Virusi vya Corona: Dawa ya kutibu malaria ya hydroxychloroquine sio tiba ya corona

Anti-malarial drugs

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Hydroxychloroquine ilipata umaarufu duniani baada ya rais Donald Trump kuzinywa

Dawa ya kutibu malaria ambayo imefanyiwa majaribio ya uwezo wake wa kutibu virusi vya corona hainusuru maisha ya watu, majaribio makubwa kuwahi kufanyika duniani yabainisha.

Dawa ya Hydroxychloroquine imekuwa ni yenye kupata angalizo kubwa kuhusu uwezo wake wa kutibu virusi vya corona baada ya Donald Trump kuipigia debe kisha kukatokea utata baada matokeo ya utafiti wa dawa hiyo yaliyokuwa yamechapishwa mitandaoni kuondolewa.

Majaribio ya dawa hiyo ambayo yalikuwa yanaongozwa na Chuo Kikuu cha Oxford kwa wagonjwa wenye virusi vya corona kwa sasa hivi yamesitishwa nchini Uingereza.

Utafiti juu ya dawa hiyo umekabidhiwa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mwanzoni kwa janga la corona, utafiti wa maabara ulionesha kwamba dawa ya kutibu malaria huenda ikaathiri virusi. Utafiti mdogo uliofanywa na China na Ufaransa ukaonesha kwamba inaweza kusaidia wagonjwa.

Kulikuwa na matumaini makubwa kwasababu dawa hiyo ni rahisi na pia imekuwa salama katika matumizi ya kutibu ugonjwa wa malaria na magonjwa mengine kama mapaku mekundu ngozini (lupus) na ule wa yabisi kavu (arthritis).

Hata hivyo, ushahidi wa kuunga mkono matumizi ya dawa hiyo kutibu virusi vya corona yamekuwa hafifu siku baada ya siku.

'Sio dawa ya ugonjwa wa Covid-19'

Hiyo ndio sababu data inayoonesha waliopona ni muhimu. Ni ya kwanza kufanyiwa majaribio kwa idadi kubwa ya watu waliokuwa hospitali.

Zaidi ya wagonjwa 11,000 wa Covid-19 wanashiriki kwenye majaribio huku wagonjwa 1,542 wakipewa dawa ya hydroxychloroquine.

Kwasababu ya utata unaotokana na matumizi ya dawa hiyo ambao unazidi kuongezeka, wadhibiti wa dawa hiyo Uingereza, jana usiku waliomba watafiti kutoka Oxford kupitia tena data yao.

Matokeo yalionesha kwamba asilimia 25.7 ya watu wanaotibiwa kwa dawa ya hydroxychloroquine walikufa ndani ya siku 28. Ikilinganishwa na asilimia 23.5 ya wagonjwa waliopewa matibabu ya kawaida hospitalini.

"Hii sio dawa ya Covid-19," amesema Profesa Martin Landray, ambaye anashiriki majaribio ya dawa hiyo. Mara moja matumizi ya dawa hiyo yakasitishwa.

Utafiti huo unawadia wakati ambapo kuna wasiwasi mkubwa kuhusu jarida la kitaaluma lililopelekea makala ya jarida la Lancet kuondolewa - moja ya majarida maarufu ya kimatibabu.

Jarida hilo lilikuwa limechapisha utafiti unaoonesha karibia wagonjwa 15,000 kutoka mamia ya hospitali waliotibiwa kwa dawa ya hydroxycholoroquine au dawa sawia na hiyo ya chloroquine.

Jarida hilo lilihitimisha kwamba dawa hiyo haisaidi badala yake inaongeza hatari ya kupata matatizo ya moyo na kutokea kwa kifo.

Makala hiyo ilipelekea Shirika la WHO kusitisha majaribio ya dawa ya kutibu malaria kuangalia kama ina uwezo wa kutibu Covid-19.

Data hiyo pia ilikuwa imekusanywa kutoka hospitali na kampuni moja ya masuala ya afya ambayo haifahamiki na wengi ya Surgisphere.

'Kukatishwa tamaa'

Wasiwasi umeibuliwa kuhusu data hiyo huku baadhi ya wanaoongoza tafiti hizo wakisema hawawezi kutetea makala walizochapisha kwasababu kampuni ya Surgisphere haikuruhusu mapitio tena huru ya utafiti wao.

Kisha jarida la kimatatibabu la New England likaondoa tena makala nyingine mtandaoni ambayo ilikuwa imechapisha iliyokuwa na data kwa mujibu wa kampuni ya Surgisphere.

Profesa Peter Horby, kutoka Chuo Kikuu cha Oxford ambaye anaendesha majaribio kuangalia idadi ya waliopona, alisema: "Hydroxychloroquine na chloroquine zimevutia angalizo kubwa na pia zimetumika kwa kiwango kikubwa kama tiba kwa wagonjwa wa Covid licha ya ukosefu wa ushahidi thabiti juu ya ufanisi wa dawa hiyo.

"Ingawa inakatisha tamaa kwamba imebainika kuwa dawa hii haikuonesha ufanisi, inatoa fursa ya kuangazia zaidi utafiti na matokeo katika dawa zengine."