George Floyd: Maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi yafanyika Marekani

Waandamanaji jijini Washington DC wamesema hawataacha kushinikiza mabadiliko

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Waandamanaji jijini Washington DC wamesema hawataacha kushinikiza mabadiliko

Maandamano makubwa ya amani yamefanyika kote nchini Marekani kupinga ubaguzi wa rangi na unyanyasaji unaotekelezwa na maafisa wa polisi ikiwa ni siku ya 12 ya maandamano yaliosababishwa na kifo cha George Floyd.

Makumi ya maelfu ya watu waliandamana mjini Washington DC ikiwa ndio maandamano makubwa kufanyika katika mji huo kufikia sasa.

Makundi ya watu pia yaliandamana mjini New York, Chicago, LA na San Fransisco. Wakati huohuo , watu walitoa heshima zao kwa Floyd katika jimbo la North Carolina, ambapo alizaliwa kabla ya ibada ya kumbukumbu yake kufanywa.

Bwana Floyd mtu mweusi ambaye alikuwa hana silaha , alifariki katika mikono ya polisi katika mji wa Minneapolis tarehe 25 mwezi Mei. Picha ya video ilimuonesha afisa wa polisi ambaye ni mzungu akiwa ameweka goti lake kwenye shingo ya Floyd kwa zaidi ya dakika tisa akiwa amekandamizwa barabarani

Afisa wa polisi Derek Chauvin amefukuzwa kazi na kushtakiwa kwa kutekeleza mauaji. Maafisa wengine watatu ambao walikuwepo katika eneo hilo pia walifutwa kazi na kushitakiwa kwa kusaidia na kuunga mkono kilichokuwa kikiendelea.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Sarina and Grace Lecroy ni miongoni mwa waandamanaji wanaowaunga mkono watu Wamarekani weusi

Maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi wa rangi pia yalifanyika katika baadhi ya mataifa mengine. Nchini Uingereza, katika bustani ya bunge katikati ya mji wa London, kulikuwa na watu wengi licha ya wito wa serikali kutokongamana kwa hofu ya kusambaa kwa virusi vya corona.

Nchini Australia , kulikuwa na maandamano makubwa katika miji ya Sidney na Melbourne na Brisbane yalioangazia jinsi raia wenye chimbuko la Australia walivyokuwa wakinyanyaswa. Pia kulikuwa na maandamano nchini Ufaransa, Ujerumani na Uhispania.

Je ni nini kilichotokea katika maandamano?

Maandamano makubwa zaidi yalifanyika mjini Washington DC ambapo waandamanaji waliokuwa wakibeba mabango yalioandikwa 'Black Lives Matters' - walikongamana kwa amani karibu na mji mkuu, katika eneo la kumbukumbu la Lincoln na nje ya bustani ya Lafayette , karibu na ikulu ya Whitehouse karibu na jumba jipya kwa jina Black Lives Matter Plaza.

Meya Muriel Bowser aliwakaribisha waaandamanaji akisema kuwa watu hao walituma ujumbe kwa rais Trump.

Siku ya Jumatatu , maafisa wa polisi walirusha vitoa machozi hewani ili kuwatawanya waandamanaji katika eneo hilo kabla ya ya rais huyo kuingia katika kanisa lililopo eneo hilo.

Chanzo cha picha, AFP/GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Mjini San Francisco, waandamanaji walifunga kwa muda geti la daraja

"Iwapo anaweza kuzuia chochote kufanyika Washington Dc basi anaweza kufika katika jimbo lolote na hakuna hata mmoja wetu atakayekuwa salama'', alisema.

''Wanajeshi wetu hawafai kutumiwa jinsi hii hawafai kutakiwa kuwasukuma raia wa Marekani''. Bi Bowser alikuwa ameomba kuondolea kwa maafisa wote wa polisi wa kijimbo na wale wa kitaifa katika mji huo, akisema kuwa uwepo wao hauna maana.

Mtu mmoja aliyekuwa akiandamana mwenye umri wa miaka 35, Eric Wood, aliambia BBC: Niko hapa kwasababu sikuweza kukosa kuwa hapa.

''Ubaguzi umekuwa miongoni mwetu kwa muda mrefu nchini Marekani''.

Crystal Ballinger , mwenye urmi wa miaka 46, alisema kwamba anahisi kuwa na matumaini kuhusu maandamano hayo wakati huu.

''Nahisi kitu tofauti kuhusu maandamano haya....nina matumaini kwamba ujumbe wa umoja na usawa unazidi kuwafikia wengi''.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mjini Chicago, baadhi ya waandamanaji walipeperusha bendera juu chini

Amri ya kutotembea nje zilizokuwa zimewekwa zimeondolewa katika maeneo mengi . Ukamataji wa watu kiholela umepungua.

Hatahivyo baadaye siku ya Jumamosi katika jimbo la Portland , Oregon walitangaza maandamano hayo kuwa mikutano isio halali na ukiukaji wa sheria baada ya maafisa wa polisi kushamabuliwa .

Maafisa wa polisi wa Seattle pia walisema kwamba vitu vilivyokuwa vikirushwa na waandamanji viliwaathiri maafisa wa polisi.