WhatsApp Pay: Facebook yazindua huduma ya kutuma fedha bila malipo

huduma ya kutuma fdha bila malipo

Chanzo cha picha, WhatsApp

Maelezo ya picha,

huduma ya kutuma fdha bila malipo

WhatsApp imezindua huduma ya malipo ya kidijitali nchini Brazil katika juhudi za kutumia umaarufu wake kuingia kwenye masoko yanayoibuka katika ulimwengu wa biashara.

Hatua hiyo inakuja wakati ambapo Facebook ambayo ni mmiliki wa WhatsApp inapania kujikita zaidi kwenye biashara za kidijitali ambazo zitajumuisha mitandao yake yote.

Huduma hiyo inayofahamika kama WhatsApp Pay itawawezesha watumiaji wa mtandao huo kutumiana pesa bila malipo au kununua bidhaa kutoka kwa wafanyibiashara wadogo.

Mwezi Januari, afisa mkuu mtendaji wa Mark Zuckerberg alielezea mpango wa kampuni hiyo kutoa huduma zake India, Indonesia na Mexico.

Katika blogu yake WhatsApp, aliangazia huduma hiyo ikisema uzinduzi wake ni sehemu ya mpango mkubwa wa kuimarisha malipo ya kidijitali kupitia mitandao yote inayomilikiwa na Facebook.

"Kwa sababu huduma ya malipo kupitia WhatsApp inawezeshwa na Facebook Pay, siku zijazo tunataka kuwawezesha watu binafsi na wafanyabiashara kutumia mfumo mmoja wa malipo wakiwa katika programu tumishi ama app za Facebook."

Chanzo cha picha, Reuters

Japo huduma ya malipo kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine haitatozwa ada yoyote wafanyibiashara wadogo watatozwa ada ya "kuwawezesha kupokea malipo kutoka kwa wateja wao," blogu hiyo iliandika.

WhatsApp ina jumla ya watumiaji 120 milioni nchini Brazil, hali inayofanya taifa hilo kuwa soko lake la pili kwa ukubwa baada ya India.

Kampuni hiyo tayari imeanza kufanyia majaribio huduma hiyo ya malipo India, ambako ina watumiaji 400 milioni.

Hata hivyo, juhudi za kampuni hiyo kuzindua huduma ya WhatsApp Pay nchini India imesitishwa kwa miaka miwili kutokana na masuala ya kisheria.

Aprili, Facebook ilitangaza kuwa imenunua 10% ya hisa katika kampuni ya mawasiliano ya Reliance Jio kwa kima cha dola bilioni 5.7 (£4.5bn).

Hatua ambayo iliifanya Facebook kuwa mshirika mkuu wa mwenyekiti wa Reliance Jio, Mukesh Ambani, ambaye ni mtu tajiri zaidi barani Asia.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

watumiaji wa simu

Kampuni hizo mbili zinapanga kupatia kipaumbele ushirikiano wao katika biashara mpya ya Jio, inayofahamika kama JioMart ambayo ilizinduliwa hivi karibuni.

Mwezi uliyopita Facebook iliwekeza kiwango cha fedha ambacho hakikutajwa katika app ya Gojek iliyo na makao yake nchini Indonesia.

Kampuni hizo zitashirikiana kupanua huduma ya malipo ya kidijitali ya Gojek inayojulikana kama GoPay.

Facebook ilinunua WhatsApp kwa karibu dola bilioni 20 mwaka 2014. Kufikia mwezi Februari mtandao huo wa kijamii ulisema kwamba una zaidi ya watumiaji bilioni mbili duniani.