Uchaguzi Tanzania 2020: Nani atahesabu kura yako katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu?

  • Ezekiel Kamwaga
  • Mchambuzi
Upigaji kura

Wiki moja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya mwaka 2017, aliyekuwa Mkuu wa Idara ya TEHAMA ya Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC), Christopher Chege Msando, alizungumza na kituo cha televisheni cha KTN nchini humo na kuahidi uchaguzi ulio huru na kwamba kila kura itahesabiwa.

Msando alikiambia kituo hicho kwamba hakutakuwa na yeyote mwenye uwezo wa kuvuruga uchaguzi huo kwa vile mifumo yote ya kuhesabu kura ilikuwa iko vizuri na kuwa ndani ya IEBC kuna mtu mmoja tu mwenye nywila (password) ya kuona upigaji kura unavyoendelea.

Siku mbili baadaye, Agosti 2, 2017, Msando alitoweka. Siku iliyofuata, mwili wake ulikutwa ukiwa umetupwa vichakani pamoja na wa msichana mwanafunzi wa udaktari aliyekuwa na urafiki. Wote walikutwa wamekufa.

Uchunguzi wa maiti uliofanywa ulibaini kwamba Msando alikufa kwa kunyongwa na pia mkono wake ulikutwa ukiwa umetobolewa kwa mateso. Kiongozi wa Upinzani wa Kenya, Raila Odinga, alikuja kutamka baadaye kwamba kilichomponza Msando kilikuwa ni hiyo nywila aliyoitangaza.

Kama kuna fundisho kubwa katika kifo cha Msando wa Kenya, kitu hicho ni kwamba katika mfumo wa sasa wa uhesabuji kura kwa njia ya kompyuta, watu muhimu zaidi katika mchakato mzima wa uchaguzi kokote duniani, si wapiga kura bali wale wanaodhibiti mfumo wa uhesabuji kura.

Kauli ya Joseph Stalin

Mmoja wa viongozi mashuhuri wa Jamhuri ya Umoja wa Nchi za Kisovieti (Urusi), Joseph Stalin, alipata kusema huko nyuma kwamba; " Inatosha kwa wananchi kuona kwamba wameshiriki kuchagua viongozi wao. Hata hivyo, kura zao haziamui chochote kwani anayeamua ni yule anayehesabu hizo kura".

Ingawa kauli hiyo ilitolewa takribani karne moja iliyopita, hadi leo hii, hakuna mtu anayeweza kubisha ukweli na uhalisi wa kauli hiyo duniani. Katika miaka ya karibuni, kauli hii imekuwa na mashiko hata katika nchi zilizoendelea.

Kama taifa kubwa kama Marekani kuna watu wanalalamika kwamba Uchaguzi Mkuu uliopita wa taifa hilo wa mwaka 2016 ulivurugwa na Russia kwa kiasi kikubwa, ni wazi kwamba hakuna nchi inayoweza kujidai iko sawa na wale 'wanaohesabu kura'.

Nani anahesabu kura yako Tanzania?

Kwa walau miaka 50 baada ya Uhuru wake, Watanzania walikuwa wakipiga kura kwa kutumia karatasi na mara zote kura zilihesabiwa kwa njia ya mkono na matokeo kubandikwa vituoni.

Mfumo wa uchaguzi wa Tanzania una namna mbili; chaguzi zinazosimamiwa na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na ule unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

NEC husimamia Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wakati Tamisemi chaguzi katika ngazi ya Serikali za Mitaa. Kumekuwa na matakwa ya kutaka chaguzi zote ziwe chini ya NEC lakini hadi sasa hali iko hivyo ilivyo.

Mabadiliko ya kiteknolojia yaliyoingia katika karne hii mpya, yameifanya Tanzania nayo kuanza kutumia kompyuta kwenye kutunza taarifa za wapiga kura, kuhesabu kura na kuzijumuisha kwa ajili ya kutoa matokeo ya mwisho.

Katika miaka ya nyuma kabla ya kuingia kwa matumizi ya Tehama katika chaguzi, watu walikuwa wakipiga kura na zikihesabiwa kwa njia ya mkono. Kazi ya vituo ilikuwa ni kuhakikisha matokeo hayo yanafikishwa -kwa mkono katika ngazi za wilaya, mkoa na kisha kufikishwa NEC Taifa.

Wakati huo, watu waliopewa kazi ya kuhesabu kura ni wasimamizi katika vituo na wale tu waliopewa mamlaka ya kufanya hivyo kupitia sheria za nchi. Kwa sababu wengi wa hawa walikuwa ni waajiriwa wa serikali, mara zote; katika uchaguzi wa namna hii, mwenye faida alikuwa ni mgombea wa chama tawala.

Kupitia mfumo wa kompyuta, matokeo sasa yanaweza kutumwa kama yalivyo kwa njia ya mtandao na kupitia katika mifumo maalumu ya kuhifadhia taarifa (servers) na kujumlishwa huko.

Matumizi ya TEHAMA yamesaidia kufupisha muda wa kupatikana kwa matokeo na kupunguza pia tabia ya watu kukimbia na maboksi ya kuhesabu kura au kujaza kura za watu ambao hawakushiriki kupiga kura au si wapiga kura halali lakini kura zao zinapigwa isivyo halali.

Katika dunia ya zamani, upenyo wa kuiba na kuvuruga mchakato wa kura ulikuwa katika hatua ya kupiga na kuhesabu kura katika ngazi za chini. Katika dunia ya TEHAMA, watu wanaweza kupiga kura kwa uhuru na uwazi, lakini matokeo yakaja tofauti kwa sababu ya uvurugaji unaofanyika katika ngazi za juu.

Kwa hiyo, katika dunia ya sasa, hata katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka huu, mtu anayehesabu kura yako si lazima awe yule unayemuona wakati ukipiga kura yako - anaweza kuwa mtu ambaye yuko zake San Francisco, Nairobi au hata Paris.

Kilichotokea katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka 2015

Katika historia ya Tanzania, hakuna uchaguzi ambao vyama washindani' Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), viliwekeza katika eneo la TEHAMA kuliko ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Aliyekuwa mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa, alikuwa mwanasiasa mbobevu aliyejua mizungu yote ya kisiasa. Katika uchaguzi ule, si kwamba alikuwa na timu ya washauri wa masuala ya TEHAMA katika uchaguzi, lakini pia alihakikisha Chadema iliyokuwa vinara wa vyama vilivyoungana kuunda ulioitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ilikuwa na vituo vya kuhakikisha kura zake hazipotei hewani.

CCM nayo haikuwa imelala katika eneo hilo. Miezi michache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, mmoja wa magwiji wa mifumo ya TEHAMA nchini, Dk. Modestus Kipilimba, alihamishiwa NEC kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kushika nafasi inayofanana na ile aliyokuwa akiifanya Msando katika Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya.

Mmoja wa marafiki zangu aliyekuwa mmoja wa mawaziri katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, ndiye aliyenipa kwanza taarifa za Kipilimba kuhamishiwa NEC na akaniambia uamuzi ule ulimaanisha kwamba "Uchaguzi Umekwisha".

Siku chache baada ya upigaji kura, baadhi ya vituo vya uhesabuji matokeo (tallying centres) vilivyowekwa na Chadema vilivamiwa na watumishi wa dola katika zoezi lililoelezwa kuwa lilihitimisha uchaguzi ule.

Hadi mwaka jana, kuna viongozi wa Chadema waliwahi kuniambia kwamba kama vituo vyao vile vya kupokea matokeo visingevamiwa na kufungwa, chama chao kingeibuka na ushindi katika uchaguzi ule uliomwingiza madarakani Rais John Magufuli.

Hadi leo, hakuna taarifa rasmi ya hasa nini kilitokea katika siku za mwisho za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 lakini kilicho wazi ni kwamba vyama vyote viwili; Chadema na CCM, vilikuwa vinajua namna ya kushinda uchaguzi kwa kutumia TEHAMA.

Suluhisho ni Tume Huru na si Kompyuta

Changamoto kubwa ambayo Tanzania na nchi karibu zote duniani zinapitia kwa sasa ni kwenye kuhakikisha ni kwa namna gani chaguzi zinafanyika kwa kutumia teknolojia za kisasa lakini wakati huohuo zikijilinda kuhakikisha matokeo hayaingiliwi na taasisi za au mataifa ya nje.

Hasara mojawapo ya mifumo yote inayotegemea TEHAMA kujiendesha ni kwamba kuna wadukuzi (hackers) wanaoweza kufanya chochote kuifanya ifanye mambo ndivyo sivyo. Kuna hatari kubwa kwamba huko mbele ya safari kunaweza kuwa na chaguzi za Tanzania lakini atakayeshinda ni mtu anayetakiwa na Slovenia, China, India na nchi nyinginezo.

Hata hivyo, pamoja na changamoto hizi za kiteknolojia, jambo lililo wazi ni kwamba hata kama Stalin alisema wapiga kura si lolote wala chochote mbele ya wanaohesabu, uwepo wa Tume Huru za uchaguzi katika nchi mbalimbali za Afrika umeweza kuleta mabadiliko.

Katika nchi kubwa kama Nigeria, wananchi waliweza kubadili serikali zao kupitia njia ya kura. Katika nchi kama Gambia, utawala wa Yahya Jammeh, uliondolewa kupitia sanduku la kura.

Kwa hiyo, pamoja na matatizo yote ya mifumo ya kuhesabu kura na changamoto za teknolojia, bado wananchi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla wana nafasi ya kubadili mambo kupitia demokrasia ya uchaguzi.

Na kama wakiangalia huku na kule wanaona changamoto lukuki, mahala ambapo Tanzania inaweza kuanzia kwa kuhakikisha kura za wananchi zilizopigwa zina maana yoyote kwenye kupata viongozi - ni kwenye kuhakikisha kuna Tume Huru ya Uchaguzi.

Lakini, pasipo Tume Huru na pasipo na uhakika wa nani hasa anahesabu kura za watu, bado wananchi wana wajibu wa kupiga kura kupata viongozi wengine. Yako maeneo ndani ya Tanzania ambako watu wamewapata viongozi waliowataka kwa kutumia kura zao.