Mzozo mto Nile: Marekani kukata fungu la msaada kwa Ethiopia

Bwawa kubwa litakapomalizika litakuwa kubwa zaidi afrika kuzalisha umeme Afrika

Chanzo cha picha, Reuters

Marekani inaripotiwa kwamba imepunguza msaada wa Ethiopia wa dola milioni 100 kutokana na utata wa bwawa kubwa la uzalishaji umeme linalojengwa kutoka kwa kijito cha mto Nile.

Vyanzo vya serikali vimesema kwamba hilo limechochewa na hatua ya Ethiopia ya kuanza kujenga bwawa kabla ya kufikia makubaliano na Misri na Sudan.

Ethiopia imesema kwamba inataka bwawa hilo kwa mradi wa upatikanaji wa umeme.

Bwawa hilo likishamalizwa kujengwa, litakuwa kubwa zaidi katika uzalishaji wa umeme Afrika na kutoa huduma za umeme kwa hadi raia milioni 65 wa Ethiopia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, serikali ya Marekani itasimamisha ufadhili wake kwa Ethiopia unaokisiwa kuwa na thamani ya dola milioni 100. Dola milioni 26 kati ya ufadhili huo ni ufadhili unaomalizika mwisho wa mwaka huu wa fedha.

Ufadhili unaoathirika unahusishwa na lishe bora, usalama wa eneo na mipaka, ushindani wa kisiasa na ujenzi, afisa amesema. Ufadhili wa miradi inayohusishwa na ugonjwa wa ukimwi, uhamiaji, usaidizi kwa wakimbizi na mpango wa amani wa chakula pia utaathirika.

Afisa kutoka idara ya Marekani ameliambia shirika la Reuters kwamba uamuzi wa Ethiopia wa kaunza kujaza bwawa hilo wakati majadiliano na Misri na Sudan yanaendelea yameshusha uaminifu uliokuwepo kwenye mazungumzo na pia kumeathiria nia ya kujitolea kwa Ethiopia.

"Awali, Marekani ilionesha wasiwasi wake mara kadhaa kwamba kuanza kujaza bwawa hilo kabla ya hatua zote za kiusalama kuchukuliwa kunaongeza uwezekano wa kutokea kwa hatari kubwa," afisa huyo alisema.

Kilimo cha nchini Ethiopia kinategemea maji ya mto Nile

Chanzo cha picha, Getty Images

Balozi wa Ethiopia nchini Marekani ameliambia gazeti la Financial Times kuwa ni matumaini yake Marekani itabadili msimamo kuhusu hatua hiyo.

"Tumewaomba kufikiria tena uamuzi wao tunasubiri. Ni matumaini yetu kwamba uhusiano wa kidiplomasia wa miaka 117 hautaathirika kwasababu ya suala ambalo halina uhusiano wowote na nchi hizi mbili," Fitsum Arega amesema.

Wanahabari wanasema hatua hiyo kwa kiasi kikubwa inaweza kuonekana kama hatua ya Rais Donald Trump kuishinikiza Ethiopia baada ya nchi hiyo kukataa mazungumzo na Misri na Sudan.