Uamuzi kuhusu kesi ya mauaji ya Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri kutolewa

Hariri, mfanyabiashara bilionea, aliitaka Syria kuondoka nchini Lebanon

Chanzo cha picha, Reuters

Uamuzi uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu utatolewa hii leo dhidi ya wanaume wanne wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Lebanon Rafik Hariri na watu wengine 21 katika shambulio la bomu mwaka 2005.

Watuhumiwa wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kishia wa kundi la Hezbollah nchini Lebanon - walihukumiwa na mahakama maalum huko Uholanzi licha ya kutokuwepo mahakamani.

Hasira iliyojitokeza baada ya shambulio la Beirut ililazimu Syria iliyokuwa inaunga mkono kundi la Hezbollah kuondoa vikosi vyake Lebanon miaka 29 iliyopita.

Hezbollah na serikali ya Syria zilikanusha kuhusika na shambulio hilo.

Zaidi ya watu 220 walijeruhiwa pale gari lililokuwa limejazwa vilipuzi lilipolipuka wakati msafara wa Bwana Hariri ulipokuwa unapita mbele ya ufuo wa Beirut.

Mauaji hayo yalibadilisha Lebanon na kuanza kuchipuka kwa makundi ya upinzani ambayo miaka kadhaa baadae yalibadilisha siasa za nchi hiyo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kijana wa Bwana Hariri, Saad, aliongoza chama kilichokuwa kinapinga Syria na kuunga mkono nchi za Magharibi na yeye mwenyewe akahudumu kama Waziri Mkuu kwa mihula mitatu.

Anatarajiwa kuhudhuria kikao cha mahakama maalum kwa Lebanon, chenye makao yake viungani mwa The Hague, umamuzi huo unapotolewa Jumanne.

Hadi kufikia sasa hakuna taarifa zozote kuhusu walipo washukiwa hao Salim Jamil Ayyash, Hassan Habib Merhi, Hussein Hassan Oneissi and Assad Hassan Sabra

Hakuna kati yao aliyesema chochote wakati wa kesi inaendelea. Lakini mahakama iliteua wakili atakayewawakilisha aliyetupilia mbali taarifa za mwendesha mashtaka akidai kwamba ziliegemea ushahidi wa kawaida tu uliokosa uthabiti na kushindwa kuthibitisha kwamba bila shaka yoyote watuhumiwa walikuwa na makosa.

Kesi hiyo inahusu nini?

Asubuhi ya 14 Februari 2005, Rafik Hariri - wakati huo mbunge ambaye alijihusisha na upinzani bungeni - alikuwa kwenye msafara wake uliokuwa unapita hoteli ya St. George mjini Beirut na bomu lililokuwa limefichwa ndani ya gari likalipuka.

Mlipuko huo ulisababisha shimo kubwa barabarani huku magari na maduka yaliokuwa karibu yakiwaka moto na kugeuka meusi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hariri alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa Sunni maarufu na wakati wa kifo chake alikuwa ameunga mkono wito wa Syria kuondoa majeshi yake nchini humo, ambayo yalikuwa Lebanon tangu mwaka wa 1976 kufuatia kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mauaji hayo yalisababisha maelfu ya watu kuandamana wakipinga serikali inayounga mkono Syria, huku kidole cha lawama kwa mauaji ya Hariri kikielekezwa kwa nchi hiyo jirani ya Lebanon iliyokuwa na ushawishi mkubwa.

Serikali ilijiuzulu wiki mbili baadae na Syria ikaondoa wanajeshi wake Aprili.

Baada ya ushahidi kukusanywa, Umoja wa Mataifa na serikali ya Lebanon mahakama maalum kwa ajili ya Lebanon 2007 kuchunguza shambulio hilo la bomu na washukiwa wanne hatimae wakafunguliwa mashtaka bila ya kuwepo mahakamani kwa makosa yaliyojumuisha njama ya kutekeleza vitendo vya ugaidi.

Mshukiwa wa tano, kamanda wa jeshi la Hezbollah Mustafa Amine Badreddine, aliondolewa kwenye orodha ya washukiwa baada ya kuuawa nchini Syria 2016.

Wafuasi wa kundi la Hezbollah wametupilia mbali kesi hiyo wakisema kwamba mchakato wa mahakama maalum hauzingatii haki.

Kwanini kesi hii ni muhimu?

Kushtakiwa kwa wanaume wote hao wanne bila ya kuwepo mahakamani kumeweka historia ya kupatikana kwa haki kimataifa na nchini Lebanon vilevile.

Mahakama hiyo ilionesha nia ya kuwawajibisha watendaji wa uhalifu katika nchi ambayo usaidizi na ulinzi unaweza kuwakinga wasishtakiwe.

Chanzo cha picha, Reuters

Hata hivyo, kumekuwa na mgawanyiko mkubwa kati ya wanaotaka uwepo wa mahakama hiyo maalum na wale waliohisi kwamba hizo ni propaganda za kisiasa tu.

Aidha kundi la Hezbolla liliapa kutowakabidhi watu hao wanne iwapo watapatikana na makosa na kushtakiwa.

Kundi hilo lina jeshi lenye nguvu nchini humo pamoja na jeshi la Lebanon na lina ushawishi mkubwa kwa wanaoendesha serikali.

Pia, mwisho wa kesi hiyo unawadia wakati nchi ya Lebanon ipo kwenye mgogoro mkubwa.

Bado inakabiliana na mkasa mkubwa wa bomu uliolipua bandari ya Beirut uliotokea Agosti 4, ambapo zaidi ya 180 waliuawa huku wengine zaidi ya 6,000 wakipata majeraha.

Hata kabla ya hapo, Lebanon ilikuwa kwenye mgogoro mkubwa wa kiuchumi huku sarafu yake ikididimia, bei za bidhaa zikiongezeka na idadi ya wasio na ajira ikizidi kuongezeka na kusababisha maandamano.

Haijalishi ni uamuzi gani utakaotolewa, bila shaka kuna uwezekano mkubwa wa kuzuka kwa wasiwasi upya.