Human Rights Watch: Haki za kiraia Tanzania zinaminywa kuelekea uchaguzi

Katika ripoti yake Human Rights Watch limekosoa sheria mpya inayodhibiti maudhui

Chanzo cha picha, Human rights Watch

Maelezo ya picha,

Katika ripoti yake Human Rights Watch limekosoa sheria mpya inayodhibiti maudhui

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW) linasema mamlaka nchini Tanzania imeongeza hatua ya ukandamizaji dhidi ya vyama vya upinzani na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.

Katika ripoti yake Human Rights Watch limekosoa sheria mpya inayodhibiti maudhui likisema inazuia vyombo vya habari kuangazia masuala ya kisiasa na taarifa kuhusu janga la corona.

Shirika hilo linadai hatua hiyo ni ishara wazi kwamba serikali ya Tanzania imeongeza juhudi za ukandamizaji nchini inapoelekea uchaguzi wa Oktoba 28.

Ripoti hiyo pia imeangazia mlolongo wa matukio yaliyofanya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu THRDC kusitisha shughuli zake na kutoa mfano wa jambo hilo kama sehemu ya ukandamizwaji unaofanywa na serikali kwa mashirika ya kiraia.

Kuhusu suala la THRDC, hivi karibuni BBC ilifanya mahojiano na Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania Kamanda Simon Sirro ambaye alisema wanachunguza bilioni 6 za Tanzania zilizoingia katika akaunti yaTHRDC:

''Kitengo chetu kinachohusika na mambo ya fedha haramu baada ya ufuatiliaji tuligundua kuwa kweli kuna fedha zimeingia nyingi, ukianzia Januari 2019 mpaka sasa mwezi wa nane takriban bilioni sita zimeingia kwenye hiyo akaunti, ndio tukataka kujua kama fedha hizo ni haramu, kikubwa zaidi zisije zikawa zimekuja kwa nia ovu''

Aliongeza kuwa wamekusanya nyaraka zote za miamala ya hizo fedha na wanafanya mahojiano na kwa kwamujibu wa kanuni zilizopo ndani ya jeshi la polisi wanamamlaka ya kusimamisha akaunti zisifanye kazi kwa muda wa siku 14 wakati uchunguzi unaendelea.

''Baada ya uchunguzi ndio tutaweza kubaini iwapo ni kosa la jinai au hapana na tukiona kwamba kuna kosa la jinai tutapeleka mahakamani, lakini tukiona kwamba hakuna kosa la jinai basi tutafungua akaunti na wataendelea na shughuli kama kawaida''

Unaweza kusikiliza zaidi mahojiano na Kamanda Simon Sirro:

Maelezo ya sauti,

Simon Sirro: Tunachunguza bilioni 6 za Tanzania zilizoingia katika akaunti hiyo

Akizungumza kuhusu matukio kadhaa ya kuchomwa moto kwa ofisi za upinzani Bwana Siro alisema wanafanya uchunguzi na kuona kama matukio ni ya kupangwa au mtu fulani alifanya kwa nia gani: ''Wahusika watachunguzwa na iwapo watapatikana na hatia watapelekwa kwenye vyombo vya dola'', alisema.

Bwana Siro aliihakikishia BBC kuwa wameweka mikakati ya pamoja ya usalama kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa wa amani na utulivu.

Shutuma za kubana uhuru wa vyombo vya habari

Shirika hilo la Human Rights Watch pia limezungumzia suala mabadiliko ya kanuni za maudhui ya redio na televisheni juu ya ushirikiano baina ya vyombo vya habari vilivyosajiliwa Tanzania na mashirika ya utangazaji ya kimataifa.

Mashirika ya kutetea haki yanatafsiri hatua hiyo kama udhibiti wa maudhui ya vyombo vya habari.

Kufikia sasa serikali haijatoa taarifa yoyote kuhusu ripoti hiyo ya Human Rights Watch.

Hata hivyo katika mahojiano na BBC hivi karibuni na Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania TCRA, kupitia Mkurugenzi wake wa leseni na udhibiti Andrew Kisaka alisisitiza kwamba vyombo vya habari vya kimataifa havijapigwa marufuku kuendelea na ushirikiano na vyombo vya habari vya ndani ya Tanzania, lakini lazima wawasilishe stakabadhi za makubaliano yao kwa mamlaka hiyo.

''Tufahamu kwamba sisi kama mamlaka ya mawasiliano Tanzania tunatoa leseni kwa vituo vya utangazaji hapa nchini na vituo hivi vinatakiwa vizingatie maadili ya utangazaji, vifanye kazi zake kwa ueledi'', alisema.

Aliongeza kuwa: ''Kanuni ya 37 ya redio na televisheni ya mwaka 2018 imeeleza kwamba vituo vya utangazaji viko huru kurusha matangazo ya vituo vya utangazaji vilivyo nje baada ya kuwa na makubaliano ya kibiashara, lakini uzoefu unaonyesha kwamba vituo vya nje vinakosea navyo na vinapokosea linaloleta mushkeli kidogo kwani vinapokosea mapungufu hayo yanaonekana katika vituo vya ndani. Kwa hiyo anayeonekana ni huyu tuliyempa leseni lakini hapo hapo maudhui sio yake ameyatoa nje. Hakukosea yeye ni maudhui ambayo ameyatoa nje ambayo hayana ueledi'' alisema.

Alisema kuwa mamlaka ya mawasiliano inataka kuwepo kwa utaratibu wa kuweza kuwasiliana na vyombo vya habari vya nje, ili kama kuna marekebisho yafanyike.

Unaweza kusikiliza zaidi mahojiano ya BBC na Andrew Kisaka:

Maelezo ya sauti,

TCRA yatoa ufafanuzi kuhusu maudhui ya vyombo vya habari vya kimataifa