Uchaguzi Tanzania 2020; Tutarajie nini katika kampeni za uchaguzi ujao?

  • Marcus Mpangala
  • Mchambuzi
Huu ni uchaguzi wa sita tangu nchi hiyo iliporejea kwenye mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1992

Kiu ya raia wa Tanzania kushiriki kampeni za uchaguzi mkuu wa urais,ubunge, udiwani inatarajiwa kukatwa ifikapo Agosti 26 mwaka huu wa 2020 ambapo uzinduzi utafanyika kwa vyama mbalimbali na kudumu kwa takribani siku 60 huku dalili zinaonesha kutakuwa na ushindani mkali katika nafasi ya urais ambapo jumla vyama vya siasa 16 vimeweka wagombea wao kufikia sasa

Duru za kisiasa zinaonesha kuwa ushindani mkali utakuwa katika kampeni wagombea watatu ikiwa watateuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Agosti 25; John Magufuli (CCM), Tundu Lissu (Chadema) na Bernard Membe (ACT Wazalendo) kwa upande wa Jamhuri, huku Maalim Seif (ACT Wazalendo) na Dkt. Hussein Mwinyi (CCM) wakitoana jasho upande wa Zanzibar.

Mabadiliko ya upashanaji habari na matumizi makubwa ya mitandao, ukosefu wa ajira, ghadhabu za kunyimwa fursa ya mikutano ya hadhara, hali ya uchumi, haki za binadamu, miradi mikubwa ya maendeleo, uhuru wa tume ya uchaguzi, kuibuka hamasa ya kisiasa miongoni mwa wananchi pamoja na ajenda ya usalama wa raia na viongozi wao ni baadhi ya mambo yanayotarajiwa kutawala sehemu kubwa ya kampeni za uchaguzi huo.

Kampeni hizo zitafika tamati tarehe ya uchaguzi mkuu Oktoba 28 ambapo mamilioni ya Watanzania watapiga kura kuchagua viongozi wapya watakaopokea kijiti cha uongozi cha miaka mitano ijayo. Huu ni uchaguzi wa sita tangu nchi hiyo iliporejea kwenye mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1992.

Ni kampeni kwa wapiga kura vijana

"Hakika huu ni uchaguzi wa vijana. Vyama vyote na wagombea wao wakiweza kuwashawishi vijana wana nafasi kubwa zaidi ya kushinda. Kundi la wapigakura wapya zaidi ya milioni 7 ni kubwa mno. Mbinu zitategemea matamanio ya kundi hili. Hapa maana yake iwapo wamejiandikisha kupiga kura wengi wao walizaliwa miaka 1990. Kundi jingine la waliozaliwa mwanzoni mwa miaka 2000. Hayo ni mabadiliko, ni sura mpya ya wapigakura, kampeni zinagusa hao wenye uchaguzi wa mwaka huu," anasema Francis Daudi, mhadhiri wa historia wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino tawi la Tabora na mchambuzi wa siasa na utawala bora.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mkutano wa 19 wa Bunge jijini Dodoma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema idadi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura imeongezeka ambapo wapigakura halali ni 29,804,992 ikilinganishwa na 23,161,440 kwa mwaka 2015.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Semistodes Kaijage wakati wa ufunguzi wa ratiba ya uchaguzi, alisema takwimu za awamu ya kwanza na pili zinaonesha kuwa wapigakura wapya walioandikishwa ni 7,326,552, walioboresha taarifa zao ni 3,548,846 na 30,487 wamepoteza sifa.

Kumbukumbu za mwaka 2015 zinaonesha wapigakura wanawake ni asilimia 53, wanaume walikuwa asilimia 47. Wapigakura vijana waliokuwa na umri kati ya miaka 18 na 35 walikuwa asilimia 57 ya wapigakura wote. Wapigakura waliokuwa na umri zaidi ya miaka 50 walikuwa asilimia 18 huku wengine asilimia 25 wakiwa na umri kati ya 36 na 50. Hata hivyo waliopiga kura mwaka 2015 ni watu 15,589,639 sawa na asilimia 67.31.

Vyama kunyukana mitandaoni

Eneo hili linahusisha mabadiliko ya upashanaji habari kati ya vyama vya siasa na wagombea wao kwa upande mmoja na wanachama na wapigakura kwa upande mwingine. Kufungiwa baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikitoa fursa kwa upinzani kuwasiliana na wafuasi wao, kumetengeneza 'vita' mpya ya matumizi ya mitandao ya kijamii kama nyenzo ya kampeni katika uchaguzi ujao.

"Bila shaka tutakuwa na kampeni za mitandaoni. Wagombea wa upinzani wanaamini vyombo vya habari havitatoa habari zao kwa ukamilifu iwe redio au Televisheni. CCM inaamini haijawekeza vema mtandaoni. Naona pia nafasi ya udukuzi ikiwa kubwa katika kampeni za uchaguzi wa mwaka huu. Naona zitakuwa kampeni za swali na jibu. Wanasiasa watajikita katika kurusha vijembe na kujibu. Upinzani badala ya kueleza sera zao wataeleza walivyoteseka miaka mitano, na CCM badala ya kusema watafanya nini wataeleza walivyofanya," ameongeza Francis Daudi.

Katika hatua za awali vyama vya ACT, Chadema na sasa NCCR Mageuzi ni vinara wa kutoa hotuba zao kupitia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, YouTube na Instagram. Viongozi Zitto Kabwe, Tundu Lissu, Maalim Seif, na Katibu wa Uenezi CCM, Humphrey Polepole wamekuwa wakitoa hotuba humo.

Nyenzo hiyo inatarajiwa kutikisa zaidi katika uchaguzi huu kutokana na imani kuwa uhuru wa vyombo vya habari kuhabarisha kwa usawa umepungua kwa kiasi kikubwa. Baadhi vimetozwa faini na Mamlaka zinazohusika kutokana na kile kilichoitwa kutangaza na kuonesha mahojiano ya upande wa kiongozi wa upinzani pasipo upande wa serikali kupatiwa fursa ya kutoa ufafanuzi.

Katika hatua nyingine baadhi ya vyama vilianzisha utaratibu wa kusajili wanachama wao kwa njia ya mtandao. Mwanachama amepewa fursa ya kujisajili mwenyewe na kupunguza usumbufu kwa kwenda kwenye tawi la chama au kupishana muda wa kazi na mwandikishaji wa wanachama, mathalani wa Chadema na CCM.

Aidha, usajili huo kwa njia ya Simujanja (Smartphone) unasaidia kumwezesha mwanachama kupata taarifa za chama kupitia simu yake ya mkononi.

Kwahiyo kampeni za mwaka huu zinaweza kufanyika kwa kuwasiliana na wanachama wa chama moja kwa moja kupitia simu zao. Badala ya kutegemea magari ya matangazo kupita mitaani kuwatangazia wanachama kuhusu mkutano wa chama husika. Hii ni njia ya kufanya kampeni kumweka mwanachama karibu na mapambano kwa njia ya faida ya teknolojia, pamoja na kupunguza utegemezi kwenye vyombo vingine vya upashaji habari.

'Jela za kisiasa'

Kabla na wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wanasiasa wa vyama mbalimbali walikuwa na uhuru wa kutosha wa kufanya shughuli za siasa kuanzia majimboni hadi kitaifa. Vyama vyote vya siasa vilikuwa na uwanja sawa na CCM. Tofauti ni mwaka huu vyama vya siasa vinashiriki baada ya kutoka katika kile kinachoitwa 'jela ya kisiasa' kutokana na kuzuiwa mikutano ya hadhara ya kitaifa.

Wabunge wa kuchaguliwa waliruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara katika majimbo yao pekee, huku siasa za kitaifa zikipigwa kufuli kwa kipindi cha miaka mitano. Wanasiasa wanaingia katika uchaguzi huu wakiwa wametoka kwenye mazingira yaliyowabana na sasa wanapata nafasi ya kupumua.

Upinzani kugawana kura

Maelezo ya picha,

Wanachama wakuu wa ACT Wazalendo Tanzania

Vyama vya upinzani vinaweza kuingia katika kampeni kila kimoja kikifanya mambo yake. Mwaka 2015 palikuwa na muungano wa vyama vya upinzani kupitia mwamvuli wa UKAWA (Umoja wa Katiba ya Wananchi) ambapo ulikuwa na mshikamano zaidi kuliko wa mwaka 2020. Muungano huo ulihusisha vyama vikubwa na vidogo ambapo ushirikiano wao uliwaletea zaidi ya wabunge 100.

Uchaguzi wa mwaka 2020 mambo yanaelekea kuwa tofauti na 2015 ambapo kulikuwa na mgombea mmoja mwenye nguvu kwa upande wa upinzani Bwana Edward Lowassa ambaye alikuwa akiungwa mkono na Ukawa dhidi ya John Magufuli wa CCM. Mwaka huu licha ya kuwa na zaidi ya vyama 15 vinavyotaka kumng'oa madarakani Magufuli, upinzani mkali utakuwa unatoka kwa Tundu Lissu (Chadema) na Bernard Membe (ACT Wazalendo).Kushindwa kwa vyama hivyo kukubaliana kutoa mgombea mmoja kutamaanisha kuwa kura za wafuasi wa upinzani zitagawanyika.

Kwa upande wa Zanzibar mgombea wa upinzani ambaye atampatia wakati mgumu Dkt Hussein Mwinyi wa CCM bado ni Maalim Seif (ACT Wazalendo) ambaye anarejea ulingoni kwa mara ya sita, ikiwa ni mara ya kwanza nje ya chama cha CUF ambacho alibidi akihame kutokana na miggoro ya ndani.

Ukimya wa utafiti wa kura za maoni

Mwaka 2020 Tanzania kampeni za uchaguzi zinawadia pasipo utafiti wowote tofauti na ule wa mwaka 2015. Mathalani utafiti unaofanywa na taasisi kama Twaweza au IPSOS, kuelekea uchaguzi huu hakuna taasisi iliyojishughulisha na utafiti wa kisiasa kupima kukubalika kwa wagombea.

Mwaka 2015 UVCCM walifanya utafiti ulionesha mgombea wa CCM John Magufuli angeshinda kwa asilimia 85. Nao utafiti wa timu ya kampeni ya CCM uliosomwa na Januari Makamba ulionesha kuwa Magufuli ageshinda kwa asilimia 69.

Utafiti wa asasi ya Twaweza nao ulisema mwaka huo Magufuli angeshinda kwa asilimia 65. Taasisi ya IPSOS ilisema Ukawa wangepata asilimia 31 katika uchaguzi huo. Mwaka 2018 Twaweza walitoa utafiti wa kushuka umaarufu wa RaisMagufuli ambapo alifikia asilimia 56.

Hata hivyo kampeni za mwaka huu zinaelekea kuanza pasipo kuona utafiti wa kura za maoni kukubalika vyama vya siasa, wagombea na wapigakura wao. Duru za kisiasa zinasema taasisi nyingi za utafiti ni kama vile zimegoma kufanya kazi hiyo licha ya kulindwa na Katiba ya Tanzania Ibara ya 18 (1 na 2) inatoa haki ya kikundi cha watu au taasisi yoyote kukusanya na kutoa habari bila kuvunja sheria. Aidha, sheria inayoagiza taasisi au mtu binafsi akitaka kufanya utafiti aombe kibali kwa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ni kikwazo.

CCM na kampeni inayojitegemea

Maelezo ya picha,

kongamano la wanachama wa CCM

Uchaguzi wa mwaka 2015 CCM ilinufaika na mgogoro uliokuwepo Chadema na Ukawa. Dk. Wilbroad Slaa alijiuzulu nafasi ya Ukatibu Mkuu Chadema. Naye mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Prof Lipumba alijizulu wadhifa huo. Matukio yote mawili yalisababisha mgogoro ndani ya muungano wa Ukawa.

CCM mwaka huu wataingia katika kampeni bila kutegemea mgogoro wa upinzani. Ukweli mmoja ni kwamba CCM wanajivunia serikali waliyounda ambayo imejikita katika kuanzisha na kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwamba miradi hiyo inajinadi na kuwapa imani kuwa watapata kura nyingi katika uchaguzi huu.

Ni maeneo gani yatasikika katika kampeni?

Usalama wa raia na viongozi wao, uhaba wa ajira, hali ya uchumi,mazingira ya biashara ni miongoni mwa mambo ambayo yatagusiwa katika kampeni za uchaguzi. Yote yatagusa jamii na kubadili mtazamo ni wagombea gani wanastahili kupatiwa kura zao.

Lakini pia kuna majimbo ambayo upinzani ilichaguliwa mwaka 2015 na mwaka huu mchuano mkali unatarajiwa kutokea kwenye majimbo hayo. Matahalani majimbo sita kati ya 10 ya jiji la Dar es salaam yalichukuliwa na wabunge kutoka upinzani. Nje ya Dar es Salaam majimbo kadhaa kama Iringa Mjini, Tanga Mjini, Arusha Mjini, Mbeya Mjini, Kigoma-Ujiji na Tarime (Mjini na Vijini) yanatarajiwa kushuhudia upinzani mkali zaidi.