Moline Odwar: Anapokuwa kwenye hedhi wakati mwengine hata huzirai

Moline Odwar
Maelezo ya picha,

Moline Odwar: 'Hedhi yangu inaweza kuchukua hadi siku 15'

Siku ya hedhi Duniani ni siku ambayo emetengwa kuangazia umuhimu wake katika maisha ya mwanamke.

Inakadiriwa kwamba wastani wa wanawake kupata hedhi ni katika mzunguko wa siku 28.

Hedhi pia imepewa majina tofauti kulingana na sehemu mtu alipo mfano, mashiro - aunty -kunyesha na kadhalika.

Lakini je hatua hii hedhi kupewa majina mbadala pengine kwa kuzingatia kabila, eneo ulipo na mengine ni katika hali ya kukejeli au kujaribu kuficha hali halisia ya maumbile ya mwanamke kutokwa na damu kila mwezi?

Cha msingi ni kufahamu kwamba kuna baadhi ya wanawake ambao katika siku za mwezi mmoja, nusu ya mwezi huo au hata zaidi huwa wako katika hedhi.

Hii inaashiria kwamba wanawake hupitia siku za hedhi kwa kutofautiana kulingana na uhalisia wa mwili wa mtu.

Moline Odwar ni mwanamke anayeishi na ugonjwa unaofanya hedhi zake kuwa tofauti na wanawake wengine.

Wakati Molline Odwar alipopata hedhi kwa mara ya kwanza miongo miwili iliyopita, ilikuwa ishara kwamba alikuwa amekomaa.

Alitazamia ingekuwa ni wakati wa kukumbukwa kwa fahari na ujasiri kama mwanamke aliyevunja ungo.

Badala yake mambo yalikuwa tofauti na simulizi alizowahi kuzisikia awali. Kwa Molline hedhi ilikuwa ni mchakato wenye maumivu makali na uchungu ajabu. Hedhi zake zilikuwa nzito na zenye kutoka kwa siku nyingi.

Hali hii yake imesababishwa na ugonjwa au hali inayojulikana kama Von Willebrand kwa kiingereza.

Maelezo ya picha,

Moline Odwar ana ugonjwa unaofahamika kama Von Willebrand

Von Willebrand ni ugonjwa gani?

Von Willebrandni ugonjwa ambao unafanya hedhi kuwa nzito mno na kutoka kwa muda mrefu unaoweza kudumu hata kwa wiki mbili au zaidi.

Hali hii ya Von Willebrand ni ugonjwa ambao huathiri wanawake na wanaume. Na kwa mwanamke maokeo yake ndio ndio hayo, kutokwa na damu kupita kiasi.

Awali, haikuwa rahisi Moline kuzungumzia hali yake lakii hi leo, amepata ujasiri na kile anachofanya ni kuchukua kila fursa kuhamasisha umma juu ya ugonjwa huu licha ya kwamba tangu jadi katika jamii nyingi ni mwiko hata kuzngumzia hedhi za kawaida tu itakuja kuwa hali kama hii.

Kulingana na wataalam Ugonjwa wa Von Willebrand (VWD) ni shida ya maumbile inayosababishwa na kukosa au kasoro ya chembechembe za von Willebrand factor (VWF) mwilini, yaani proteni inayosaidia damu kuganda au kutofanyakazi kama inayotarajiwa.

Hili huathiri kuta za mishipa ya damu, na mtu kuvuja damu kuliko kawaida.

Kwa kawaida mwili wa binadamu huwa na jinsi ya kujidhibiti wakati kunapotokea ajali, hili huzuia damu kutoka kwa wingi japo kwa watu ambao wana ugonjwa huu mwili huwa haujidhibiti wakati damu inavuja na iwapo mtu anaishi na hali hii anaweza kutokwa na damu puani akatokwa hadi akafariki au kuzirai.

Maelezo ya picha,

Moline Odwar sasa amepata ujasiri wa kuzungumzia hali yake ya kupata hedhi kwa siku hata zaidi ya 15.

Ni changamoto gani hasa anazopitia Moline Odwar.

"Kwa sababu vipindi vyangu ni vya muda mrefu, husababisha uchovu na kichefuchefu kwa kuwa huwa ninapoteza madini aina ya chuma mwilini. Pia kisaikolojia ninakuwa na msongo wa mawazo kwasababu hedhi yenyewe ni nzito mno na inayodumu kwa siku nyingi kila mwezi, kwa kweli sio rahisi "Molline alisema.

Moline akiwa mmoja ambaye anaishi na hali hii ana changamoto za kuhakikisha kuwa katika kipindi cha siku kati 7-15 ambazo anakuwa na hedhi anataulo au pedi za kutosha. Kwa mfano anasema kuwa anatumia pedi zaidi ya 10 kwa siku, hivyo basi inabidi agharamike zaidi katika ununuzi wake.

Kingine ni kuwa kule kutokwa na damu kwa wingi humsababishia yeye kuzirai wakati mwengine au kuhisi kizunguzungu.

Maelezo ya picha,

Moline Odwar akiwa katika hedhi wakati mwengine hata huzirai

Je ugonjwa huu unatiba?

Moline alianza kutafuta majibu ya jinsi ya kudhibiti hali yake, na hata kuvuka mpaka kwa suala hilo, akiwa na matumaini kuwa huo utakuwa mwanzo wa kufungua ukurasa mpya maishani.

Wakati alipokuwa akitafiti mitandaoni juu ya ugonjwa wa Von Willebrand, alikutana na Bi Laurie Kelley ambaye anaendesha warsha na masomo kwa watu binafsi na familia wanaokuwa na shida za kutokwa na damu inayohusiana na ugonjwa huo.

Akiwa alibarikiwa na watoto watatu, mmoja kati ya hao ana hali ya haemophilia, Bi.Laurie ameandika vitabu 11 juu ya tatizo la Haemophilia na kingine kinaangazia ugonjwa wa Von Willebrand, kwa hio yeye amekuwa akishirikiana na Moline katika kuhakikisha kuwa watu wanaelewa tofauti ya kutokwa na damu kuliko ilivyo kawaida na jinsi ya kukabiliana na hali hiyo.

Kwa hio Moline alisafiri Marekani kusomea zaidi hali anayoishi nayo ilimradi awe kielelezo kwa wanawake wengine.

kwa sasa yeye ni mwanaharakati wa maswala haya na amehamasisha wengi jinsi ya kuishi na hali hii na ni yepi ya kuzingatia.

Ugonjwa huu wa Von Willebrand hujitokeza zaidi kwa wanawake kwasababu wanakuwa na damu ya kila mwezi na pia wakati wanapojifungua watoto.

Lakini pia hauna tiba ingawa matibabu yanaweza kusaidia kuzuia au kusitisha damu kutoka kabisa kulingana na matibabu atakayopewa mgonjwa.

Na kwake Moline Dunia inaposherehekea siku hii ya hedhi ni muhimu hamasisho zaidikuendelezwa kwa wanawake ambao huenda wanatokwa na damu kwa siku nyingi, bila wao kujua kuwa wana ugonjwa unaosababisha hayo.