Tanzania imesalia na wagonjwa 66 kwa mujibu wa serikali

Life has hardly changed in Tanzania since the first case was reported

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Nchini Tanzania maisha bado hayajabadilika sana tangu kutangazwa kwa mgonjwa wa kwanza aliyeambukizwa virusi vya corona

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kwamba Tanzania ina wagonjwa 66 wa virusi vya corona nchini humo, hii ikiwa ndio takwimu ya hivi karibuni kutolewa kuhusu ugonjwa huo tangu ilipoacha kutoa takwimu zake Aprili 29.

Bwana majaliwa amesema kuwa wagonjwa 66 wamelazwa katika mikoa 10 na kwamba mikoa mingine 16 haijaripoti mgonjwa yoyote kufikia sasa.

Siku za nyuma, Rais John Magufuli aliwahi kutangaza kwamba ana imani nchi hiyo haina tena maambukizi ya virusi vya corona kwasababu ya maombi ya Watanzania.

Ubalozi wa Marekani mwezi uliopita ulionya kwamba hospitali jijini Dar es Salaam zina wagonjwa wengi na kwamba uwezekano wa kupata maambukizi ulikuwa juu - lakini haukutoa ushahidi wa kuthibitisha madai yake.

Waziri mkuu akizungumza bungeni Jumatatu, alisema kwamba idadi ya maambukizi nchini humo imepungua.

Aliwataka raia wa Tanzania kuendelea kutekeleza mwongozo wa hatua kiusalama uliotolewa kuzuia kusambaa kwa virusi.

Idadi ya walioambukizwa virusi vya corona iliyothibitishwa hadi kufikia sasa bado haijathibitishwa.

Pia unaweza kusoma:

Aprili 29, siku ya mwisho data kutolewa rasmi, serikali ilisema imerekodi waathiriwa 506 ikiwemo vifo 21.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Juni 1, alisema mji wa Dar es Salaam ulikuwa na wagonjwa wanne pekee wa virusi vya corona.

Shule za upili, vyuo na vyuo vikuu zilifunguliwa Juni 1, huku michezo ikiruhusiwa kuendelea na shughuli zake.

Ugonjwa wa corona umeondolewa kwa nguvu za Mwenyezi Mungu

Aidha, Rais Magufuli siku za nyuma aliwaomba raia wa taifa hilo kutumia siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Aprili 2020, kumuomba Mwenyezi Mungu ili kuwaepusha na janga la ugonjwa wa corona.

Katika chapisho lake la mtandao wa Twitter Magufuli aliwataka raia wa taifa hilo kusali na kwa imani yake Mungu atawasikia.

Baada ya tukio hilo,alitoa ujumbe wa shukrani kwa viongozi wa dini na watanzania wote kwa kuitika wito wa kumuomba Mungu ili aliepushe taifa na janga la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona, na kusema kuwa ana imani kuwa ugonjwa wa corona umeondolewa kwa nguvu za Mwenyezi Mungu.

Pia unaweza kutazama:

Maelezo ya video,

Virusi vya corona: Rais Magufuli atoa maagizo ndege za kubeba watalii kuingia