Virusi vya corona: Rais Magufuli asema ana imani ugonjwa wa corona umeondolewa kwa nguvu za Mwenyezi Mungu

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA

Maelezo ya picha,

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Rais wa Tanzania John Magufuli ametoa ujumbe wa shukrani kwa viongozi wa dini na watanzania wote kwa kuitika wito wa kumuomba Mungu ili aliepushe taifa na janga la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona, na kusema kuwa ana imani kuwa ugonjwa wa corona umeondolewa kwa nguvu za Mwenyezi Mungu.

Rais Magufuli ameeleza hayo alipokuwa akitoa salamu kwa waumini wa kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Chamwino jijini Dodoma, Jumapili hii leo.

''Palipo na Mungu hakuna kinachoshindikana, kwa niaba ya serikali niwashukuru watanzania wote ambao wengi walifunga, wengi walitubu, na wengi walisali na kuswali kwa ajili ya kumtanguliza Mungu mbele na mimi nina amini na nina uhakika watanzania wengi wanaamini kwamba ugonjwa wa corona katika nchi yetu umeondolewa kwa nguvu za Mwenyezi Mungu''.

''Leo humu wote tumekaa simuoni aliyevaa barakoa, hata wewe baba Paroko hujavaa chochote kufunika pua na mdomo wako hata injili isingetoka vizuri, umemtanguliza Mungu, hata wakati wa kutukomunisha hukuvaa chochote mkononi kwa sababu Mungu ni muweza wa yote''. Alisema Magufuli.

Maelezo ya picha,

Waumini wakiwa kanisani

Pamoja na hayo amewataka watanzania kuendelea kuchukua hatua ambazo wanazichukua kama vile kujifukiza na shughuli nyingine kujikinga.

''Miti ilibarikiwa na Mungu na kutumia miti katika hatua mbalimbali pia ni ushuhuda wa pekee wa maarifa tuliyopewa na Mungu, watanzania madawa wanayo lakini tunadharau madawa yetu, madawa ya watanzania ni madawa halisi kwa sababu yana mkono wa Mungu''.

Rais Magufuli aliwaomba raia wa taifa hilo kutumia siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Aprili 2020, kumuomba Mwenyezi Mungu ili kuwaepusha na janga la ugonjwa wa corona.

Katika chapisho lake la mtandao wa Twitter Magufuli aliwataka raia wa taifa hilo kusali na kwa imani yake Mungu atawasikia.

Maelezo ya video,

Virusi vya corona:Rais Magufuli atoa maagizo ndege za kubeba watalii kuingia