Tanzania: Kiongozi wa upinzani Freeman Mbowe avamiwa na kushambuliwa

Mbowe na Zitto

Chanzo cha picha, Chadema

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA Freeman Mbowe amevamiwa na kushambuliwa na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake jijini Dodoma.

Msemaji wa Chadema Tumaini Makene, ameithibitishia BBC tukio hilo ambalo lilitokea usiku wa Jumatatu.

Kiongozi huyo wa Chadema anaendelea kupata matibabu katika moja ya hospitali zilizopo jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika amevieleza baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania kuwa shambulio hilo lina sura ya kisiasa. Mnyika hata hivyo amesema kuwa taarifa zaidi zitatolewa baadae.

Shambulio dhidi ya Bwana Mbowe linakuja siku moja baada ya mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu kutangaza rasmi nia ya kuwania urais kupitia chama cha Chadema.

Chanzo cha picha, Getty Images

Ingawa Chadema inalihusisha shambulizi hili na siasa, lakini polisi nchini humo imesema italifanyia uchunguzi na kuomba watu kamwe wasilisihusishe na siasa.

Shambulio hili limepokelewaje?

Viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, wanaona kama tukio hilio ni mwendelezo wa kushambuliwa kwa viongozi wao.

Baadhi yao wamekuwa wakitumia mitando ya kijamii kuelezea kugutushwa kwao na shambulio dhidi ya Bwana Mbowe.

''Nimepokea taarifa za kushambuliwa kwa mwenyekiti wa kitaifa wa Chadema na kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni Mh. Freeman Mbowe kwa mshutuko mkubwa. Nitatoa taarifa rasmi kuhusu shambulio hilo la kioga saa saba saa za Afrika Mashariki'' aliandika katika Twitter yake mwanasiasa wa upinzani Tundu Lissu.

Chanzo cha picha, Tundu Lissu/Twitter

Septemba 2017, Lissu alishambuliwa vibaya kwa risasi jijini Dodoma na kulazimiki kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu.

Mbowe ni nani?

Freeman Mbowe ni mbunge wa jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni Tanzania.

Mbowe ni moja ya wanasiasa walioasisi uanzishwaji wa Chadema mwaka 1992, wakati huo akiwa kijana.

Alichaguliwa kuliwakilisha jimbo la Hai kwa mara ya kwanza mwaka 2000. Mwaka 2005 aligombea urais na kumaliza nafasi ya tatu nyuma ya Prof Ibrahim Lipumba wa CUF na aliyeibuka mshindi Jakaya Kikwete wa CCM.

Mwaka 2010 alirejea kwenye ubunge na kuchaguliwa tena 2015.

Mbowe yupo madarakani kama kiongozi mkuu wa Chadema kwa zaidi ya miaka 15 sasa.

Kwa wafuasi wake, anaonekana ni kiongozi mahiri aliyeweza kuiongoza Chadema kutoka chama kidogo cha upinzani kuwa kuwa wapinzani wakuu. Kutoka kuwa na wabunge watano mpaka 50.

Mbowe pia amekuwa moja ya wakosoaji wakuu wa serikali ya rais John Pombe Magufuli, hatua ambayo inampa sifa ya uthabiti. Hata hivyo, kwa wapinzani wake ndani na nje ya Chadema wamekuwa wakimshutumu kiongozi huyo kwa kuminya demokrasia ndani ya chama chake.