Kifo cha George Floyd : Jenerali Mark Milley aomba msamaha kwa 'kuenda' kanisani na Trump

Majeshi ya Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images

Mkuu wamajeshi nchini Marekani amekiri kuwa alikosea kuungana na Rais Donald Trump wakati wa alipotembea kuenda kanisa lililopo karibu na Ikulu ya Marekani ambalo liliharibiwa na waandamanaji.

Tukio hilo la Juni tarehe moja na ambalo lilizua utata lilionesha "taswira kwamba jeshi linajihusisha na siasa za ndani ya nchi", Jenerali Mark Milley alisema.

Bwana Trump alitembea hadi kanisa hilo na kupiga picha akiwa ameshikilia Bibilia baada ya maandamano ya amani ya kupinga mauaji ya Mmarekani mweusi George Floyd kuvunjwa kwa nguvu.

Hatua ya kutumia wanajeshi kukabiliana na waandamanaji imezua mjadala mkali nchini Marekani.

Trump mara kwa mara alitumia maneno "Utawala wa sheria", kuleta kikosi malum cha ulinzi katika mji mkuu wa Marekani, na kuapa kuwa atawapeleka wanajeshi katika miji mingine ya Marekani huku akilaani maandamano ya vurugu yaliyoshuhudiwa nchini humo.

Baadhi ya maandamano ya kupinga mauaji ya George Floyd mjini Minnepolisi mwezi uliyopita, mwanzoni yalikuwa ya amani lakini baadaye yalikumbwa na vurugu na wizi katika miji tofauti.

Lakini tangu maafisa wanne waliohusika na mauaji hayo kufunguliwa mashitaka, maandamano hayo yamekuwa ya amani, huku wanaharakati wa kimataifa wakiungana kupinga mateso ya polisi na ukosefu wa usawa katika jamii.

Kanda ya video ya mauaji ya Minneapolis inaonesha afisa wa polisi mzungu akipiga goti katika shingo ya Bwana Floyd kwa karibu dakika tisa.

Jenerali Milley amesema nini?

Mkuu huyo wa majeshi alikuwa akizungumzia kuhusu video hiyo wakati wa sherehe ya uzinduzi wa Chuo Kikuu cha Ulinzi nchini.

Alisema: "Sikustahili kuwa hapo. Uwepo wangu hapo wakati wa tukio hilo ilionesha taswira kwamba majeshi yanajihusisha na siasa za ndani ya nchi.

"Kama afisa mkuu wa majeshi ilikuwa makosa na nimepata funzo, natumai nimejifunza kutokana na tukio hilo."

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Jenerali Milley (Kulia) akiwa na rais Trump na waziri wa Ulinzi Mark Esper (Kati)

Jenerali Milley aliongeza kusema: "Lazima tuhakikishe tunatenganisha jeshi letu na siasa ilituendelee kudumisha sifa yetu."

Pia alisema kuwa alighadhabishwa na mauaji ya "kinyama" ya George Floyd.

Jenerali Milley alisema: "Maandamano yaliyofuatia hayakuangazia mauaji hayo tu bali pia yaligusia vitendo visivyokuwa vya haki vilivyotendewa Wamarekani weusi kwa karne kadhaa."

Jenerali huyo alikuwa amevalia sare za kijeshi wakati alipotembea pamoja kuenda katika kanisa hilo na wakosoaji wanasema hatua hiyo iliashiria anaunga mkono utumizi wa wanajeshi dhidi ya waandamanaji.

Waziri wa Ulinzi Mark Esper pia alikuwepo wakati wa matembezi hayo, lakini hajasema kuwa alikosea kufanya hivyo, huku akiwaambia wanahabari kwamba alienda kuchunguza uharibifu uliyofanywa dhidi ya kanisa hilo.

Maafisa wa ngazi ya juu waliambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba Bwana Trump alimgombeza bwana Esper kwa kutoa tamko hilo.

Mvutano kati ya majeshi na Rais

Hii ni ishara ambayo inaonesha mvutano uliopo kati ya Ikulu ya Marekani na majeshi kuhusu namna ya kushughulikia historia ya ubaguzi nchini humo na muamko wa sasa wa kushinikiza mabadiliko.

Hatua hiyo ambayo sasa, Jenerali Milley analijutia, limeweka majeshi katikati ya malumbano ya kisiasa, hasa wakati ambapo nchi inajiandaa kwa uchaguzi mkuu miezi michache ijayo.

Majenerali kadhaa wa zamani wamemkosoa hadharani Bwana Trump kwa jinsi alivyoshugulikia suala ambalo linaangazia haki za binadamu -na usawa kwa Wamarekani weusi.

Waziri wa kwanza wa ulinzi, Jenerali mstaafu James Mattis, alisema hakuwahi quota kwamba siku moja wanajeshi watapewa amri ya kukiuka haki ya kikatiba ya wananchi wenzao.

Lakini tamko lililotolewa na Jenerali Milley, ikizingatiwa nafasi yake katika majeshi ya Marekani, iinaonesha wazi mzozo uliopo kati yake na rais.

Nini kilifanyika siku hiyo?

Maandamano ya amani yalivunjwa katika bustani ya Lafayette iliyopo karibu na White House huku baadhi ya waandamanaji wakipuliziwa maji ya mwasho ili rais na msafara wake upite kuelekea kanisa la St John's Episcopal.

Wakati maandamano ya kupinga mauaji ya Geoge Floyd yalipokuwa yakiendelea, Bw. Trump, alitoa agizo kwa Magavana kutumia kikosi maalum cha ulinzi wa ndani kudhibiti maandamano ''la sivyo atatumia wanajeshi wa Marekani kukabiliana na maandamano hayo".

Bwana Trump, ambaye anajiona kama kipenzi cha wafuasi wa wa kiinjilisti na wapiga kura wakihafidhina, baadaye alitembea hadi katika kanisa lililochomwa siku iliyotangulia na kupiga picha mbele ya kanisa hilo akiwa ameshikilia Bibibilia.

Viongozi kadhaa wa kidini walikosoa hatua hiyo ya Trumpo. Askofu mkuu mwandamizi wa Kanisa la Episcopal, Michael Curry, alimlaumu Bwana Trump kwa kutumia kanisa "kwa maslahi ya kisiasa".