Virusi vya corona: Tunayoyafahamu kuhusu mmea wa artemisia unaotumiwa na Madagascar

  • Na Peter Mwai
  • BBC Reality Check
Mmea wa artemisia umekuwa muhimu sana katika kudhibiti malaria

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mmea wa artemisia umekuwa muhimu sana katika kudhibiti malaria

Madagascar iliwavutia wengi na kuangaziwa sana Aprili taifa hilo lilipotangaza kwamba lilikuwa limevumbua dawa ya corona kutoka kwa mmea.

Dawa hiyo iliyokuwa imeandaliwa kama kinywaji ilitengenezwa kwa kutumia mmea wa artemisia, na rais Andry Rajoelina aliipigia debe sana.

Kufikia sasa bado hakuna ushahidi kwamba mmea huo - ambao kemikali zake huweza kudhibiti malaria - unaweza kutibu Covid-19, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO). 

Tunafahamu nini kufikia sasa kuhusu mmea huu na nguvu zake?

Mmea huu unatoka wapi?

Mmea huo kwa jina kamili huitwa Artemisia annua na asili yake ni bara Asia, lakini hukuzwa katika maeneo mengi duniani yenye joto na jua.

Mmea huu umekuwa ukikuzwa katika baadhi ya mataifa ya Afrika mashariki zikiwemo Kenya na Tanzania.

Mmea huu umetumiwa kama tiba ya kiasili nchini China kwa zaidi ya miaka 2,000 kutibu magonjwa mengi, ukiwemo ugonjwa wa malaria. Hutumiwa pia kupunguza maumivu na kudhibiti homa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mimea ya Artemisia ikikuzwa Madagascar

Nchini Uchina, mmea huo hufahamika kama "qinghao."  

Kwa Kiingereza huitwa sweet wormwood au annual wormwood, na baadhi ya watu wamekuwa wakiutumia kwa sababu mbalimbali kama tiba, na hata kuongezwa kwenye vinywaji.

Artemisia inaweza kudhibiti Covid-19?

Rais Rajoelina wa Madagascar mwezi Aprili mwaka huu alisema majaribio yalikuwa yamefanyiwa tiba ya Covid-Organics iliyotengenezwa kwa kutumia mmea huo na kwamba majaribio hayo yalionesha mafanikio.

Alirudia madai hayo mwezi huu wa Septemba.

Lakini taifa lake halijatoa ushahidi wowote wa kisayansi hadharani kuthibitisha madai hayo.

Aidha, viungo halisi vilivyo kwenye dawa hiyo ya kinywaji kwa jina Covid-Organics havijulikani hasa, ingawa serikali ilisema 60% inatokana na mmea wa artemisia annua.

Kiwango hicho kingine kinatokana na mimea mingine ya kiasili.

Madagascar pia imekuwa ikitengeneza tembe za Covid-Organics na hata dawa ya kudungwa kwa kutumia sindano. Rais Rajoelina anasema majaribio ya hiyo ya dawa ya kuchomwa mwilini kupitia sindano yanaendelea.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rais Andry Rajoelina anasema dawa hiyo inafanikiwa dhidi ya Covid-19

Wanasayansi kutoka Ujerumani na Denmark wamekuwa wakifanyia majaribio kemikali kutoka kwa mimea ya artemisia annua, na walisema mmea huo ulionyesha mafanikio dhidi ya virusi vya corona kwenye maabara.

Utafiti huo - ambao haujahakikiwa na wanasayansi wengine - ulibaini kwamba kemikali za mmea huo zilionyesha sifa za kukabiliana na virusi hivyo zilipotolewa kwa mmea huo kwa kutumia maji au kilevi.

Watafiti hao kwa sasa wanafanya kazi kwa pamoja na Chuo Kikuu cha Kentucky kufanyia majaribio mmea huo kwenye binadamu.

China pia imekuwa ikiufanyia majaribio mmea huo.

Na nchini Afrika Kusini, kuna wanasayansi wanaofanyia majaribio mmea wa artemisia annua na mmea mwingine unaokaribiana sana na huo - artemisia afra - kubaini iwapo unaweza kufanikiwa kutibu Covid-19. Utafiti huo unafanyika katika maabara lakini hakuna matokeo yoyote yaliyotolewa kufikia sasa.

WHO wanasema nini kuhusu artemisia?

WHO wanasema kufikia sasa hawajapokea taarifa zozote kuhusu majaribio yaliyofanywa na Madagascar kuhusu matumizi ya Covid-Organics dhidi ya virusi vya corona.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Maelezo ya picha,

Madagascar inasema imesambaza Covid-Organics kwa takriban watu 7 milioni

Jean-Baptiste Nikiema kutoka WHO kanda ya Afrika aliambia BBC kwamba shirika hilo huenda likahusika katika hatua za baadaye za majaribio ya dawa hiyo.

Lakini hilo litategemea habari watakazozipokea kuhusu majaribio ya awali.

Lakini kwa sasa WHO wanasisitiza kwamba hakuna ushahidi wowote kwamba dawa zinazotokana na artemisia hufanikiwa dhidi ya Covid-19.

Shirika hilo linaongeza kuwa tiba zote za miti shamba "zinafaa kuchunguzwa kubaini uwezo wake na madhara" kupitia majaribio yaliyofanywa kwa njia ya kisayansi.

Mmea huu unatumiwaje dhidi ya malaria?

Kemikali iliyo ya nguvu hutolewa kwenye majani yaliyokaushwa ya artemisia annua na hufahamika kama artemisinin. Kemikali hii ndiyo inayotibu malaria.

Wanasayansi nchini Uchina waligundua nguvu za kemikali hiyo wakati wakitafuta tiba ya malaria miaka ya 1970.

Dawa zinazotumia Artemisinin kwa pamoja na kemikali nyingine, kwa kifupi ACTs, hupendekezwa na WHO kutumiwa dhidi ya malaria, ikiwa ni pamoja na aina ya viini vya malaria vilivyo sugu dhidi ya chloroquine.

Afrika, mataifa mengi huanza kwa kutumia Sulfadoxine pyrimethamine au Amodiaquine kutibu mgonjwa wa malaria kwanza na zikishindwa basi ACTs hutumiwa.

ACTs huwa na aina moja au nyingine ya artemisinin (aina kuu ni artesunate, artemether na dihydroartemisinin) na kemikali nyingine. Aina ya artemisinin hupunguza sana viini vya malaria katika siku tatu za kwanza na kisha kemikali hiyo nyingine huvimaliza viini vilivyosalia.

Upatikanaji wa ACTs kwa wingi katika mataifa yaliyoathiriwa sana na malaria umetajwa kama moja ya sababu kuu za kupungua pakubwa kwa watu wanaouawa na malaria duniani katika miaka 15 iliyopita.

Hatari ya viini kuwa sugu

Kwa kuwa viungo kutoka kwa artemisia annua vimekuwa vikitumiwa sana kwenye tiba za kiasili za malaria, kwa mfano kuongezwa kwenye chai, kuna wasiwasi kwamba matumizi haya yasiyodhibitiwa ya mmea huyo yanaweza kusababisha viini vya malaria kuwa sugu dhidi ya dawa za ACTs.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Viini vya malaria vimeanza kuwa sugu dhidi ya baadhi ya dawa

Yapo mataifa kadha kusini mashariki mwa bara Asia ambapo viini vya malaria vimebainishwa kuanza kuwa sugu dhidi ya artemisia.

"Tunafahamu kuwa baada ya muda, viini hivi (vya malaria), vitaanza kuwa sugu, lakini kipindi hicho kinafaa kuwa mbali sana kadiri iwezekanavyo," anasema Jean-Baptiste Nikiema kutoka WHO.

WHO kwa sasa huhimiza watu kutotumia aina za artemisinin kwenye tiba za kiasili au kwenye vinywaji, wasiwasi ukiwa kwamba hilo litachangia viini vya malaria kuwa sugu dhidi ya dawa za ACTs.