Pierre Nkurunziza: Mahakama yatoa uamuzi wa kuziba ombwe la uongozi Burundi

Mrithi wa Nkurunzinza

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Jenerali Ndiyashimiye kuapishwa kabla ya Agosti.

Mahakama ya kikatiba ya Burundi imeamua kuwa rais mteule Meja Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye aapishwe urais mara moja na hakutakuwa na rais wa mpito.

Toka kutangazwa kifo cha Nkurunziza mapema wiki hii kumekuwa na ombwe la uongozi nchini humo.

Katiba ya nchi hiyo inaeleza kuwa spika wa bunge atatakiwa kuchukua nafasi hiyo kwa mpito pale rais anapofariki. Hata hivyo Spika Pascal Nyabenda hakuapishwa mara moja hali ambayo wachambuzi wametafsiri kama ishara ya msuguano ndani ya chama tawala nchini humo.

Baraza la mawaziri nchini Burundi katika kikao chake cha Alhamisi liliamua kulipeleka suala hilo katika mahakama ya katiba na kutangaza litaongoza nchi kwa pamoja hadi rais mpya atakapoapishwa.

Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano uliokuwa chini ya uongozi wa Makamu wa Rais wa kwanza Gaston Sindimwo.

Chama cha mawakili nchini Burundi kimetoa wito wa kuapishwa mara moja kwa rais mteule.

Wakati mahakama ikitoa uamuzi huo, taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema Rais Mteule Ndayishimiye, pia ni mgonjwa.

Mke wake alipigwa picha akitia saini kitabu cha maombolezo japo Ndayishimiye hajaonekana hadharani.

Ndayishimiye wa chama tawala cha CNDD-FDD aliyechaguliwa Mei 20 awali ilikuwa aapishwe mwezi Agosti.

Huku hayo yakijiri kundi la upinzani linataka uchaguzi ufanywe upya.

Ndiyashimiye ni nani?

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Baadhi ya wachambuzi wanaamini Jenerali Ndayishimiye hatabiriki katika misimamo yake.

Bwana Ndayishimiye ni miongoni mwa waliokuwa waasi wa CNDD-FDD waliojiunga na kundi hilo baada ya kunusurika katika mauaji ya kikabila ya wanafunzi Wahutu katika chuo kikuu cha Burundi mwaka 1995, kufuatia mauaji ya rais Melchior Ndadaye mnamo mwaka wa 1993.

Baadae kundi la CNDD-FDD lilibadilishwa na kuwa chama cha kisiasa ambacho kilianza kushiriki katika mazungmzo ya amani mjini Arusha Tanzania mwaka wa 2000 na kuafikiana kuhusu usitishwaji wa vita.

Wakati kundi la waasi la CNDD-FDD lilipojiunga na serikali mwaka wa 2003, Ndayishimiye tayari alikuwa amepandishwa cheo cha Meja Jenerali, na alihamishwa aende kuhudumu katika makao makuu ya jeshi la taifa.

Ndayishimiye aliteuliwa waziri wa usalama wa ndani na usalama wa umma nchini Burundi baada ya rais Nkurunziza kushinda uchaguzi mkuu wa 2005, na badaye kuhamishwa hadi ofisi ya rais mwaka 2007 ambapo alihudumu kama mshauri wa kijeshi.

Wachanganuzi wa siasa za Burundi wanasema kwamba Jenerali Ndayishimiye ni mtu mwenye msimamo wa kadri asiyekimbilia mambo.

Wakati wa mzozo uliokumba Burundi mwaka wa 2015 kufuatia jaribio la mapinduzi, jenerali Ndayishimiye ni miongoni mwa viongozi wachache waandamizi jeshini ambao hawakutajwa katika orodha ya wale waliohusika katika uhalifu dhidi ya binadamu na mashirika ya kimataifa.

Kuna wale ambao pia wanasema Jenerali Ndayishimiye hatabiriki katika misimamo yake.

Nkurunziza ni nani?

Chanzo cha picha, Getty Images

Pierre Nkurunziza amekuwa mwanasiasa wa Burundi na kuwa madarakani tangu mwaka 2005.

Bwana Nkurunziza, kijana wa aliyekuwa mbunge, alinusurika mauaji 1993 ya wanafunzi wa Kihutu katika chuo kiuu cha Burundi ambapo alikuwa mhadhiri na kujiunga na waasi wa FDD kundi ambalo baadae lilibadilika na kuwa chama tawala cha CNDD-FDD ambacho alikuja akawa kiongozi.

Alikuwa mwenyekiti wa chama tawala cha CNDD-FDD, hadi alipochaguliwa kama rais wa Burundi.

Maelezo ya video,

Safari ya kisiasa ya Pierre Nkurunziza nchini Burundi

Baada ya makubaliano ya Amani ya Arusha kati ya serikali na waasi, Nkurunziza alitajwa kuwa waziri wa mambo ya ndani kabla ya bunge kumchagua kama rais Agosti 2005.

2015, Nkurunziza alichaguliwa katika uchaguzi uliokuwa na utata na chama chake kwa muhula wa tatu madarakani.

Wafuasi wake na wanaompinga Nkurunziza walikosa kukubaliana katika suala la ikiwa ilikuwa halali kwake kugombea tena na maandamano yakafuata.