Virusi vya corona: Hali ikoje baada ya Tanzania kufungua milango kwa watalii

  • Aboubakar Famau
  • BBC Africa, Tanzania
Tanzania will hope to attract visitors back to its big tourist spots like the Zanzibar
Maelezo ya picha,

Tanzania ina matumaini ya kuvutia watalii katika maeneo yao ya vivutio vya utalii kwenye visiwa vya Zanzibar

Kama nchi zingine zozote zile duniani zinazotegemea utalii, janga la corona limeathiri vibaya sekta hiyo nchini Tanzania.

Lakini kwa sasa hivi hali tofauti baada ya serikali ya Tanzania mwezi uliopita kutangaza kufunguliwa kwa sekta ya utalii.

Tanzania imewaondolea watalii wanaoingia nchini humo karantini ya siku 14, lakini imeweka itifaki za usalama ili kuhakikisha usalama wa wageni na wenyeji.

Mwandishi wa BBC Aboubakar Famau, hivi karibuni alitembelea mkoa wa Arusha kutathmini hali ilivyo.

"Mji wa Arusha, ndio lango kuu la vivutio vya Tanzania na Afrika, kuanzia safari za mbugani na hifadhi mbalimbali za taifa." anasema Famau.

Shughulli nyingi za kiuchumi katika mji huu zinategemea utalii, lakini janga la corona limewafukuza wageni.

Baadhi ya hoteli za kitalii zilifugwa huku maelfu ya wafanyakazi wakibaki na hofu ya maisha ya baadae.

Lakini hivi sasa, kumeanza kuwa na matumaini baada ya wageni kuanza kuja.

''Kiujumla sisi ni kama hali hii imeamsha matumaini mapya kwetu, na kama unavyoona tayari awali palikuwa panafunguliwa duka moja ama mawili sasa hivi kuna maduka kama 20 ambayo yanafunguliwa, mfanyabiashara, George Tarimo.

''Biashara sasa hivi kwa kweli hamna lakini tumefurahi kusikia utalii unafunguka, tumekaa sana nyumbani kwa hiyo tunaomba Mungu iwe hivyo,'' mfanyabiashara Hulder Kioo.

Licha ya changamoto zilizopo lakini baadhi ya wageni hawaoneshi kukata tamaa

"Kwa hakika mimi ni mmoja wa watu ambao hawaamini kwamba kirusi hiki kinaambukiza kwa njia ya upepo na kwamba ni tofauti na mafua mengine tu, sivai barakoa, naishi maisha ya kawaida, lakini bila shaka kuna mambo mingi ambayo yameathiriwa hapa Arusha, hoteli na mighahawa imefungwa, lakini mimi najihisi salama kabisa." amesema mtalii Caren kutoka Sweden.

Maelezo ya sauti,

Ndege za watalii na abiria kuruhusiwa kuingia Tanzania

Katika wakati huu ambapo mighahawa, mabaa na hata hoteli zimeanza kufanya kazi, tahadhari ni muhimu kuzingatiwa.

Pia kumewekwa magari mapya kwa ajili ya wagojwa. Magari ya safari nayo yanapulizwa dawa kabla na baada ya kutoka safari, na hospitali imeongezewa vifaa ili kusaidia wagonjwa.

Hata hivyo, licha ya tahadhari zote zinazochukuliwa, lakini changamoto bado zipo.

Sirili Ako, ni mtendaji mkuu wa chama cha mawakala utalii Tanzania.

''Watalii kwa sasa hivi bado hatuwezi kusema kwamba wameanza kuja kwa kiasi, isipokuwa wachache wamekuja ni kweli, kwahiyo tumefurahishwa sana na hicho na tumeona kwamba wamefurahi kwasababu tumewaona wanatembea na tunawafuatilia.''

Kutokana na tahadhari hizi, bila shaka maisha kwa watalii yatakuwa tofauti kulinganisha na miaka iliyopita.

Purity Munge ni meneja mauzo katika hoteli ya Mt. Meru iliyopo Arusha.

''Sasa hivi haturuhusiwi tena buffe, kwahivyo kila mteja ana hudumiwa na mhudumu mmoja ili kuepuka kuspread huu ugonjwa.''

Wafanyakazi katika mahoteli wanaendelea kuboresha mazingira, lakini wakati huo huo, swali ni je, lini sekta hii itarudi kama iliyokuwa na kurudisha imani katika jamii kama ilivyokuwa awali?