Virusi vya corona: Je wanasayansi wamebaini nini?

Uchunguzi wa virusi vya corona
Maelezo ya picha,

Uchunguzi wa virusi vya corona

Uchunguzi wa mlipuko sio kama wa mtu aliyetekeleza mauaji. Ni mchakato wa kukimbia kwenye tukio kabla ya ushahidi uliopo haujapotea; walioshuhudia wanahojiwa - kisha shughuli ya kutafuta na kudhibiti kinachosababisha vifo inaanza kabla ya mlipuko kuongezeka.

Licha ya juhudi kuendelezwa hata katika ngazi ya kimataifa, virusi vya corona bado vinaendelea kusababisha vifo kwa maelfu ya watu kila siku.

Miezi sita sasa imetimia, je wanasayansi wamebaini nini katika juhudi zao za kudhibiti mlipuko huo?

Kuanza kuonyesha tahadhari

Kuelewa kiini cha virusi vyovyote ni muhimu ili kutabiri athari zake kiafya na vile unavyoweza kusambaa kwa haraka.

Lakini kuanzia mwanzo, virusi vya corona viliingia kwa namna iliyoshangaza ulimwengu,

Dunia ilikuwa imejitayarisha kukaribisha mwaka mpya, Dr. Li Wenliang alikuwa anafanya kazi katika idara ya dharura hospitali kuu ya Wuhan pale wagonjwa wote wakiwa wanaugua -homa ya mapafu - na kulazwa.

Akizungumza na wafanyakazi wenzake katika kundi lililoundwa kwenye mtandao wa WeChat Desemba 30, alishirikisha wengine hofu yake - kwamba je hiyo homa hiyo inaweza kuwa mlipuko mpya wa ugonjwa wa Sars (ugonjwa unaosababisha matatizo katika mfumo wa kupumua)?

Sars, aina nyingine ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona, mara ya kwanza uligundulika nchini China 2003 na kusambaa hadi nchi 26 ambapo watu zaidi ya 8,000 waliambukizwa.

Hatahivyo, Dr. Li alikuwa amebaini kwamba huu haukuwa mlipuko wa pili wa ugonjwa wa Sars bali mlipuko wa kwanza waugonjwa wa virusi vya corona (Sars- Cov-2).

Siku tatu baada ya kushirikisha wenzake kwa njia ya mtandao kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mlipuko, Dr. Li alikamatwa na polisi pamoja na wenzake wengine wanane, kwa kusambaza uvumi kulingana na vyombo vya habari vya China.

Muda mfupi baada ya kurejea kazini, Dr. Li, 34, alipata ugonjwa wa COvid-19. Aliaga dunia Februari na kuacha mke wake mja mzito na kijana mmoja.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Maafisa wa afya wakimwanalia mgonjwa wa corona

Kilichotokea kwenye eneo la chimbuko la corona

Kipindi cha wiki za mwisho wa Desema 2019, wakati ambapo madaktari na wauguzi zaidi pamoja na Dkt. Li walipoanza kutoa onyo juu ya uwezekano wa kutokea kwa mlipuko, ni wahudumu wa afya waliobaini kwanza kwamba kuna tatizo - kwa kuwa idadi kubwa ya wagonjwa walikuwa wanafanyakazi katika soko la kuuza vyakula vya baharini la Huanan.

Akiwa katika eneo jipya la mji, soko la vyakula vya baharini la Huanan lilikuwa kitovu cha wafanyabiashara wadogo wanaouza kila kitu kuanzia kuku, samaki, wanyama wa baharini na wengine wa mwituni.

Wakati waathirika wengi zaidi wa virusi walipokuwa wanaibuka, Desemba 31, Tume ya Afya ya Wuhan ikarekodi ripoti yao rasmi ya kwanza mjini Beijing.

Siku iliyofuata, soko hilo likawekwa kwenye karantini.

Leo hii, wanasayansi kwa kauli moja wanaamini kwamba mlipuko mkubwa ulitokea katika soko hilo la vyakula vya baharini lakini ikiwa hapo ndio chanzo cha virusi vya corona hilo bado halijathibitishwa.

Vipimo vilivyochukuliwa kutoka kwa Wanyama na binadamu katika soko hilo vimethibitishwa kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

Hata hivyo kulingana na watafiti wa kimatibabu mjini Wuhan, waathirika wa kwanza wa virusi vya corona walikuwa wameanza kubainika wiki nne kabla ya kujulikana na mlipuko huo kwenye soko la kuuza vyakula vya baharini: mwanaume mzee kutoka Wuhan aliyekuwa ameanza kuonesha dalili mapema Desemba mosi, 2019 wala hakuwa na uhusiano wowote na soko la kuuza vyakula vya baharini la Huanan.

Januari, wafanyakazi wa afya mjini Wuhan walianza kushuhudia idadi kubwa ya watu walioathiriwa na virusi vya corona katika hospitali mbalimbali za mji huo, lakini hakuna aliyeweza kutabiri kwamba kasi ya kusambaa kwa virusi hivyo sio tu nchini China lakini pia kote barani Asia.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Dokta Li Wenliang

Siku tisa tu baada ya kuripotiwa kwa kifo cha kwanza cha mwenye ugonjwa wa Covid-19, Januari 11, waathirika wapya tayari walikuwa wameanza kubainika kuanzia China hadi Japani, Korea Kusini na Thailand.

Hapo sasa ndio shughuli ya kuanza kumtafuta muuaji ilipoanza, ambapo, licha ya maendeleo yote yaliyopatikana duniani katika sekta ya matibabu na teknolojia, bado tuko hatua moja nyuma...

Ndani ya kipindi cha miezi sita tu, ugonjwa wa Covid-19 ulikuwa umesambaa kwa nchi 188 na kuambukiza watu zaidi ya milioni 6.6 ndani ya miezi sita.

Kuanza kumtafuta muuaji

"Swali letu la kwanza kawaida ni,'' ni nini?" anasema Profesa wa masuala ya kinga ya mwili Kristian Andersen.

Maabara ya Andersen imebobea katika magonjwa yenye kuhusisha chembe za urithi. Walichunguza vile virusi hivyo vinavyoweza kuhama kutoka mnyama hadi kwa binadamu na kusababisha milipuko mikubwa.

Mwishoni mwa Januari, ndani ya saa kadhaa kwa wale waliokuwa wanalazwa hospitalini, vipimo vilivyochukuliwa kwa njia ya pua vilikuwa vinatathminiwa na wanasayansi katika Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Virusi ya Wuhan.

Walikuwa wanatafuta vinasaba vyake - ambavyo vinaweza kuonesha hasa huo ni ugonjwa ni upi na vile unavyoweza kusambazwa.

Kawaida, utafiti wa vinasaba vya virusi huchukua miezi kadhaa hata miaka kukamilika, hata hivyo, kasi ya utafiti wa vinasaba vya virusi vya corona haikuwa ya kawaida na Januari 10, wanasayansi katika taasisi ya Utafiti wa Virusi ya Wuhan - ikiongozwa na Profesa Yong-Zheng Zhang - ilichapisha matokeo yake ya kwanza yanayoonesha mtiririko wa vinasaba vilivyopatikana katika ugonjwa wa Covid-19 na kuzua mjadala upya.

"Baada tu ya kuona utafiti wa kwanza, mara moja tukabaini kwamba huu ni ugonjwa wa aina ya virusi vya corona - na kwamba ulikuwa unafanana na ugonjwa wa Sars kwa asilimia 80," anasema Profesa Andersen.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Maafisa wa polisi nje ya soko la Huanan

Virusi vya corona ni familia kubwa ya virusi huku mamia ya virusi hivyo vikifahamika kuwa miongoni mwa wanyama kama nguruwe, popo na paka. Ugonjwa wa Covid-29 ni wa saba kuaminika kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu.

"Swali letu la pili lilikuwa je ugonjwa huu unaweza kugundulika vipi? - na hilo likasababisha shughuli ya upimaji kuelewa namna virusi hivyo vinavyosambaa," anasema Profesa Andersen.

"Na swali la tatu likawa je ni jinsi gani tunaweza kutengeneza chanjo dhidi ya virusi hivyo? Maswali yote yakiwa yanaweza kujibiwa na matokeo ya uchunguzi wa vinasaba vya virusi."

Profesa Anderson anasema kuna ushahidi mkubwa tu kwamba chanzo cha virusi hivyo ni popo.

"Bila shaka ugonjwa huu ulianza kwa popo. Tunatambua hili kwasababu kuna ulinganisho mkubwa wa virusi hivyo kwa popo," anaelezea. "Kile tusichokijua ni vile ugonjwa huo ulivyofika kwa binadamu."

Nchini China, siku mbili tu baada ya kutoa matokeo ya utafiti wa vinasaba vya ugonjwa wa Covid-19 kwa wengine duniani, maabara ya Profesa Zhang ilifungwa na mamlaka ya eneo na ikapokonywa leseni ya kufanya utafiti. Kulingana na vyombo vya habari vya China, hakuna sababu maalum iliyotolewa lakini mchango wa timu hiyo kuhusu utafiti wa ugonjwa huu duniani tayari ulikuwa umeanza kufanyiwa kazi.

Kutafuta, kubaini na kutenga wagonjwa

Wakati janga hilo lilikuwa limeshika kasi, angalizo likahama kutoka chanzo cha ugonjwa huo hadi namna unavyoweza kudhibitiwa.

Wanasayansi wakaanza kufuatilia virusi hivyo kwa njia mbili: wachunguzi wakaanza kufuatilia mtu mmoja mmoja na kuwatenga ambao walidhaniwa kupata maambukizi; wakati huohuo, wataalamu wakaanza kufuatilia vinasaba vya virusi vya corona ili kuelewa zaidi vile ulivyokuwa unasambaa kwa harakaa kote duniani.

Maelezo ya picha,

Profesa Kristian Andersen

Kutafuta watu wanaodhaniwa kupata maambukizi

Korea Kusini, taifa la watu milioni 51, ni miongoni mwa yanayochukuliwa kufanikiwa duniani katika kuudhibiti ugonjwa wa virusi vya corona.

Mafanikio yake yalitokona na uwezo wake wa kutafuta waliodhanikiwa kupata maambukizi: wachunguzi waliwatafuta wahusika pamoja na wale waliokuwa wamewasiliana nao hivi karibuni.

Kisha wataalamu wanaowatafuta wanaamua ni kina nani wa kujitenga wenyewe au kuweka karantini jingo zima au shirika kama vile hospitali au makazi ya kuhudumia wazee au hata ofisi.

Ikiwa imebaini kiasi kidogo tu cha watu walioambukizwa Januari na Februari, raia wengi wa Korea Kusini walidhani kwamba wameepuka milipuko mikubwa.

Hata hivyo kufikia Februari mwisho, mji mmoja ukawa na maambukizi elfu kadhaa nda iya siku chache tu.

Wagonjwa 31 walibainika kupata maambukizi ya virusi va corona kufikia Februari 17.

Lakini wanaotafuta walioambukizwa walifanikiwa kubaini wote waliokuwa wamewasiliana nao na la kushangaza ni kwamba ikatokea kuwa zaidi ya watu 1,000 ndani ya siku 10 - walipatikana na kuhitajika kujitenga wenyewe hivyo basi kusaidia kukwepa mlipuko mkubwa.

Kanisa la Shincheonji Church of Jesus lenye wafuasi karibia 300,000 kote nchini humo, lilidai kwamba mwasisi wake Lee Man-hee, ndio anayekuja baada ya Yesu Kristo nayeye tu ndio mwenye uwezo wa kufasiri bibilia.

Wengi nchini humo wamekuwa wakikashifu kanisa hilo kwa madai kwamba ni dhehebu fulani lenye kuendesha itikadi zao na kulishtumu kwa kusajili vijana wengi.

Lakini mgonjwa wa 31 alikuwa maarufu sio tu kwasababu alikuwa na uhusiano na kanisa la Shincheonji licha ya kwamba alikuwa anaonesha dalili, siku 10 kabla ya kupimwa alisafiri katika mji wa Daegu na kukaribiana na watu zaidi ya 1,000.

Baada ya kupata ajali Februari 6, mgonjwa huyo wa 31, alilazwa hospitalini Februari 7 ambapo alikutana na watu 128.

Maelezo ya picha,

Watoa huduma ya afya

Kisha akajiondoa hospitali kwa mud ana kurejea nyumbani kuchukua vitu vyake, safari ya saa mbili unusu kabla ya kurejea hospitali.

Baadae wiki hiyo akatika hospitalini mara kadhaa na kwenda kula chakula cha mchana na rafiki zake, na mara mbili akahudhuria ibada kanisani kwa saa mbili lililokuwa na mkusanyiko wa watu kama 1,000.

Kwasababu ya usiri wa kanisa la Shincheonji, Profesa Kim anasema kigumu zaidi ilikuwa kuchunguza nani mwengine alihudhuria ibada wiki hiyo.

"Lakini hatimae, mamlaka ikafanikiwa kupata orodha yote ya majina ya watu 9,000 wa kanisa hilo.

Mara ya kwanza tulianza kuwapigia simu na kuwauliza ikiwa walikuwa na dalili za virusi vya corona.

Karibia 1200 walisema wanazo lakini baadhi walikataa kupimwa au kujitenga wenyewe."

Kwasababu mamia ya waumini hawakuwa tayari kutoa siri zao, Profesa anasema hakuwa na budi.

"Ilikuwa ni suala la tunaweza kutenga vipi watu wa kanisa hilo na wengine wanaoishi kwenye mji wa Daegu. Kwahiyo serikali ikatoa amri kwa makanisa yote kujitenga."

Na waathirika wapya wakawa wanafuatiliwa kwa karibu, wanapimwa na kwa haraka mji huo ukadhibiti maambukizi hadi kufikia mapema Aprili, mji wa Daegu haukuwa umeripoti kisa chochote cha corona.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wahudumu wa afya wakiwa kwenye mavazi ya kujikinga dhidi ya maambukizi

Tishio lisiloonekana

Kifo cha kwanza Italia cha Covid-19 kilitokea katika mji mdogo wa Vo eneo la Vento. Eneo hilo ni kaya kwa watu 3,000.

Baada ya kifo cha kwanza Februari 21, mamlaka ya eneo iliamua kufunga Kijiji kizima na kuanza kufanya vipimo kwa wakazi licha ya kwamba walikuwa wanaonesha dalili au la.

Na baada ya utafiti kufanywa ulioongozwa na Profesa mshiriki Enrico Lavezzo. Anasema muhimu walichobaini ni kusambaa kwa ugonjwa huo kimya kimya.

"Zaidi ya asilimia 40 ya watu waliokuwa na virusi, hawakuwa na hofu kwamba wanaweza kusambaza ugonjwa huo kwa wengine. Hili ni tatizo kubwa hasa katika suala la kudhibiti magonjwa ya kuambukiza,'' anasema Profesa Lavezzo.

"Wengi walioonesha dalili wanaishi nyumbani lakini wale wasiokuwa na dalili walikuwa wanaendesha shughuli zao kama kawaida. Wangeenda nje, wangekutana na watu na kuchangamana na wengine - bila hata kujua kwamba wanaweza kusambaza virusi kwa wengine."

Maelezo ya picha,

profesa Enrico Lavezzo

Mchanganyiko wa magonjwa wa kukatisha tamaa

Wanasayansi wamebaini kwamba virusi hivyo vinaweza tu kuingia ndani ya mwili kwa njia moja, kushika vitu na kuusambaza hadi kwa seli za mwanadamu.

Maabara ya Profesa Michael Farzan ilikuwa ya kwanza kubaini namna hiyo ya kuambukiza kwa virusi vya corona wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Sars 2003.

Lakini, Michael anaeleza kwamba viini vinapatikana katika kila sehemu ya mwanadamu, ndani ya pua, mapafu, utumbo, hata kwenye moyo, figo na ubongo.

Mara nyingi virusi ama huwa vinasambaa wa haraka au vinaweza kusababisha ugonjwa mbaya. Covid-19 ni ugonjwa mbaya sana kwasababu una yote hayo.