Kijana Matayo Kudenya aliyetaabika kwa muda mrefu apata msaada wa kutolewa tende ya korodani Tanzania

  • Aboubakar Famau
  • BBC Swahili
Matayo Kudenya

Matayo Kudenya, kijana aliyekuwa akisumbuliwa na tatizo la tende ya korodani , hatimae amepata msaada wa kufanyiwa upasuaji bila gharama kwa udhamini wa hospitali ya Decca iliyopo jijini Dodoma.

Jopo la madaktari bingwa wanne, madaktari wawili wa usingizi wawili na wauguzi wawili wameshiriki katika upasuaji huo ambao umechukua jumla ya saa tatu na dakika arobaini na tano na kufanikisha kuondoa uvimbe wa kilo 25 zilizokuwa katika korodani ya Matayo.

DKt Martin Singani ndie aliyekuwa daktari kiongozi wengine wakiwa ni Dkt Gustavus Deusdedith, Dkt. Charles Abeid na Dkt Ambilikisye Kajange

Dkt Gustavus Deusdedith, mmoja wa madaktari amemwambia mwandishi wetu Aboubakar Famau kwamba mgonjwa anaendelea vizuri.

Video ya wito uliotolewa na Kudenya akizungumza na BBC

Maelezo ya video,

Ngiri maji yenye uzito wa kilo 20 yavunja ndoto ya mkulima Tanzania

Daktari amesema, katika uchunguzi wao wa kitaalamu, wamebaini kuwa Matayo, alisumbuliwa na matende kama ya juu ya mguuni na sio ngiri maji kama alivyoeleza mwenyewe hapo awali.

Kwa upande wake, Steven John ambae ni mjomba wa Matayo amesema, ameguswa sana na msaada huo ana anashukuru sana.

"Sina la kusema kwa msaada huu. Machozi yananitoka," amesema John.

Kutokana na ukubwa wa upasuaji wake, Matayo aliwekewa chupa 15 za maji na tatu za damu

Itambukwa kuwa, BBC ndio iliyorusha taarifa za Matayo akiomba kusaidiwa, hivyo kupelekea kupata msaada huo.

Wataalamu wanasema inaweza kumchukua Matayo kuanzia siku 10 mpaka 14 kupona.