Jacob Blake: Watu wawili wapigwa risasi katika usiku wa maandamano Wisconsin Marekani

Protesters hold up make-shift shields during unrest in Kenosha

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Kenosha jimbo la Wisconsin ambalo limeshuhudia siku tatu za maandamano usiku

Watu wawili wameuawa na mmoja kujeruhiwa wakati wa maandamano ya usiku wa tatu katika mji wa Kenosha huko Marekani ambako chimbuko lake ni mtu mweusi kupigwa risasi na polisi.

Polisi imesema kwamba watu watatu wamepigwa risasi lakini haikutoa taarifa zozote kuhusu waathirika.

Ripoti kutoka vyombo vya habari awali vilisema kwamba vinaamini mashambulizi hayo yametokana na makabiliano kati ya waandamanaji na wanaume waliokuwa na silaha ambao waliokuwa wanalinda kituo cha mafuta cha petroli.

Maandamano yalizuka baada ya Jacob Blake kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya na polisi Jumapili.

Picha za video zimeonesha mwanaume huyo, 29, akipigwa risasi mara kadhaa wakati akiinama kuingia ndani ya gari. Mawakili wake wanasema itahitajika miujiza kutokea ili aweze kutembea tena.

Chanzo cha picha, Reuters

Katika taarifa yao, Polisi ya Kenosha ilijibu taarifa za risasi kufyatuliwa na watu kupigwa risasi mara kadhaa katika mji huo takriban saa 23:45 Jumanne.

"Ufyatuaji huo wa risasi ulisababisha vifo vya watu wawili na mwathirika wa tatu aliyepigwa risasi alisafirishwa hadi hospitali akiwa na majeraha mabaya lakini sio ya kuhatarisha maisha yake," taarifa hiyo imesema.

Iliongeza kwamba jitihada za kutambua walioathirika bado zinaendelea na hakuna taarifa zaidi zilizotolewa wakati huo. Uchunguzi umeanzishwa.

Awali, afisa wa Kaunti ya Kenosha Sheriff David Beth aliliambia gazeti la New York Times kwamba uchunguzi wa mauaji hayo utaangazia kundi la wanaume waliokuwa na silaha nje ya kituo cha petroli.

Maelezo ya picha,

Ofisi za kuchunguza tabia za wakosaji idara ya urekebishaji tabia zilivyoharibiwa

Picha za kwenye video zinaonesha mwanaume mwenye bunduki akifukuzwa na kundi la watu kabla ya kuanguka na anaonekana akifyatua risasi mara kadhaa.

Video nyingine inaonesha raia waliojihami kwa silaha wengi wakiwa wamevaa nguo za kijeshi, wakikusanyika nje ya biashara zao waliosema kwamba wanalinda.

Video pia inaonesha watu wakikimbia huku risasi zikifyatuliwa na wengine wakijeruhiwa.

Maandamano ya awali yamesababisha uharibifu katika ofisi za serikali na biashara binafsi na pia kumekuwa na taarifa za makundi ya watu yakijitokeza kulinda mali.

Gavana wa Wisconsin Tony Evers alisema Jumanne kuwa anatuma vikosi zaidi vya usalama mjini humo wakati maandamano yanaendelea kupamba moto.

Chanzo cha picha, BENCRUMP.COM

Maelezo ya picha,

Jacob Blake alipigwa risasi mara saba mgongoni

Mawakili wa familia ya mtu mweusi aliyepigwa risasi na polisi katika jimbo la Wisconsin nchini Marekani wanasema anahitaji "miujiza" kutembea tena.

Jacob Blake, 29, alipigwa risasi mara kadhaa akifungua mlango wa gari mjini Kenosha.

Moja ya risasi alizopigwa ilipitia katika uti wake wa mgongo, mawakili wanasema.

Kupigwa risasi kwa Bwana Blake kumetibua maandamano na ghasia wakati mwingine. Gavana wa Wisconsin ametuma wanajeshi zaidi wa ulinzi wa kitaifa Kenosha.

Bwana Blake kwa sasa amepooza, na madaktari hawana hakika ikiwa atafanikiwa tena kutumia miguu yake

Tunachokijua kuhusu kisa cha kupigwa risasi kwa Jacob Blake

"Familia yake inaamini miujiza inaweza kutokea, lakini matokeo ya uchunguzi wa kimatibabu yanaonesha kwa sasa amepooza, kwasababu risasi hizo zilijeruhi uti wake wa mgongo, itakuwa miujiza kwa Jacob Blake Jr kutembea tena," wakili Ben Crump aliwaambia wanahabari siku ya Jumanne.

Mtu huyo aliye na miaka 29, alipigwa risasi mbele ya wanawe wa kiume waliokua ndani ya gari, aliachwa na mashimo ya risasi tumboni, kujeruhiwa mkono pamoja na figo na ini lake. Sehemu kubwa ya utumbo wake ulitolewa, mawakili wake waliwambia wanahabari.

Mama yake Julia Jackson aliwafahamisha wanahabari kwamba mwanawe "anapigania maisha yake", lakini angelijua kinachoendelea kwa sasa, maandamano na uharibifu, hangelifurahia hata kidogo".

Picha kutoka mji huo uliopo kilo mita 100,000 kusini magharibi mwa ufuo wa Ziwa Michigan zinaonesha majengo na magari yalioharibiwa kufuatia maandamano ya siku mbili nyakati za usiku kupinga ukatili wa polisi.

Siku ya Jumanne, Gavana Tony Evers alisema atawapeleka walinzi zaidi wa kitaifa mjini Kenosha kuchunguza majengo ya serikali na kuwapa ulinzi wazima moto. Hali ya hatari pia imetangazwa Wisconsin.

Tukio la kupigwa risasi kwa Bwana Blake limetokea wakati ambapo idara ya polisi nchini Marekani inakabiliwa na tuhuma za kuwanyanyasa Wamarekani weusi, huku suala la ubaguzi wa rangi likiendelea kuwa chanzo cha mgogoro katika jamii, tangu kifo cha Mmarekani mwingine mweusi mikononi mwa polisi mjini Minneapolis, George Floyd, mwezi Mei.

Katika taarifa yake, Bi. Jackson aliangazia moja kwa moja suala la ubaguzi wa rangi na kutoa wito wa "mshikamano".

Tunafahamu nini kuhusu tukio hilo?

Polisi wanasema kuwa walikuwa wakishughulikia mzozo wa kifamilia kabla ya kufika katika eneo la tukio siku ya Jumapili lakini hawakutoa maelezo zaidi. Kufikia sasa haijabainika ni nani aliyewapigia simu polisi, ni wangapi walihusika na tukio hilo, na nini kilichokea kabla ya Blake kupigwa risasi.

Kanda ya video ya tukio hilo inamuonesha Bwana Blake akifungua mlango na kisha kuegemea upande wa ndani hali ambayo ilimfanya polisi kumshika mashati na kuanza kumpiga risasi. Milio saba ya risasi inasikika katika video hiyo, huku walioshuhudia wakipiga mayowe.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Majumba yamechomwa moto wakati wa maandamano Kenosha

Mchumba wa Bw. Blake Laquisha Booker, alisema watoto - walioshuhudia kila kitu kilichotokea walikaa nyuma ya gari - wakipiga mayowe wakati baba yao anapigwa risasi.

Mawakili Blake wanasema alikuwa akijaribu "kuzuia kutokea kwa mzozo wa kinyumbani". Mashuhuda pia waliwaambia wanahabari mjini humo.

Rekodi ya Mahakama zinaonesha kulikuwa na Kigali cha wadi cha kumkamata Bw. Blake aliyeshitakiwa kwa unyanyasaji wa kimapenzi na mzozo wa kinyumbani.

Wisconsin inachunguza tukio la Kenosha, huku maafisa waliohusika wakipewa likizo ya lazima. Ombi linalowataka washitakiwe limetiwa saini na maelfu ya watu

Baba yake Bwana Blake amesema hana Imani na uchunguzi unaoendelea.

"Mzungu yeyote, anayefanya uchunguzi kuhusu kijana mweusi ambaye alipigwa risasi saba mgongoni, na ambaye hajapata jibu ama kuonesha juhudi za kupata jibu, haruhusiwi," aliwaambia wanahabari.