Breonna Taylor: Maafisa wawili wa polisi wapigwa risasi wakati wa maandamano mjini Louisville

Police nje ya makoa makuu ya mji wa Louisville

Chanzo cha picha, Reuters

Maafisa wawili wa polisi wamepigwa risasi huku maelfu ya watu wakiandamana katika mji wa Louisville baada ya jopo la mahakama kuamua kwamba hakuna mtu atakayeshtakiwa na mauaji ya Breonna Taylor.

Bi Taylor , mwenye umri wa miaka 26 , mfanyakazi mmoja wa hospitali alipigwa risasi mara kadhaa baada ya maafisa wa polisi kuvamia nyumba yake tarehe 13 mwezi Machi.

Brett Hankison ameshtakiwa, sio kwa kifo cha Taylor lakini kwa kuhatarisha maisha baada ya kufyatua risasi katika nyumba ya jirani yake huko Louisville.

Maafisa wengine wawili hawakushtakiwa.

Naibu afisa mkuu wa polisi Robert Schroeder amesema kwamba hali ya maafisa hao haipo hatarani . Aliongezea kwamba mmoja ya washukiwa amekamatwa. Hali ya tahadhari imetangazwa mjini Louisville na walinzi wa kitaifa pia wamepelekwa katika eneo hilo.

Meya Greg Fischer ameweka masharti ya kutotoka nje katika mji huo kwa siku tatu. Awali alikua amesema kwamba ametangaza hali ya tahadhari kutokana na uwezekano wa kuzuka wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Chanzo cha picha, Facebook

Maelezo ya picha,

Bi Taylor, alikuwa afisa wa kiufundi wa matibabu alifariki akiwa na umri wa miaka 26

Je mwendesha mashtaka alisema nini?

Chini ya sheria ya Kentucky, mtu hupatikana na hatia ya kutaka kusababisha hatari ya mtu mwengine iwapo atatekeleza kitendo kinachoonyesha , kwamba haoni thamani ya maisha ya mtu mwengine.

Kosa hilo dogo linaweza kumfanya mtu kupewa hukumu ya hadi miaka mitano kwa kila kosa.

Brett Hankison alishtakiwa kwa mashtaka matatu.

Ndugu za bi Taylor ambao wametumia kifo chake kulalamikia mauaji yake walikuwa wamewataka maafisa hao watatu ambao wote ni wazungu kushtakiwa kwa mauaji ya bila kukusudia.

Lakini hilo lilikataliwa na jopo la mahakama ambalo lilichunguza ushahidi.

Siku ya Jumatano , jaji Annie O' Connell alitangaza mashtaka ambayo yalikuwa yamewasilishwa dhidi ya bwana Hankison.

Mwanasheria mkuu katika jimbo la Kentucky bwana Cameron alifanya kikao na vyombo vya habari ambapo alielezea uamuzi huo.

''Hii ni kesi yenye hisia chungu nzima, alisema. ''Hakuna kitu ambacho mnaweza kuwapatia hii leo ili kuondoa majonzi na uchungu wa moyo baada ya kumpoteza mwanao, mpwa , dada na rafiki'', aliongezea katika ujumbe kwa failia ya bi Taylor.

Bwana Cameron alisema kwamba ripoti ya mauaji yake imebaini kwamba risasi sita ziliingia katika mwili wa bi Taylor, lakini moja tu ndio iliomuua. Uchambuzi huo ulihitimisha kwamba afisa wa polisi Myles Cosgrove alifyatua risasi iliomuu bi Taylor.

Mwanasheria mkuu alisema kwamba haikuwa wazi iwapo risasi za bwana Hankison zilimpiga bi Taylor , lakini zilipiga nyumba moja jirani.

Maelezo ya video,

Protesters march in Louisville following the grand jury decision

Mwendesha mashtaka mkuu alisema kwamba maafisa wegine wawili -Jonathan Mattingly na bwana Cosgrave walikuwa na haki ya kujilinda mbali na kwamba sheria zinawalinda dhidi ya kuwawekea mashtaka ya uhalifu.

Bwana Cameron, mwanachama wa Republican ambaye ndie mwanasheria wa kwanza mweusi aliongezea: Iwapo tutafanya uamuzi kutokana na hisia hakuna haki. Kupigwa na watu wengine sio haki. Haki inayotafutwa kupitia ghasia sio haki ni kisasi .

Aliongezea kwamba shirika la FBI bado linaendelea kuchunguza ukiukaji wa haki za jimbo hilo katka kesi hiyo.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

The National Guard were deployed in Louisville ahead of the announcement

Je uamuzi huo umepokelewaje?

Ben Crump, wakili wa ngazi za juu kwa familia ya bi Taylor amesema kwamba uamuzi huo ni wa ''kukasirisha na kukera ".

Maafisa mwezi huu walikubaliana kuilipa familia yake $12m (£9.3m) kupitia makubaliano. Alipoulizwa kuhusu uamuzi huo rais Donald Trump alisema kwamba ''nilidhani ulikuwa mzuri sana''.

Alimpongeza mwanasheria mkuu wa jimbo la Kentucky ambaye alihutubia mkutano mkuu wa chama cha Republican mwezi uliopita , ''kwa kufanya kazi nzuri sana''.

''Nadhani yeye ni nyota'', alisema akiongezea kwamba aliidhinisha uamuzi huo wa gavana wa jimbo la Kentucky kutuma walinzi wa kitaifa katika eneo hilo.

Ni nini kilichomtokea bi Taylor?

Muda mfupi baada ya saa sita usiku siku ya Ijumaa tarehe 13 mwezi Machi , alikuwa kitandani na mpenzi wake , Kenneth Walker wakati waliposikia mlango ukigongwa nje.

Maafisa wa polisi wa eneo la LouisVille waliokuwa wamevalia nguo za raia walikuwa wakifanya msako wa dawa za kulevya hivyobasi walitumia kifaa cha mbao ili kugonga mlango huo ili kuingia ndani.

Jaji mmoja alikuwa ametoa agizo kwa maafisa wa polisi kufanya msako ndani ya nyumba ya bi Taylor kwasababu uchunguzi ulimshuku mpenzi wake wa zamani Jamarcus Glover kuwa mlanguzi wa mihadarati - na kwamba alikuwa anatumia anwani hiyo kupokea dawa hiyo.

Bi Taylor hakuwa na rekodi yoyote ya uhalifu.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Watu waandamana kufuatia uamuzi wa kesi ya uhalifu dhidi ya maafisa wa polisi iliohusu kifo cha Breonna Taylor

Bwana Walker ambaye anamiliki leseni ya bunduki , baadaye aliwaambia maafisa wa polisi kwamba alidhania kwamba mvamizi huyo wa usiku alikuwa bwana Glover, kulingana na gazeti la The New York Times.

Maafisa wanasema kwamba risasi ya bwana Walker ilimpiga afisa wa polisi , Jonathan Mattingly mguuni na kumpatia jeraha ambalo baadaye lilihitaji upasuaji . Maafisa wengi watatu walifyatua risasi 32 ili kujibu kulingana na ripoti hiyo ya uchunguzi kutoka kwa FBI.

Bi Taylor ambaye pia alikuwa ameamka kitandani kufuatia vurumai hiyo pia alipigwa risasi na kufariki nyumbani kwake.

Kulingana na ripoti ya ukamataji , maafisa wa polisi walikuwa wamepatiwa idhini ya kutobisha hodi iliowaruhusu kuingia katika nyumba hiyo bila onyo.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Hakuna dawa za kulevya zilizopatikana katika nyumba hiyo, ijapokuwa mwendesha mashtaka wa kaunti ya Jefferson Thomas Wine anasema kwamba msako huo ulifutiliwa mbali baada ya shambulio hilo la risasi.

Lakini bwana Cameron alisema siku ya Jumatano kwamba maafisa hao hawakuwa na agizo kama hilo .

Mwanasheria mkuu alisema kwamba taarifa ya maafisa kwamba walijitambulisha inathibitishwa na shahidi huru. Baadhi ya majirani waliviambia vyombo vya habari katika eneo hilo kwamba hawakuwasikia maafisa hao wakijitambulisha.

Hakuna dawa za kulevya zilizopatikana katika nyumba hiyo, ijapokuwa mwendesha mashtaka wa kaunti ya Jefferson Thomas Wine anasema kwamba msako huo ulifutiliwa mbali baada ya shambulio hilo la risasi.

Ripoti hiyo ya maafisa wa polisi ilikuwa na dosari ikiwemo madai kwamba bi Taylor hakuwa na jeraha na kusema kwamba polisi hawakutumia nguvu kuingia licha ya kwamba kifaa hicho cha mbao kinachotumiwa kuvunja mlango na polisi kilitumika .

Bi Walker awali alikuwa ameshtakiwa kwa kutekeleza jaribio la mauaji ya afisa wa polisi lakini kesi dhidi yake ilifutiliwa mbali mnamo mwezi Mei kufuatia uchunguzi wa kesi hiyo.

Chanzo cha picha, LMPD

Maelezo ya picha,

Kutoka kushoto: Brett Hankison, Jonathan Mattingly na Myles Cosgrove