Marekani na Sudan zazungumza kuhusu kuondolewa kwenye orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi

Mike Pompeo w=with Sudan's PM

Chanzo cha picha, Sudan government

Maelezo ya picha,

Hii ni ziara ya kwanza kwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani kwenda Sudan kwa miaka 15

Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok amesema amefanya mazungumzo na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo kuhusu tukio la kuorodheshwa kuwa mfadhili wa ugaidi.

Sudan inataka kuondolewa kwenye orodha hiyo ili vikwazo dhidi yake viondolewe.

Nchi hiyo ilikuwa kwenye orodha tangu miaka ya 1990 wakati kiongozi wa kundi la wanamgambo wa al-Qaeda Osama Bin Laden alipokuwa anaishi nchini humo, kama mgeni wa serikali ya aliyekuwa rais wa Sudan Omar al Bashir.

Bashir aling'atuliwa mamlakani na tangu wakati huo uhusiano na Marekani ulianza kuimarika.

Sudan iko kwenye orodha hiyo sambamba na Korea Kaskazini, Iran na Syria.

Viongozi wa nchi hiyo wako na shauku kubwa kuondokana na vikwazo vya kiuchumi na kupata fursa ya kuwa kwenye mfumo wa dola kimataifa ili kuvutia mikopo na uwekezaji.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mike Pompeo amekuwa akihamasisha uhusiano mzuri kati ya Israel na mataifa ya Kiarabu

Moja kati ya masharti yaliyowekwa na Marekani kwa Sudan ili kuondolewa kwenye orodha hiyo ni kuwalipa fidia wanafamilia wavuvi 17 wa Kimarekani waliokufa kwenye meli yao ambayo ilipigwa bomu na kundi la al-Qaeda katika bandari nchini Yemen mwaka 2000.

Sudan ilikubali sharti hilo mwezi Februari.

'Matumaini ya kurudi kwa mahusiano ya Israel na nchi za kiarabu'

Awali, Bwana Pompeo alisema alikuwa safarini kwa ndege ya moja kwa moja akitokea Tel Aviv kwenda Khartoum, safari inayoelezwa kuwa ya 'kihistoria' na ubalozi wa Marekani mjini Yerusalemu.

Anakuza mahusiano ya karibu kati ya Israel na nchi za kiarabu katika ziara yake Israel, Sudan, Bahrain na Umoja wa falme za kiarabu.

Katika ziara yake huko Israel, ametaka nchi za kiarabu kufikia makubaliano ya amani na Israel.

Pompeo alikuwa akilenga makubaliano kati ya umoja wa falme za kiarabu na Israel, ambayo mpatanishi wake ni Rais wa Marekani, Donald Trump, mwanzoni mwa mwezi huu.

Tuna ''matumaini sana kuwa tutaona mataifa mengine ya kiarabu yakiunga mkono hili'', alisema.

Lakini serikali ya mpito ya sasa ya Sudan ''haina mamlaka kuamua kuweka mambo sawa na Israel'', Msemaji Faisal Saleh alinukuliwa na Shirika la habari la AFP.

Je hiki ni kipindi kipya kati ya Israel na nchi za kiarabu?

Makubaliano ya hivi karibuni ni makubaliano ya tatu ya amani kati ya Israel na nchi ya kiarabu.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema makubaliano yanaleta matumaini mema siku za usoni.

Maafisa wa Israel na Marekani wanaamini Bahrain, Oman na Sudan zitafuata.

Mwezi Februari, Bwana Netanyahu alikutana na kiongozi wa Baraza la Sudan Abdel Fattah al-Burhan nchini Uganda, ambapo Israel ilisema nchi hizo mbili zilikubaliana kuanzisha uhusiano mwema.

Hatahivyo, Wizara ya mambo ya nje ya Sudan ilimfuta kazi msemaji wake juma lililopita baada ya kusifu makubaliano ya amani kati ya Sudan na umoja wa falme za kiarabu kuwa ''ni hatua nzuri na ya werevu.''