Virusi vy corona: Idadi ya vifo yafikia 100,276 Marekani

A healthcare worker wheels the body of a deceased person into a makeshift morgue near a hospital in New York. File photo

Chanzo cha picha, Reuters

Idadi ya wagonjwa waliofariki kutokana na virusi vya corona nchini Marekani imepita 100,000 katika kipindi cha chini ya miezi minne.

Taifa hilo limeandikisha vifo vingi zaidi ya taifa lolote lile huku watu milioni 1.69 wakithibitishwa kuambukizwa virusi hivyo idadi ambayo ni asilimia 30 ya maambukizi yote duniani.

Maambukizi ya kwanza nchini Marekani yaliripotiwa mjini Washington tarehe 21 mwezi Januari.

Kote duiniani kumekuwa na watu milioni 5.6 walioambukizwa virusi hivyo huku idadi ya vifo ikifikia 354,983 tangu mlipuko wa virusi hivyo kuzuka mjini Wuhan nchini China mwisho wa mwaka jana.

Kufikia sasa idadi ya waliofariki nchini Marekani imefikia 100,276, kulingana na Chuo kikuu cha John Hopkins mjini Maryland ,ambacho kimekuwa kikifuatilia mlipuko huo.

Muhariri wa BBC katika eneo la Marekani ya kaskazini Jon Sopel anasema akwamba idadi hiyo ni sawa na idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouawa katika vita vya Korea, Vitenam, Iraq na Afghanistan katika kipindi cha miaka 44 wakipigana.

Hatahivyo Marekani imeoredheshwa ya tisa duniani kwa kiwango cha watu wanaofariki nyuma ya Ubelgiji, Uingereza , Ufaransa na Ireland kulingana na chuo hicho.

Je takwimu za taifa hilo zinasema nini?

Majimbo 20 yaliripoti kuongezeka kwa kesi mpya kwa wiki iliokuwa inaisha siku ya jumapili, kulingana na utafiti wa Reuters.

Jimbo la North Carolina , Wisconsin na Arkansas ni miongoni mwa yale yanayoandikisha ongezeko la wagonjwa wanaofariki.

Hatahivyo idadi ya wanaofariki inaendelea kuongezeka katika miji mikuu ikiwemo Chicago, Los Angeles na makaazi ya Washingtin DC.

Hatahivyo idadi ya wanaofariki katika majimbo yalioathirika zaidi imeanza kupungua ikiwemo New York ambapo watu 21,000 wamefariki.

Wakati wa kilele cha maambukizi hayo katika mji huo, idadi ya vifo vya kila siku ilikuwa mamia.

Hospitali ziishindwa kuhimili idadi hiyo huku vyumba vya kuhifadhi maiti kwa muda mfupi vikijengwa nje ya hospitali hizo.

Je janga hilo limekabiliwa vipi kisiasa?

Rais Donald Trump amesisitiza kwamba iwapo utawala wake usingechukua hatua yoyote idadi ya vifo ingekuwa mara 25 zaidi ya ilivyo sasa ijapokuwa wakosoaji wake wamemkosoa kwa kuchelewa kuchukua hatua.

Magavana pia wamelaumumiwa kwa kutochukua tahadhari za mapema kwa tisho la virusi hivyo katika nyumba za wazee.

Awali , rais huyo wa chama cha Republican alipuuza mlipuko huo akiufananisha na mlipuko wa homa ya msimu.

Mapema mwezi Februari alisema kwamba Marekani imedhibiti virusi hivyo na kwamba ifikiapo mwezi Aprili vitakuwa vimeisha.

Alitabiri kwamba kutakuwa na vifo 50,000-60,000 kabla ya ugonjwa huo kudhibitiwa kabisa.

Chanzo cha picha, Reuters

Utafiti kutoka chuo kikuu cha Columbia mjini New York umesema kwamba chini ya watu 36,000 wangekuwa wamefariki iwapo Marekani ingechukua hatua za mapema.

Joe Biden, ambaye huenda akawa mpinzani wa rais Trump katika uchaguzi wa Novemba alitoa ujumbe moja kwa moja wa familia zilizowapoteza wapendwa wao siku ya jumatano.

''Kwa wale wanaoendelea kuomboleza , poleni'', makamu huyo wa rais wa zamani alisema kupitia mtandao wa Twitter. ''Taifa linaomboleza nanyi''.

Je makali ya amri ya kutotoka nje yanapunguzwa vipi?

Huku karibia raia milioni 39 wakikosa kufanya kazi wakati huu wa mlipuko, Marekani inaendelea kuondoa polepole masharti hayo kutoka jimbo moja hadi jingine ili kuufungua uchumi wa virusi vya corona licha ya idadi ya vifo kuendelea kuongezeka.

Majimbo yote 50 yameanza kupunguza masharti ya Covid-19 kwa njia moja au nyengine.

Bustani kubwa ya burudani duniani Walt Disney mjini Florida, ina mipango ya kufunguliwa mwezi Julai, iwapo gavana wa jimbo hilo atakubali.

Maeneo manne ya kucheza kamare mjini Las Vegas yanayomilikiwa na hoteli ya MGM Resort pia yanatarajiwa kufunguliwa Julai 4.

Kampuni hiyo inasema wafanyakazi watafanyiwa vipimo vya Covid-19 mara kwa mara. Kufikia sasa hakuna chanjo ya ugonjwa huo.

Pia hakuna tiba iliothibitishwa kutibu virusi hivyo lakini dawa kadhaa zinafanyiwa vipimo.

Kura ya maoni ya AP-NORC, iliofanywa mwezi huu imebaini kwamba asilimia 49 ya Wamarekani wanasema watapata chanjo ya corona.