Waridi wa BBC: Mume wangu alikuwa akija nyumbani kulala na wapenzi wake wa nje
- Anne Ngugi
- BBC Swahili

Chanzo cha picha, Narumbe Ekiru
Narumbe Ekiru akitabasamu
Narumbe Ekiru hupenda kutabasamu sana. Ukikutana naye utadhani ni mtu mwenye furaha tele maishani. lakini hali ni tofauti.
Kutabasamu kwake huficha ukweli wa mambo yaliyomo ndani ya moyo wake.
Chanzo chake hasa ni mahangaiko na masikitiko aliyoyapitia katika maisha yake ya ndoa.
Mwanadada huyu mwenye miaka 35 sasa, anapozungumzia ndoa yake ya miaka 11, anaifananisha na matukio kwenye sinema ila yalitendeka.
Usiku wa kuogofya
Mwanamke huyu anasema moja ya siku ambazo hatawahi kuzisahau maishani ni wakati ambapo bila yeye kutarajia, mumewe alirejea nyumbani jioni akiwa ameandamana na mwanamke aliyekuwa mpenzi wake.

Chanzo cha picha, Narumbe Ekiru:
"Nilishtuka mume wangu aliponieleza kuwa nitafute kwa kulala ili mradi apate kufurahia usiku na mpenzi wake
Alimweleza kuwa usiku huo alikuwa na mgeni mpenzi wake ambaye lazima angelala naye usiku huo.
"Nilishtuka mume wangu aliponieleza kuwa nitafute kwa kulala ili mradi apate kufurahia usiku na mpenzi wake. Mume wangu alinieleza kuwa niamue kama ningelala kwenye kochi au nitafute jirani au rafiki yangu. Lakini usiku huo ulikuwa wake na mpenzi wake, " Narumbe anakumbuka
Narumbe anasema kuwa matukio ya usiku huo yalimchanganya mno .
Alijikuta tu anaitikia lolote ambalo mume wake alikuwa anamweleza. Alishindwa kusema chochote wala kuchukua hatua zozote za kutetea ndoa yake.
Aliamua kuondoka na kumuacha mume wake, baba ya watoto wake na mpenzi wake, kulala na mwanamke huyo usiku huo.
Je Narumbe alikwenda wapi ?
Alipotoka nje na kumuacha mume wake na mpenzi wake, alikuwa hajui iwapo abishie majirani milango, au alale tu nje ya nyumba yake .
"Kulikuwa na giza nje, lakini giza kubwa lilikuwa katika moyo wangu nisijue la kufanya. Hapo hapo nilikumbuka kuhusu rafiki yangu wa karibu ambaye hakuwa anaishi mbali na kwangu. Ni yeye aliyenipokea na kunipa pa kulala usiku huo, " Narumbe anakumbuka.
Usiku wenyewe Narumbe anasema kuwa ulikuwa mrefu zaidi. Hakuweza kufunga macho hata tone la usingizi halikumjia.
Akilini mwake alikuwa anacheza picha za mume wake akiwa na mpenzi wake na jinsi walivyokuwa wanaburudika. Mwanadada huyu anasema kuwa usiku huo ulikuwa umejaa kiza kikuu na alijikakamua tu kuishi.
Alfajiri na mapema, Narumbe anasema kuwa mumewe alimpigia simu na kumweleza arejee nyumbani kwani yeye na mgeni wake walikuwa wamemalizana.

Chanzo cha picha, Narumbe Ekiru
Alfajiri na mapema, Narumbe anasema kuwa mumewe alimpigia simu na kumweleza arejee nyumbani kwani yeye na mgeni wake walikuwa wamemalizana.
Amini usiamini Narumbe alijikokota hadi kwake nyumbani. Mwanadada huyu anasema kuwa akilini mwake alikuwa anataka ndoa yake inawiri na angefanya lolote kuiokoa .
Aliingiaje kwenye ndoa?
Narumbe Ekiru alingia kwenye maisha ya ndoa akiwa na umri wa miaka 19. Alijitosa kwenye ndoa na shauku ya kutamani iwe nambari moja kwa hali na mali. Mwanamke huyu alifahamu tangu akiwa binti kuwa mwanamke mzuri ni yule ambaye huvumilia, na hutafuta kila mbinu kuishi na mume wake bila ugomvi.
"Miaka ya kwanza ya ndoa yangu tulianza na ufukara mkubwa kiasi kuwa tulianza kuishi nyumba ya rafiki wa karibu wa mume wangu. Kusema ukweli mume wangu hakuwa na chochote hata kijiko kwahivyo tulianza maisha ya chini mno na tukaanza kupanda polepole," Narumbe anakumbuka.
Kando na hayo ni kuwa mwanadada huyu alisumbuka kushika mimba.
Kwa mara tatu mimba alizokuwa nazo zilitoka. Aliposhika mimba kwa mara ya nne ndipo alipojaaliwa mtoto wao wa kwanza mwaka wa 2007, na baada ya hapo alijaliwa watoto wengine wavulana mwaka wa 2009 na mwaka wa 2012 mtawalia .
Mwanadada huyu anasema kuwa hata kipindi ambacho mume wake alipopatwa na ugonjwa alisimama naye.

Chanzo cha picha, Narumbe
Mwanadada huyu anasema kuwa hata kipindi ambacho mume wake alipopatwa na ugonjwa alisimama naye.
Katika hali hio iliwabidi wahame na kuanza maisha mapya kijijini kwa kukosa namna ya kuishi mijini.
Baada ya miaka miwili ya kuishi kijijini na mume wake kupata nafuu walihama tena.
Lakini maisha yalibadilika hususan tabia na mienendo ya mume wake waliporejea tena mjini na kuanza maisha yaliokuwa angalau na ustarehe.
Visa vya michepuko
Waliporejerea maisha ya mjini, biashara ya mume wake ilianza kunawiri, na kwa hivyo maisha ya ufukara waliyaaga kwaheri. Narumbe anasema kuwa mumewe naye alibadilikia wakati huo.
Akiwa na ujauzito wa mtoto wa pili , anakumbuka kuwa mume wake alirejea nyumbani na mwanamke mwengine aliyekuwa na mtoto mdogo.
Narumbe anasema kuwa mumewe alimweleza kuwa amemletea msaidizi kwani kama mjamzito alihitaji usaidizi wa hapa na pale nyumbani.
Ila alichokuja kugundua baadaye ni kuwa mwanamke aliyeletwa nyumbani kwake kama kijakazi, alikuwa ni mpenzi wa kando wa mume wake.
Kulingana na Narumbe, mpenzi wa mumewe baadaye alishika mimba akiwa pale pale nyumbani kwao.

Chanzo cha picha, Narumbe Ekiru
Narumbe anasema kuwa waliendelea na uhusiano wa kimapenzi na mumewe. Alipangishiwa nyumba kwengine na wakaendelea na uhusiano huo
Vuta nikuvute ilipojiri ilibidi mpenzi wa mumewe aondoke
Narumbe anasema kuwa waliendelea na uhusiano wa kimapenzi na mumewe. Alipangishiwa nyumba kwengine na wakaendelea na uhusiano huo .
Baada ya hapo kila baada ya muda Narumbe anadai kuwa mume wake alikuwa anaingia kwenye mahusiano ya mapenzi na wanawake tofauti.
Kilichokuwa kinamkera sana ni kwamba mume wake alikuwa anamueleza kuhusiana na visa na vituko vyake na wale wapenzi wake .
"Katika muda niliokuwa kwenye ndoa yangu , mume wangu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanawake tisa. Wote hao alikuwa ananieleza jinsi walivyo na kila kitu kuhusu maisha yao. Hali hiyo ilikuwa inanipa uchungu na kero nyingi , ila kila wakati nilidhani kuwa mume wangu angebadilika na kurudi kwangu kama mke wake , ila haikuwa hivyo," Narumbe anakumbuka
Wakati mmoja alitoroka ndoa yake kwa kushindwa kuhimili 'kuchovyachovya' kwa mume wake.
Licha ya kuwa mbali naye, alikuwa anahisi kuwa mke mwema ni yule ambaye huvumilia matukio na changamoto za ndoa , ila wakati aliotoroka alihisi kana kwamba hangeweza kuhimili machungu ya mume anayeruka kutoka kwa mpenzi mmoja hadi mwengine.
Kifo cha mumewe na wanawe wawili
Vifo vya watu hawa muhimu katika maisha ya mwanamke huyu vilifanyika miaka tofauti na katika mazingira tofauti kama alivyoelezea.
Mwana wake wa tatu ndiye aliyefariki kwanza mwaka wa 2013 akiwa na siku saba baada ya kuzaliwa. Hii ni baada ya kuugua kwa muda mfupi .
Mvulana wake wa kwanza akiwa na miaka 9 alianza kuugua, Kifua kikuu (TB) ugonjwa ambao ulimdhoofisha sana.
Kando na hayo Narumbe anasema kuwa Macho na masikio ya mwana wake yalikuwa yanamsumbua sana na kwa miaka miwili, mtoto huyo aling'ang'ana na usumbufu wa mwili wake. Alizidiwa na kufariki mwezi Mei mwaka wa 2016.
"Wakati huu wote nilikuwa najiuliza ni kwanini watoto wangu wameanza kufariki. Vile vile nilikumbuka ugumu na mahangaiko ya kushika mimba. Baada ya kupoteza mimba tatu kutoka kabla ya kujifungua. Nilijwa na maswali mengi na sikuwa na wakunijibu," anakumbuka Narumbe
Narumbe alikuwa amesalia na mvulana wake mmoja tu na mume wake naye alikuwa tayari amemuoa mwanamke mwengine baada ya Narumbe kuacha ndoa ile.
Kifo cha mume wake kilitokea wakati ambapo Narumbe anasema alikuwa amejitenga kwa maombi . Narumbe anasema kuwa mumewe aliaga mwaka wa 2017 mwezi sawia na wakati ambapo mwana wao wa kwanza alifariki . Kulingana na alivyoelezwa ni kuwa mumewe alipatwa na mshtuko wa moyo alipokuwa kwenye bodaboda, na juhudi zake kupelekwa hospitalini hazikufua dadu kwani alifariki kabla ya kupewa matibabu yoyote.
Kuwapata watoto wengine

Chanzo cha picha, NARUMBE
Kwa sasa Ekiru Narumbe amejikakamua kuwa mama mlezi wa watoto zaidi ya 40.
Kwa sasa Ekiru Narumbe amejikakamua kuwa mama mlezi wa watoto zaidi ya 40.
Hawa anawapa malezi katika makao ya watoto. Mwanzoni makao haya yalikuwa yameanzishwa na aliyekuwa mume wake ambaye ni marehemu lakini baada ya kifo chake aliamua kuendeleza kazi ya kuwapa malezi na upendo watoto wanaohitaji usaidizi .
Kando na kuwa ana jukumu la kumpa malezi na upendo mtoto wake wa kipekee aliyesalia hai.
Narumbe ni mtoa nasaha ambaye ; yeye kama mama aliyepitia uchungu wa kufiwa na watu aliowapenda na vilevile kufa kwa ndoa yake anafahamu misukosuko ya maisha jinsi hutokea katika maisha ya mtu.