Rais Magufuli atangaza kufungua shule zote Juni, 29

Wanafunzi watakiwa kuvaa barakoa wanapokuwa shuleni
Maelezo ya picha,

Wanafunzi watakiwa kuvaa barakoa wanapokuwa shuleni

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ametangaza rasmi kufunguliwa kwa shule zote nchini humo, Juni 29.

Rais Magufuli pia ametangaza shughuli zote ambazo zilikuwa zimesitishwa kutoka na corona kurudi kama zamani nchini humo.

Rais Magufuli ametangaza wakati akitoa hotuba yake ya kuvunja bunge la 11 la nchi hiyo mapema leo.

Amepongeza namna watanzania walivyochua tahadhari na kushirikiana katika mapambano dhidi ya virusi vya corona ikiwemo Bunge ambalo liliendelea na shughuli zake kama kawaida. ''Pamoja na hofu kubwa iliyokuwepo Bunge hili liliendelea na vikao vyake kama kawaida. Mheshimiwa Spika , bunge hili liliendela kwa ajili ya kuwatumikia wananchi ingawa ninafahamu wapo wachache waliokimbia…na sijui kama wamesharejea lakini niseme tu kwamba kukimbia halikuwa jambo sahihi kwa sababu matatizo au changamoto hazikimbiwi na kukimbia changamoto ni ishara ya udhaifu lakini pia ni ishara ya woga.'' Alieleza Magufuli.

Amesema kuwa mpaka sasa Tanzania imeweza kutatua kwa kiasi kikubwa ikiwemo kupunguza athari zitokanazo na virusi vya corona ikiwemo athari za kiuchumi.''Kama mnavyofahamu benki ya dunia na shirika la fedha duniani yamebashiri kuwa 60% ya nchi za kusini mwa jangwa la sahara zitashuhudia ukuaji hasi wa uchumi mwaka 2020 hata hivyo sisi Tanzania kutokana na hatua tulizochukua, uchumi wetu hautakuwa kwa Negative.'' Alisema Rais Magufuli.

Maelezo ya picha,

wanafunzi

Rais Magufuli amesema kuwa Serikali imeweza kulinda ajira za Watanzania pia kuendelea na miradi yake mikubwa, pia imekua na uhakika wa usalama wa chakula , hali inayoashiria kuwa maamuzi ya kutofunga shughuli za kiuchumi yalikuwa sahihi.

''Namshukuru Mungu kwa kuliepusha taifa hili na virusi vya corona na nina washukuru viongozi wa dini kwa kuitika wito wa serikali kufanya maombi maalum ya kutuepusha na janga la corona.''

''Kutokana na kushuka kwa hali ya maambukizi ya ugonjwa wa corona napenda kutumia nafasi hii kutangaza kuwa shule zote zilizokuwa zimebaki zifungulliwe, lakini pia shughuli zote zilizokuwa zimezuiwa nazo ziendelee'', Alisema. Hata hivyo Rais Magufuli amewasihi Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.