Virusi vya corona: Changamoto za gharama ya intaneti barani Afrika

A silhouetted man types on his phone in low light conditions

Chanzo cha picha, Reuters

Ugonjwa wa covid-19 umesababisha mataifa mengi barani Afrika kufunga maeneo mengi yakiwemo ya biashara na burudani ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Hii imeleta ongezeko la matumizi ya intaneti - iwe ni masomo kupitia mtandao, kutekeleza majukumu ya kikazi kutoka nyumbani, shughuli za mawasiliano na hata sekta ya afya.

Omar Abdallah ni mwanablogi kutoka Mombasa, na anasema kumekuwa na ongezeko la watu wanaotembelea tovuti yake ya OmmyDallah.com kupata taarifa za burudani. Hata hivyo, maazimio yake ya kukuza tovuti hiyo yamekumbwa na changamoto.

''Kazi yangu inategemea sana intaneti, lakini kuna tatizo kubwa la bei. Wakati mwingine unapata kwamba kampuni moja ya mawasiliano iko na intaneti yenye kasi nzuri, lakini bei iko juu sana.

Pia unapata kampuni nyingine ina intaneti ya bei nafuu, lakini sio ya kutegemewa unaponunua,'' anasema Omar.

Chanzo cha picha, EPA

Mbunifu Isaya Yunge ambaye anamiliki kampuni ya SmartKaya kutoka Dar Es Salaam Tanzania anasema amepata njia ya kudhibiti gharama ya intaneti.

''Mimi natumia Fibre ya Tsh 120,000 (52 USD) kwa mwezi ambayo ina kasi ya zaidi ya 40 Mbps, na hii inanifaa sana kwa matumizi ya ofisini na pia nyumbani. La muhimu ni watu kufahamu wanatumia intaneti kwa kazi gani - ofisini, burudani au matumizi ya kawaida - na kisha kununua vifurushi ambavyo vinafaa kwa kazi hiyo,'' anasema Yunge.

Japokuwa matumizi ya intaneti yameongezeka katika wakati huu wa maambukizi ya corona, zaidi ya asilimia 60% ya watu barani Afrika bado hawajafikiwa na teknolojia ya 4G, kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia.

Je, changamoto hizi zinaweza kutatuliwa vipi ili Afrika isibakie nyuma katika mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea?

Rais wa shirika la Internet Society Kenya (ISOC Kenya) Wainaina Mungai anasema makampuni mengi ya huduma za mitandao yanakabiliwa na gharama kubwa ya kuwekeza katika miundombinu hitajika kama vile mabomba na nyaya kutoka mijini hadi mikoani na vijijini.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Watu wakitumia simu za kiganjani

Mtaalamu wa maswala ya intaneti Barrack Otieno anasema ni sharti wanasiasa na viongozi wawajibike katika kuweka sera ambazo zina ondoa vikwazo kwa makampuni ya mawasiliano.

''Viongozi wanafaa kuweka sera ambazo zinapunguza gharama kwa makampuni ya mawasiliano. Njia moja ni kupunguza au kuondoa kodi husika katika kuweka miundombinu,'' anasema Otieno.

Maelezo ya picha,

Kupata huduma za intaneti kulitambulika rasmi na Umoja wa Mataifa kuwa haki ya kimsingi mwaka 2016

Aidha wataalamu wanasema kuna haja ya serikali tofauti kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na makampuni ya mawasiliano ili kuelewa changamoto zilizopo na kukubaliana kuhusu jinsi ya kutatua matatizo hayo kwa njia bora ambayo itawafaa zaidi wananchi.

Pia wanasema serikali zinafaa kuzingatia kuweka huduma za intaneti kama vile Wi-Fi katika maeneo fulani ili wananchi waweze kupata huduma hizo.