Bata walioanguliwa kwa mayai ya dukani nchini Marekani

Beep, Peep and Meep

Chanzo cha picha, Charli Lello

Maelezo ya picha,

Beep, Peep na Meep ni bata watatu weupe walioanguliwa kwa mayai ya dukani

Mwanamke mmoja ameangua bata watatu na kuwapa majina ya Beep, Peep na Meep kwa kutumia mayai aliyonunua kutoka duka moja la kufanya manunuzi.

Charli Lello, 29, kutoka Hertfordshire, aliweka mayai hayo kwenye kiangulio ili kupitisha muda wakati ambapo walihitajika kusalia nyumbani kwasababu ya virusi vya corona.

Amesema bata hao watakuwa na maisha mazuri kwa pamoja na kuku wake wadogo.

Msemaji wa duka hilo alisema, mayai ambayo yanaweza kuangua ni salama kwa matumizi na hayawezi kutofautishwa na mayai ya kawaida labda tu yawekwe kwenye kiangulio.

Chanzo cha picha, Charli Lello

Maelezo ya picha,

Charli Lello aliamua kutumia mayai ya dukani kuangua bata kama njia moja ya kujipa shughuli kipindi hiki akiwa nyumbani

Bi Lello, ambaye kawaida anafanya kazi kama naibu meneja katika duka hilo, alipata wazo baada ya kuona video ikisambaa kwenye mtandao wa Facebook iliyomuonesha mtu mmoja akiangua mayai ya kware aliyonunua kutoka kwa duka kubwa la manunuzi.

"Nilipokuwa katika duka la Waitrose, niliona mayai ya bata nikaanza kufikiria kwamba yanaweza kufanya vizuri pia. Nilikuwa na hamu sana ya mayai haya kuangua lakini pia nilifahamu fika kwamba nimeyanunua dukani.

"Yamechukuliwa, yakatingishwa yakiwa kwenye gari la kuyasafirisha, kisha yakazungushwa yakiwa kwenye toroli wakati yanasubiri kupangwa kwenye rafu za dukani, pia hakuna anayeweza kusema yameokotwa na kurejeshwa na watu wangapi, kwahiyo nilijua kwamba yanaweza yasiangue."

Chanzo cha picha, Trevor the duck/Facebook

Maelezo ya picha,

BataTrevor aliyefariki baada ya kushambuliwa na mbwa

Mwezi mmoja baada ya kuyaweka kwenye kiangulio, Bi. Lello, alisikia sauti kwa mbali na baadae vifaranga vikaanza kujitokeza kutoka kwenye ganda la yai.

Pia ungependa kusoma:

Alisema hiyo imekuwa tajriba nzuri kuona mayai ya dukani yakiangua vifaranga lakini hicho ni kitu ambacho hatakirudia.

"Kilichonifanya nikajaribu ni kwamba kwa sasa hivi niko nyumbani na nina muda wa kuwatunza bata hao hadi pale ambapo hawatanihitaji kuwa nao kila wakati. Kwa mazingira ya kawaida hilo ni jambo ambalo haliwezekani na pia haitakuwa hatua nzuri kwao," amesema.

Chanzo cha picha, Charli Lello

Maelezo ya picha,

Mabata wawili na kasha lao la mayai waliloanzia maisha

Msemaji wa duka la jumla ambapo mayai hayo yalinunuliwa alisema ni vigumu sana kubaini jinsia ya bata wenye manyoya meupe.

Ameongeza pia "Ni jambo la kipekee kwamba mayai ya dukani yameangua. Lakini pia tunatambua kwamba hili sio jambo linalowezekana."