Virusi vya corona: Nairobi na Mombasa zaendelea kufungwa

Rais Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta ametangaza kuongeza marufuku ya kutotoka nje nchini Kenya, shughuli za usafiri katika kaunti ya Nairobi na Mombasa zimesitishwa kwa siku 30 zaidi.

Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi, bwana Kenyatta ameondoa marufuku ya kutotoka nje katika maeneo ya Eastleig, na Old Town kuanzia saa kumi asubuhi tarehe 7, Juni, 2020.

Kaunti za kwale na Kilifi pia zinafunguliwa kuanzia saa kumi asubihi 7, Juni 2020 kwa sababu maambukizi yameanza kupungua katika maeneo hayo.

Wakati huohuo, rais amelegeza masharti ya kutotoka nje usiku ,hatua ya kusalia ndani sasa itaanza kuwanzia saa tatu usiku hadi kumi asubuhi.

Bwana Kenyatta amefafanua kuwa kama kulegeza masharti kwa asilimia 20 kungesababisha maambukizi laki 2 na vifo 30,000 kufikia Desemba.

" Ikiwa masharti yangelegezwa kwa asilimia 60, kilele chake kingefikia Oktoba na maambukizi 450,000 na vifo 45,000," rais amesema.

Rais ameelezea mifano ya nchi zingine kama Korea Kusini, Pakistan na Malaysia na kuweka bayana kwamba ukosefu wa mchakato makhususi wa kufungua tena shughuli maambukizi yanaweza kuongezeka zaidi au kupata wimbi la pili la maambukizi.

Kwa mifano ya Kenya, kituo kilichotengwa cha Siaya kina vitanda kumi na tayari watu 9 wamelazwa ambapo kituo cha Busia kilichotengwa kuhudumia wagonjwa wa Covid-19 kina vitanda 34 na kituo hicho kilijaa wagonjwa siku mbili zilizopita.

Tangazo lingine ni shule kufunguliwa kuanzia Mosi, Septemba.

Baada ya kushauriana na washika dau wa elimu, rais amesema wizara ya elimu pamoja na ya afya, itatangaza mwongozo mpya wa elimu na kuonesha vile hali ya kawaida katika taasisi za masomo itakavyorejelelewa taratibu kuanzia muhula wa tatu kuanzia Septemba mosi, 2020. Wizara ya elimu pia itatarajiwa kutangaza kalenda mpya ya shule katikati ya Agosti.

Chanzo cha picha, Reuters

Rais amedokeza kwamba haikuwa kazi rahisi hata kwa timu yake ya wataalamu juu ya suala la kufunga au kufungua uchumi wa nchi.

"Lazima tukubali kwamba sio suala la kuwa uko sahihi au hauko sahihi, tumejikuta katika yote mawili ambayo ni sawa. Wale wanaotaka kufungua uchumi wako sahihi na wale wanaopinga ufunguaji wa uchumi pia wako sahihi," amesema.

Rais ameelezea kwamba hata yeye ni furaha na nia yake kufungua uchumi wakati huu kama ilivyo kwa raia.

Rais ametaka watu kuwa wa kweli na hali jinsi ilivyo na kusisitiza kwamba ikiwa hatua zilizopo hazingechukuliwa hali ingekuwa mbaya zaidi.

"Lazima tuambiane ukweli. Kiwango cha maambukizi Kenya kingekuwa juu sana ikiwa si kwa hatua tulizochukua awali."

Rais ameongeza kwamba ikiwa nchi haingechukuwa hatua hizo, maambukizi yangefikiwa kilele chake mwisho wa Agosti ambapo wakenya karibia 75,000 wangekuwa wamepoteza maisha yao huku maambukizi yakifikia zaidi ya 800,000.

Rais Kenyatta ametangaza kwamba ndani ya siku saba, wizara ya mambo ya ndani na ya afya, zitazungumza kuweka mikakati ya kufunguliwa kwa shule na maeneo ya kuabudu.

Pia rais ameongeza marufuku ya safari za kimataifa kulingana na jinsi ugonjwa huo unavyoendelea kote duniani.

"Wakati huohuo, Wizara ya usafiri imeagizwa ndani ya siku saba kushauriana na washika dau muhimu na kuunda mwongozo wa kurejelelewa kwa usafiri wa ndege ndani ya nchi," amesema.

Wakati huohuo, amearifu umma kwamba maambukizi ya virusi vya corona kwa sasa hivi yamefikiwa 2,600 baada ya kugudunduliwa kwa maambukizi mapya 126 ndani ya saa 24 zilizopita.