Polisi: Idris Sultan kupandishwa mahakamani kwa makosa ya mtandao kesho

Mchekeshaji Idriss Sultan wa Tanzania alikamatwa siku ya Jumanne juma lililopita
Maelezo ya picha,

Mchekeshaji Idriss Sultan wa Tanzania alikamatwa siku ya Jumanne juma lililopita

Polisi nchini Tanzania imeiambia BBC kuwa kuna uwezekano mkubwa wa mchekeshaji maarufu nchini humo Idris Sultan kupandishwa mahakamani kesho Jumatano kwa tuhuma za makosa ya kimtandao.

Msemaji wa polisi nchini humo, David Misime ameiambia BBC kuwa upelelezi wa makosa ya kimtandao unachukua muda lakini wapo tayari kwa kesho kumpeleka mahakamani.

"Unajuwa upelelezi wa makosa ya mtandao yanachukua muda mrefu lakini wataalamu wetu wamefanya jitihada kubwa sana. Tunategemea kesho kufanya maamuzi ya kumfikisha mahakamani ama ikishindikana basi atapewa dhamana ili kuvuta muda wa kmfikisha mahakamani ila tuha uhakika kuwa kesho tutampeleka mahakamani," Bw Misime ameiambia BBC.

Leo Jumanne imetimu wiki moja kamili toka mchekeshaji huyo na mshindi wa zamani wa shindano la Big Brother Africa kushikiliwa na polisi bila dhamana.

Bw Sultan aliitwa polisi baada ya mkanda wa video kusambaa mitandaoni hivi karibuni akionekana akiicheka picha ya zamani ya rais Magufuli.

Je, polisi wanamtuhumu na nini mchekeshaji huyo?

Bw Misime ameambia kuwa mchekeshaji huyo anahusishwa na tuhuma tatu, kufanya makossa ya kimtandao, kujaribu kuharibu ushahidi na kutumia nambari ya simu ambayo haijasajiliwa kwa jina lake.

"Tulipomuita kwa mahojiano ya kufanya makosa ya kimtandao, tukagundua kuwa kuna makosa ambayo tunaona ameyatenda, lakini kibaya zaidi tukagundua alipoitwa kuna ushahidi aliuharibu ili kuficha ukweli…la tatu tumebaini kuwa alikuwa akitumia namba ya simu ambayo imesajiliwa kwa jina la mtu mwingine, tunafikiri alifanya hivyo ili kutenda makosa hayo ya kimtandao ambayo tulikuwa tunamhoji nayo."

Wiki iliyopita, wakili wa Bw Sultan, Bennedict Ishabakaki aliiambia BBC kuwa mteja wake anahojiwa na polisi kwa kosa la "uonevu/unyanyasaji wa kimtandao" baada ya "kuicheka picha ya Rais John Pombe Magufuli" na hivyo kutuhumiwa kuvunja kifungu cha 23 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 kinachokataza uonevu wa kimtandao.

Kosa hilo kwa kingereza linatambulika kama 'cyber bullying'.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu akikutwa na hatia ya kutenda kosa hilo anaweza kuadhibiwa faini ya Shilingi milioni tano za kitanzania au kifungo cha miaka mitatu au akapewa adhabu zote mbili.

Kumekuwa na kampeni katika mitandao ya kijamii nchini Tanzania ambapo watu kadhaa wakiwemo wanasiasa wa upinzani wa wanaharakati wanatuma ujumbe wa kutaka msanii huyo kuachiwa huru.

Kampeni hiyo inaendeshwa kwa kutumia anuani maalumu ya mtandao ya #FreeIdrisSultan.

Ruka Twitter ujumbe, 1

Mwisho wa Twitter ujumbe, 1

Hii ni mara ya pili kwa mchekeshaji huyo kuingia matatani kwa kutumia picha ya rais Magufuli katika sanaa yake.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alimuamuru kuripoti polisi baada ya kubadili picha yake na ya magufuli.

Makonda alidai kuwa msanii huyo hatambui mipaka ya kazi yake. Hata hivyo aliachiwa baadae bila kupandishwa mahakamani.