Ghadhabu Afrika kusini baada ya mwili wa mwanamke kupatikana ukining'inia kwenye mti

Tshegofatso Pule

Chanzo cha picha, @Keba99

Maelezo ya picha,

Tshegofatso Pule alitoweka kwa siku nne kabla ya mwili wake kupatikana

Hashtag ya #JusticeForTshego imekuwa ikisambaa nchini Afrika Kusini kufuatia mauaji ya kinyama ya Tshegofatso Pule, 28.

Mwili wake uliokuwa umechomwa kisu ulipatkana ukining'inia kwa mti karibu na mji wa Johannesburg.

Bi Pule alikuwa na ujauzito wa miezi minane, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari ambavyo vimenukuu tamko la polisi.

Afrika Kusini imekuwa ikishuhudia viwango vya juu vya dhulma dhidi ya wanawake. Mwaka jana Cyril Ramaphosa alisema taifa hilo "ni mahali hatari kwa wanawake duniani ".

Takwimu zilizotolewa mwaka jana zinaonesha kuwa wanawake 2,930 waliuawa katika kipindi cha miezi 12- kuanzia 2017 hadi 2018, kumaanisha mtu mmoja aliuawa kila baada ya saa tatu.

Bi Pule alitoweka wiki iliyopita na mwili wake ulipatikana Jumatatu, kwa mujibu wa ripoti za gazeti la Sowetan.

Gazeti hilo pia lilimnukuu msemaji wa polisi kapteni Kay Makhubele akisema kuwa uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo cha kifo hicho.

Baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mtandao wa kijamii wa Twitter, kuwaomba polisi kuwasaka waliotekeleza unyama huo, lakini pia wakihoji mfumo wa haki utahakikisha Bi Pule anatendewa haki.

Mwaka jana, visa vya mauaji dhidi ya wanawake vilisababisha msururu wa maandamano ya watu waliokuwa wakishinikiza mamlaka nchini Afrika Kusini kuchukuwa hatua.

Tangu wakati huo mahakama maalum ya kushughulikia uhalifu wa uhalifu wa kingono zilifunguliwa tena - baada ya kushindwa kufanya kazi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na changamoto za kifedha, kulingana na ripoti ya mwandishi wa BBC Pumza Fihlani mjini Johannesburg.

Juhudi zaidi zimeelekezwa katika uimarishaji wa usalama kwa waathiriwa wa unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na miradi inayofadhiliwa na serikali ambayo inalenga kubadili tabia ya wanaume, nasema mwandishi wetu.