinafanyakazi vizuri.

Kituo hicho kiko chini ya Umoja wa Afrika na kina majukumu ya kuratibu mapambano dhidi ya mlipuko wa mangonjwa barani Afrika.

WHO inasema nini?

Kwa upande wake Shirika la Afya Duniani kupitia Mkuu wake wa bara la Afrika Dkt Matshidiso Moeti lilisema halikubaliani na kauli ya Rais Magufuli kuwa vifaa vya kufanyia vipimo vya corona vina maambukizi ya virusi.

''Tunaamini kwamba vifaa vya kufanyia vipimo vilivyotolewa vinazingatia ubora wa kimataifa na vimenunuliwa kupitia WHO na zile zilizotolewa kama msaada na Jack Ma hazijaingiwa na virusi'' alisema Dkt. Moeti

Aliongeza kusema, ''Samahani sikubaliani na kauli ya [Rais wa Tanzania] kwamba vifaa vya kufanyia vipimo vilivyopo vina maambukizi ya virusi. Kwa kweli hatukubaliani na kauli hiyo.

Mashaka ambayo alikuwa nayo Rais magufuli

Rais Magufuli akihutubia taifa hilo, alitilia mashaka ufanisi wa vifaa vya kupima corona katika maabara kuu ya nchi hiyo.

Rais Magufuli aliwahi kuwa na hofu na hivyo kutuma sampuli kadhaa ambazo hazikuwa za binadamu katika maabara ya taifa hilo ili kupima ubora na usahihi wa majibu ya mashine hizo katika vipimo vya ugonjwa huo.

''Sampuli hizo zilipewa majina ya binadamu na kupelekwa bila ya wataalamu wa maabara kujua kuwa si za bidanamu'', ameeleza Magufuli.

Sampuli ya oili ya gari ilipewa jina la Jabiri Hamza na haikukutwa na corona. Sampuli ya Tunda la fenesi ilipewa jina la Sara Samuel majibu yake hayakukamilika, sampuli ya papai iliitwa Elizabeth na kukutwa na corona.

Sampuli ya ndege kwale pia ilikutwa na corona pamoja na mbuzi pia.

"…Lazima ugundue kuna mambo ya ajabu yanafanyika nchi hii. Ama wahusika wa maabara wamenunuliwa na mabeberu, ama hawana utaalamu jambo ambalo si kweli kwa kuwa maabara hii imetumika sana katika magonjwa mengine. Ama zile sampuli zinazoletwa maana vifaa vyote vinatoka nje, hivyo lazima kuna kitu fulani kinafanywa," alisema Magufuli.

Magufuli alisema kutokana na taarifa hizo anaamini kuna watu ambao walipewa majibu yasiyo sahihi.

"Lazima kuna watu wameambiwa positive lakini si wagonjwa wa corona, na inawezekana wengine wakafa kwa hofu. Papai lile lipo halijafa linaiva tu. Mbuzi yule yupo tu hajafa, fenesi lile lipo tu labda lije kuoza…kwa hiyo natoa wito kwa Watanzania msiwe na hofu…mbona mafua yamekuwepo lakini haya ni makali, nayo yatapita..."