Virusi vya corona: Picha za wanaotoroka vituo vya karantini kuchapishwa magazetini Kenya

Mutahi kagwe

Chanzo cha picha, MINISTRY OF HEALTH KENYA/TWITTER

Maelezo ya picha,

Waziri wa Afya Kenya asema wanaotoroka karantini kuchukuliwa hatua

Serikali ya Kenya inatengeneza muongozo wa uangalizi salama wa wagonjwa wa virusi vya corona wakiwa nyumbani.

Kulingana na waziri wa afya Mutahi Kagwe serikali inachukua hatua hiyo ili kupunguza msongamano katika hospitali za umma ili kuzuia kujaa kupitia kiasi.

''Hospitali za Mbagathi na Kenyatta zinakaribia kujaa . Wagonjwa wengi waliothibitishwa ni wagonjwa wa pumu na wanaweza kutibiwa kutoka nyumbani'', alisema waziri huyo.

Kagwe alitoa tangazo hilo huku wagonjwa wengine 124 wakithibitishwa kuwa na virusi hivyo hatua inayofanya idadi ya wagonjwa walioambukizwa virusi hivyo nchini Kenya kufikia 2,340.

Picha za wanaotoroka karantini kuchapishwa magazetini

Serikali imetishia kutoa picha za wagonjwa wa Covid -19 waliotoroka vituo vya karantini katika vyombo vya habari.

Kagwe amesema kwamba hatua hiyo itachukuwa wajibu muhimu ili kuwasaidia raia kuwatambua wale walio hatari kwao.

Kagwe amesema kwamba wale wanaotafutwa wamebadilisha mbinu na wameamua kuzima simu zao na kuendelea kutangamana na raia na hivyobasi kuhatarisha maisha ya wengine.

'Unapozima simu yako , na kutoka Kawangware na kuelekea Thika na kurudi huku marafiki zako wakitupigia simu' , hiyo ina maana gani, alisema Kagwe.

Aliongezea, "Tunapofikia wakati ambapo tuna thibitisho kwamba unatoroka , hakuna chochote kinachoweza kuizuia wizara kuchapisha picha zako magazetini.

Alisema kwamba picha zitaandamana na maelezo yanayosema kwamba mgonjwa huyu ametoroka katika kituo cha karantini na hivyobasi ni mtu hatari kwa umma.

Waziri huyo amesema kwamba wagonjwa sita waliotoroka karantini Turkana walitafutwa na kurudishwa katika kituo hicho.

Kaunti ya Elgeyo Marakwet ndio kaunti ya hivi karibuni kupata maambukizi ya ugonjwa huo.

Kufikia sasa jumla ya kaunti 36 zimerekodi wagonjwa wa maambukizi hayo.

Wagonjwa hao wapya waligunduliwa baada ya wizara kufanyia vipimo sampuli 2640.

Mombasa yathibitisha wagonjwa 40 wapya

Maelezo ya picha,

Waziri wa afya Mutahi kagwe amesema kwamba wale watakaotoroka karantini picha zao zitawekwa magazetini

Kati ya wagonjwa hao wapya 40 wanatoka Mombasa, 38 kutoka mji mkuu wa Nairobi , 26 kutoka Busia . 6 kutoka Kajiado, 3 kutoka Kiambu, 2 kutoka Garissa, 2 kutoka Taita Taveta , 2 kutoka Murang'a na mmoja kutoka Elgeyo Marakwet.

Mjini Mombasa wagonjwa 14 wameripotiwa katika eneo bunge la Mvita, 11 kutoka eneo bunge la Kisauni, 6 kutoka eneo bunge la Changamwe, 1 kutoka Nyali na mmoja kutoka Jomvu.

Mjini Nairobi, eneo bunge la Kibra limethibitisha wagonjwa 25, Kamukunji wagonjwa 4, Dagoretti wagonjwa 5 , Langata mgonjwa 1 na Embakasi mashariki mgonjwa 1.

Bwana Kagwe alitangaza kwamba wagonjwa wengine wanne walifariki kutokana na ugonjwa huo na hivyobasi kufanya idadi ya waliofariki kufikia 78.

tunaendelea kukupasha...........