Viongozi wa mataifa jirani waahidi kusaidia Msumbiji katika mkutano wa SADC

Wakazi wanaoishi karibu na bandari ya Mocímboa da Praia wanaendelea kukimbia makazi yao

Chanzo cha picha, EPA

Mapigano yanaendelea nchini Msumbuji huku majirani wa nchi hiyo wakiahidi kutoa msaada kujinasua ya hali hiyo.

Wakazi wanaoishi karibu na bandari ya Mocímboa da Praia wanaendelea kukimbia makazi yao huku mapigano yakiendelea kati ya wanajeshi wa serikali ya Msumbiji na wanamgambo wa Kiislamu.

Eneo lililovamiwa liko karibu na miradi ya utafutaji wa gesi asili yenye thamani ya dola bilioni 60 na ulilengwa mara kadhaa na wanamgambo mwaka huu, kabla ya Msumbiji kutwaa tena bandari hiyo wiki iliyopita.

Baadae jeshi la Msumbiji lilisisitiza kwamba limechukua udhibiti wa bandari na Rais Filipo Nyusi alizuru eneo la Cabo Delgado ambalo limekuwa likilengwa na wanamgambo tangu mwaka 2017.

Laini za simu kwa ajili ya mawasiliano bado zimekatwa na miundo mbinu imeharibiwa.

Rais Nyusi alisema nini?

Alisema wapiganaji ambao wanahusishwa na kundi la kigaidi la Islamic State 'IS' hawajatoa tishio lolote dhidi ya jitihada za kimataifa kuharibu gesi iliyohifadhiwa.

Ingawa waasi hao wanaonekana kuingia nchini humo kwa kasi na kufanya usalama wa taifa la Msumbiji kuwa mashakani.

Taarifa kuhusu kile kinachoendela Mocimboa da Praia ni vigumu kubaini kwani barabara, umeme na mitambo ya simu imekatwa.

Kuna ushahidi unaodai kuwa waasi hao wana silaha za uhakika na wana nia madhubuti kufanikisha lengo lao.

Wanamgambo wanaofahamika kama al-Shabab, au vijana - ambao wana ajenda ya kiislamu, lakini kwa miongo wamejengwa na ukosefu wa miundo mbinu, ukosefu wa ajira, uchaguzi usio wa haki, rushwa na migogoro.

Siku ya Jumatano juma lililopita Msumbiji ilisema kuwa vikosi vyake vinapigana kuchukua udhibiti wa bandari hiyo baada ya taarifa kadhaa kudai kwamba imetekwa na wanamgambo wa Islamic State Jumatano.

Jeshi limesema kuwa hatua imechukuliwa kukabiliana na kundi hilo ambalo limekuwa likitumia wenyeji kama ngao yao.

Hatua hiyo inafuatia mapigano ya siku kadhaa ya kutaka kuchukua bandari hiyo yenye utajiri wa gesi eneo la kaskazini.

Hatua hiyo imekuja huku viongozi wa mataifa jirani wakithibitisha kujitolea kwao kusaidia Msumbiji kukabiliana na tatizo la ugaidi na mashambulizi yanayotokea nchini humo," wakati wa mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Mwandishi wa BBC Africa Andrew Harding alisema kuwa kutekwa kwa bandari hiyo ni pigo kubwa kwa jeshi la Msumbiji, ambalo lina wakati mgumu kudhibiti ukuaji wa makundi ya waasi katika eneo hilo la utajiri wa mafuta la Cabo Delgado.

Bandari ya Mocimboa da Praia inatumiwa kwa uwasilishaji wa mizigo kwa miradi ya eneo la pwani takribani umbali wa kilomita 60 (maili 40), ambayo inaendelezwa na kampuni kubwa za mafuta duniani ikiwemo Total.

Wanamgambo - wenye kuhusishwa na kundi la Islamic State - wamekuwa wakitwaa miji kadhaa ya kaskazini katika miezi ya hivi karibuni, na kulazimisha maelfu ya watu kutoroka makazi yao.

Hili lilikuwa moja ya mashambulizi kadhaa katika bandari ya Mocimboa da Praia mwaka huu.

Tanzania pia imesema itafanya mashambulio dhidi ya wanamgambo wa jihadi katika misitu karibu na mpaka na Msumbiji.